Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mtoto Claire Gakii kutoka Kenya ashinda tuzo ya UPU kuhusu usalama barabarani

Makutano ya barabara yenye shughuli nyingi.
UN Road Safety Fund
Makutano ya barabara yenye shughuli nyingi.

Mtoto Claire Gakii kutoka Kenya ashinda tuzo ya UPU kuhusu usalama barabarani

Utamaduni na Elimu

Mtoto wa kike Claire Gakii mwenye umri wa miaka 13 kutoka Kenya ameshinda tuzo ya shindano la kimataifa la 52 la Shirika la posta duniani- UPU la uandishi wa barua lililotaka watoto kumwandikia barua mtu fulani na kueleza atahitaji nguvu gani za kiajabu kufanikisha lengo la kufanya barabara kuwa salama kwa watoto. 

Tweet URL

Katika shindano hilo lililo andaliwa kwa ushirikiano wa Mfuko wa Umoja wa Mataifa wa Usalama Barabarani na UPU, Claire ameibuka mshindi kati ya barua za watoto milioni 1.7 zilizowasilishwa kutoka nchi 35 na amekabidhiwa tuzo hiyo hii leo huko Riyadh, Saudi Arabia ambapo kumefanyika mkutano wanne wa UPU, na kabla ya Siku ya Posta Duniani.

Nukuu ya barua yake 

Katika shindano la mwaka huu watoto walitakiwa kueleza watahitaji nguvu gani kufanikisha barabara kuwa salama kwa watoto

Claire katika barua yake alisema pamoja na mambo mengine atashirikiana na maafisa wa usalama, kuelimisha watoto pamoja na utungaji wa sera za kulinda watoto na kuhakikisha zinatekelezwa. 

“Nitafanya kazi mkono kwa mkono na mafias wa usalama barabarani kuwa fundisha watoto jinsi ya kutumia barabara na sababu za njia za watembea kwa miguu, Nitatengeneza sera za kuliwanda watoto na kuhakikisha sera hizo zipo wazi kuonekana na zinatekelezwa. (……..) Naamini kwamba kama sote tukifanya kazi pamoja, tutaweza kuleta mabadiliko katika maisha ya watoto na kusaidia kuzuia ajali barabarani.”

Jukumu la wote 

Akizungumza katika hafla hiyo Mkurugenzi Mkuu wa UPU Masahiko Metoki amegusia jambo lililoangaziwa na watoto wengi katika barua zao nalo ni “Hatutaweza kutegemea nguvu zisizo za kawaida ili kuhakikisha kuna usalama barabarani.” 

Metoki amegusia barua ya mshindi akisema kama jamii itafanya kazi pamoja inaweza kufikia dhamira muhimu ya kuwa na barabara salama “Kwakweli nguvu kuu za Claire, ni hatua ambazo hata watu wa kawaida wanaweza kuchukua.”  Akizungusia hatua kama kufanya kazi kutoa elimu kwa watoto, ushirikishwaji wa jamii na utungaji sera.

Mshindi wa pili katika shindano hilo ni Matilde Magalhães Da Silva mwenye umri wa miaka 11 kutoka Ureno, huku Dao Khuong Duy mwenye umri wa miaka 12 kutoka Vietnam akiibuka mshindi wa tatu.