Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Bahari ya mediterania imekuwa makaburi kwa watoto na ndoto zao za baadaye

Vijana wahamiaji wasioambatana na wazazi wao wanasubiri kuhamishwa hadi kwenye kituo cha mapokezi huko Lampedusa, Italia, baada ya kuvuka Bahari ya Kati ya Mediterania.
© UNICEF/Niccolò Corti
Vijana wahamiaji wasioambatana na wazazi wao wanasubiri kuhamishwa hadi kwenye kituo cha mapokezi huko Lampedusa, Italia, baada ya kuvuka Bahari ya Kati ya Mediterania.

Bahari ya mediterania imekuwa makaburi kwa watoto na ndoto zao za baadaye

Wahamiaji na Wakimbizi

Zaidi ya watoto 11,600 walivuka kupitia bahari ya Kati ya Mediterania hadi nchini Italia bila ya kuambatana na wazazi au walezi kati ya mwezi Januari mpaka katikati ya mwezi Septemba 2023 limesema leo shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF.  

Mkurugenzi wa UNICEF Kanda ya Ulaya na Asia ya Kati ambaye pia ni Mratibu Maalum wa Wakimbizi na Wahamiaji barani Ulaya Regina De Dominics amesema idadi hiyo ni ongezeko la asilimia 60 ikilinganishwa na kipindi kama hicho mwaka jana, ambapo karibu watoto 7,200 wasio na wazazi au waliotengwa walifanikiwa kuvuka katika safari hiyo inayoelezwa kuwa ni ya hatari.

“Bahari ya mediterania imekuwa makaburi kwa watoto na ndoto zao za baadaye” amesema Bi. Dominics na kuongeza kuwa ongezeko la watoto wanaotafuta hifadhi na usalama barani Ulaya ni matokeo ya sera zilizochaguliwa na mifumo iliyovunjika ya uhamiaji.

Kuna zaidi ya watoto 21,700 wasio na walezi nchini Italia kwa sasa, ikilinganishwa na idadi ya mwaka jana ya watoto 17,700.

Kwanini watoto wanasafiri wenyewe?

Vita, mizozo, ghasia na umaskini ni miongoni mwa vichochezi vikuu vya watoto kukimbia nchi zao bila ya wazazi au walezi.

Kwa mujibu wa UNICEF ushahidi unaonesha kuwa watoto wasio na walezi wako katika hatari ya unyonywaji na kunyanyaswa katika kila hatua ya safari zao, huku wasichana na watoto kutoka Afrika, Kusini mwa Jangwa la Sahara wakiwa kwenye uwezekano mkubwa wa kuteseka.

Wengine wengi hupoteza maisha

Kati ya mwezi Juni na Agosti mwaka huu, takriban watu 990 wakiwemo watoto walikufa maji au kutoweka walipokuwa wakijaribu kuvuka Bahari ya Kati ya Mediterania. 

Idadi hii ni mara tatu ya idadi ikilinganishwa na kipindi kama hicho majira ya joto mwaka jana 2022 ambapo watu wasiopungua 334 walipoteza maisha. 

Ajali nyingi za meli haziacha mtu yeyote aliyenusurika, na nyingi hazijarekodiwa, na kufanya idadi halisi ya waliojeruhiwa kuwa kubwa zaidi.

Katika matukio ya uokozi, watoto wanaookoka katika safari hizo za baharini hupatiwa hifadhi katika vituo vinavyojulikana kama maeneo yenye watu wengi zaidi kabla ya kuhamishiwa kwenye vituo vinavyopokea wakimbizi ambavyo mara nyingi hufungwa na kuna udhibiti wa watu kutembea.

Huko Lampedusa, UNICEF hutoa huduma muhimu za ulinzi ikijumuisha afya ya akili na usaidizi wa kisaikolojia na kuhakikisha wanapata taarifa na kupatiwa rufaa kwenda maeneo mengine kupata huduma maalum.