Hata kuwaeleza wazazi inakuwa ni mtihani : Mwanaharakati wa kupinga uonevu mtandaoni
Hata kuwaeleza wazazi inakuwa ni mtihani : Mwanaharakati wa kupinga uonevu mtandaoni
Wasiwasi, msongo wa mawazo na hata kujiua kwa watoto ni miongoni mwa matokeo mabaya ya uonevu mtandaoni, na mikakati bora ya kuzuia inayohusisha teknolojia kubwa lazima iandaliwe, limesema leo Baraza la Haki za Kibinadamu la Umoja wa Mataifa HRC mjini Geneva Uswisi.
Kulingana na matokeo ya utafiti wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF, wanafunzi milioni 130 duniani kote wanakabiliana na uonevu, ambao umechochewa na kuenea kwa teknolojia za kidijitali.
UNICEF inakadiria kuwa mwanafunzi mmoja kati ya watatu wa umri wa miaka 13 hadi 15 ni mwathirika.
Hatari ya kujiua
Baraza hilo limesikia ushuhuda kutoka kwa Santa Rose Mary mwenye umri wa miaka 15, mchechemzi wa masuala ya watoto kutoka nchini Uganda, ambaye amesema kwamba mara taarifa binafsi za mtu au picha zake nyeti zikishirikiwa mtandaoni, “huwezi hata kukabiliana na jamii unapoishi, huwezi hata kuwakabili wazazi wako mwenyewe”.
Ameonya kuwa hali kama hizo zinaweza kusababisha mtoto kujitoa uhai wakati "Anapopata hisia za kutohitajika katika jamii".
Naibu mkuu wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa Nada Al-Nashif amebainisha kuwa kulingana na kamati ya kutokomeza aina zote za ubaguzi dhidi ya wanawake (CEDAW), uonevu wa mtandaoni unaathiri wasichana karibu mara mbili zaidi ya wavulana.
Madhara makubwa
Bi. Al-Nashif amenukuu utafiti kutoka shirika la afya la Umoja wa Mataifa duniani (WHO), unaoonyesha kwamba watoto wanaodhulumiwa au kufanyiwa uonevu mtandaoni wana uwezekano mkubwa wa kutoroka shule, kutofanya vizuri kwenye mitihani na wanaweza kukosa usingizi na madhara ya kisaikolojia.
Baadhi ya tafiti pia zinaonyesha kuwa kuna uwezekano wa "athari kubwa zinazoendelea hadi utu uzima, kama vile kuenea kwa msongo wa mawazo na ukosefu wa ajira”, amesema.
Kupata haki
Bi. Al-Nashif ameliambia Baraza hilo kuwa mada tata ya uonevu mtandaoni iko kwenye kitovu cha masuala ya haki za binadamu, kidijitali na sera.
"Ili kupata haki hii, ni lazima tuchukue mtazamo kamili, na kushughulikia sababu za msingi wa suala hili", amesema, akisisitiza kwamba "kiini cha suala hili ni sauti ya watoto wenyewe".
Pia amesisitiza "uhalisia na uwezo wa makampuni katika fursa ya mtandaoni", akisisitiza juu ya wajibu wa makampuni ya teknolojia kutoa zana za faragha zilizobadilishwa na kufuata miongozo ya udhibiti wa maudhui kulingana na viwango vya kimataifa vya haki za binadamu".
Mashambulizi milioni 15: Facebook na Instagram
Mwakilishi wa Meta, mkurugenzi wa sera ya usalama Deepali Liberhan, ameshiriki katika majadiliano na kuzungumzia ukubwa wa tatizo.
Amesema katika robo ya tatu ya 2023 pekee, vipande milioni 15 vya maudhui viligunduliwa kwenye majukwaa ya Meta ya Facebook na Instagram ambayo yalijumuisha uonevu na unyanyasaji, vingi viliondolewa na Meta kabla hata ya kuripotiwa, au kuwekwa hewani amesema.
Bi. Liberhan ameangazia pia sera za udhibiti wa maudhui ya kampuni na njia ambazo Meta ilikuwa ikizitekeleza kwenye majukwaa yake, kwa kushirikiana na wataalamu kujulisha hatua inazochukua, na kujumuisha zana za kupinga unyanyasaji na uonevu katika uzoefu wa mtumiaji mtandaoni.
Wajibu wa pamoja
Mwishoni mwa kikao hicho, mwanajopo Philip Jaffé, mjumbe wa kamati ya Haki za mtoto, amesisitiza kuhusu wajibu wa pamoja kwa ajili ya usalama wa watoto wetu.
Amesisitiza kuwa "Tunahitaji kuwafanya watoto kufahamu zaidi haki zao na kufanya mataifa na sehemu nyingine za jamii kufahamu zaidi wajibu wao wa kuwalinda watoto ".