Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ethiopia: Tunakaribisha mazungumzo baina yetu na Sudan na Misri kuhusu Bwawa Kuu la Renaissance

Naibu Waziri Mkuu wa Ethiopia Demeke Mekonnen Hassen akihutubia mjadala mkuu wa mkutano wa 78 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa 23 Septemba 2023
UN /Cia Pak
Naibu Waziri Mkuu wa Ethiopia Demeke Mekonnen Hassen akihutubia mjadala mkuu wa mkutano wa 78 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa 23 Septemba 2023

Ethiopia: Tunakaribisha mazungumzo baina yetu na Sudan na Misri kuhusu Bwawa Kuu la Renaissance

Ukuaji wa Kiuchumi

Ethiopia imetumia hotuba yake kwenye Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kueleza kuwa iko tayari kwa na mazungumzo na Sudan na Misri kuhusu ujenzi unaoendelea nchini Ethiopia wa Bwana Kuu la Renaissance, GERD, ujenzi ambao umechochea mvutano baina ya taifa hili la Pembe ya Afrika na nchi mbili hizo kwa kutambua kuwa bwawa hilo linatumia maji ya mto Nile.

Naibu Waziri Mkuu wa Ethiopia, Demeke Mekonnen Hassen amesema hayo katika hotuba yake akihusisha mazungumzo hayo ya utatu na umuhimu wa ushirikiano wa kikanda katika kutatua mizozo.

Bwawa Kuu la Renaissance litaleta ustawi wa ukanda mzima

“Tuko tayari kushirikiana na majirani zetu kwenye maeneo ya biashara, muungano wa kikanda. Vikwazo vyovyote dhidi ya ustawi wa eneo letu lazima viondolewe kwa njia ya pamoja,” amesema  Naibu Waziri Mkuu Mekonnen ambaye pia ni Waziri wa Mambo ya Nje.

Amesema ushirikiano wa kikanda una athari chanya kwenye maisha ya watu, hasa ushirikiano huo unapoungwa mkono na miradi thabiti ya miundombinu na kwamba ,”mradi wa Bwawa Kuu la Renaissance ni moja ya miradi hiyo. Mradi unaokidhi maendeleo halali ya waethiopia na ukanda mzima.”

Kwa mantiki hiyo amesema anakaribisha kurejea kwa mazungmzo ya utatu baina ya Ethiopia, Misri na Sudan akisisitiza azma ya Ethiopia ya kufikia suluhu ya pamoja itakayokuwa na manufaa kwa pande zote chini ya uwezeshaji wa Muungano wa Afrika.

Bwawa hilo lijulikanalo pia kama Bwawa la Hidase limeanza kujengwa katika jimbo la Benishangul-Gumuz nchini Ethiopia, takribani kilometa 14 mashariki wa mpaka na Sudan na lengo kuu ni kuzalisha umeme.

Hata hivyo ujenzi huo umeibua mzozo kwa hofu kuwa litatumia kiwango kikubwa cha maji cha mto Nile, ambao ni tegemeo pia kwa Sudan na Misri.

Muundo wa Baraza la Usalama ufanyiwe marekebisho

Naibu Waziri Mkuu huyo wa Ethiopia ametumia hotuba yake pia kusisitiza umuhimu wa kuweko kwa mfumo mpya wa usalama amabo unaheshimu  uhuru wa kila nchi mwanachama wa Umoja wa Mataifa na ambao pia unazuia mizozo.

“Kama mmoja wa washiriki wa muda mrefu wa operesheni za ulinzi wa amani za Umoja wa Mataifa duniani kote, Ethiopia inasisitiza marekebisho ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na kwamba marekebisho hayo si jambo la kusema lifanyike au la, ni suala muhimu.”

Amesema hoja ya bara la Afrika kuwa na ujumbe wa kudumu kwenye Baraza hilo kwa mujibu wa dira yake ni halali kisiasa na kimaadili.