Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mkuu wa WFP akutakana na Papa Francis wajadili kuhusu njaa na amani duniani

Picha ya mwaka 2019 ikionesha wanawake wakiwa wamebeba msaada wa chakula walioupata kutoka WFP katika eneo la Thaker, jimbo la Unity, Sudan Kusini. Mwaka huu mafuriko katika maeneo kadha ya Sudan Kusini yameilazimu WFP kupeleka tena msaada wa chakula
WFP/Gabriela Vivacqua
Picha ya mwaka 2019 ikionesha wanawake wakiwa wamebeba msaada wa chakula walioupata kutoka WFP katika eneo la Thaker, jimbo la Unity, Sudan Kusini. Mwaka huu mafuriko katika maeneo kadha ya Sudan Kusini yameilazimu WFP kupeleka tena msaada wa chakula

Mkuu wa WFP akutakana na Papa Francis wajadili kuhusu njaa na amani duniani

Msaada wa Kibinadamu

Hii leo jijini Roma nchini Italia Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula duniani WFP Cindy McCain amefanya mazungumzo ya faragha na Kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani Papa Francis wakijadili kuhusu uhitaji wa dharura wa kushughulikia changamoto ya upatikanaji wa chakula pamoja na changamoto nyingine za kibinadamu zinaikabili dunia. 

Tweet URL

Taarifa kutoka WFP imesema katika mazungumzo hayo Bi.McCain alimshukuru Papa Francis kwa mchango wake wa kupaza sauti kuzungumzia suala la njaa duniani na wale walio katika mazingira magumu. 

“Alisisitiza jukumu la kipekee la Mtakatifu Papa Francis analoweza kufanya katika kuchagiza amani, kuzuia mizozo inayosukuma mamilioni ya watu katika njaa kila mwaka, na kwamba katika ulimwengu ulio na mgawanyiko mkubwa, chakula kinaweza kuwa nguvu inayowaunganisha.” Imesema sehemu ya taarifa hiyo. 

Mkuu huyo wa WFP pia alizungumzia changamoto wanayokabiliana nayo ya ufadhili ambayo imesababisha shirika hilo kupunguza usaidizi katika maeneo kama Sudan Kusini, Jamhuri ya Kidemokrasia Kongo DRC, Syria, Jordan, Afghanistan, Bangladesh, Haiti na nyingine nyingi. 

“Bi.McCain amemueleza Papa Francis kuwa maamuzi haya ya kuvunja moyo ambayo WFP inalazimika kufanya kila siku ni kutokana na uhaba wa fedha, rasilimali kupangiwa majukumu mengine ya kuwalisha na kuwasaidia wenye njaa.”

Viongozi hao wawili pia walizungumzia umuhimu wa kutafuta majawabu ya changamoto hizo.

Makadirio ya WFP yanaonesha zaidi ya watu milioni 345 wanakabiliwa na njaa mwaka huu 2023 ikiwa ni ongezeko la takriban watu milioni 200 tangu mwaka 2020.

Mwaka 2016 Papa Francis alitembelea ofisi za Makao Makuu ya WFP ambayo yapo jijini Roma nchini Italia na alitoa msaada wake na kuwatia moyo katika juhudi zao za kufikia ulimwengu usiokuwa na njaa.