Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Misri yatoa kauli kuhusu mradi wa Bwawa Kuu la Renaissance Ethiopia

Waziri wa Mambo ya Nje wa Misri Sameh Hassan Shoukry Selim akihutubia mjadala mkuu wa mkutano wa 78 wa  Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, UNGA78 Septemba 23, 2023.
UN /Cia Pak
Waziri wa Mambo ya Nje wa Misri Sameh Hassan Shoukry Selim akihutubia mjadala mkuu wa mkutano wa 78 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, UNGA78 Septemba 23, 2023.

Misri yatoa kauli kuhusu mradi wa Bwawa Kuu la Renaissance Ethiopia

Amani na Usalama

Waziri wa Mambo ya Nje wa Misri, Sameh Shoukry amesema nchi yake inapinga mikakati ya taifa moja kusimamia rasilimali za maji zinazotumiwa na nchi zaidi ya moja akihusisha mradi wa Bwawa Kuu la Renaissance nchini Ethiopia unaotumia maji ya Mto Nile ambao unatumiwa na zaidi ya nchi moja.

Katika hotuba yake kwenye mjadala mkuu wa mkutano wa 78 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, UNGA78, Shoukry amesema “hakuna  fursa ya kupotosha kuwa uamuzi uliokwishafikiwa bila kuhusisha wengine, unaweza kupandikizwa pindi linapokuja suala la maisha ya wamisri zaidi ya milioni 100.”

Tuko makini kuendelea na mazungumzo ya dhati

Alikuwa anagusia kile alichoelezea kuwa kuendelea kwa Ethiopia kujaza maji kwenye bwawa hilo akisema ni ukiukwaji dhahiri wa kanuni za sheria ya kimataifa.

Amesema licha ya Ethiopia kuendelea yenyewe na mpango huo, Misri iko makini kuendelea kushiriki kwa kina kwenye michakato inayoendelea ya mazungumzo ili kufikia makubaliano ya kina yanayokidhi haki na maslahi ya wote.

"Bado tunasubiri washauri wetu wenye nia ya dhati wakutane na wale wa Ethiopia wenye azma ya dhati ili kufikia makubaliano yanayokidhi maslahi ya Misri, Sudan na Ethiopia,” amesema Bwana Shoukry.

Mapema leo, Ethiopia nayo ilisema kuwa iko tayari kwa mazungumzo ya pande tatu kuhusu mradi huo ambao ilianza kuutekeleza mwaka 2011.

Kuunga mkono harakati za amani

Waziri huyo wa Mambo ya Nje wa Misri amegusia pia changamoto zinazokumba Afrika akisema mfumo ulioanzishwa na nchi jirani na Sudan unaendelea kuangaza mwanga kwenye mzozo nchini humo na hivyo kuna nuru ya kupatikana kwa suluhu ya kudumua y kisiasa bila kuengua pande husika nchini Sudan.

Ameeleza utayari wa nchi yake kusaidia suluhu ya kisiasa nchini Libya, akisema kuwa Misri inasisitiza kuondoka haraka na bila masharti yoyote kwa vikosi vya kigeni Libya, sambamba na askari wa kukodiwa.

Nchi chache zinaamua bila kujali maslahi ya walio wengi

Amegusia pia kile alichosema ni mataifa machache kudhibiti mfumo wa ushirikiano wa kimataifa na upitishaji wa maamuzi ambao haujali kabisa maslahi ya watu na jamii zingine.

Ametaja Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa akitoa wito wa utekelezaji wa makubaliano ya Ezulwini na Azimio la Sirte viwe msingi wa kupanua uwakilishi wa  bara la Afrika kwenye Baraza hilo.