Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Samadi ya ng’ombe yachukua nafasi ya mkaa wa miti - Madina

Madina Jubilate Kimaro, Balozi wa Mazingira wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto duniani, UNICEF nchini Tanzania.
UN/Assumpta Massoi
Madina Jubilate Kimaro, Balozi wa Mazingira wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto duniani, UNICEF nchini Tanzania.

Samadi ya ng’ombe yachukua nafasi ya mkaa wa miti - Madina

Tabianchi na mazingira

Je umewahi kuona changamoto ukaigeuza fursa si kwako tu bali kwa wengine pia? Hiyo imemtokea Madina Jubilate Kimaro, msichana mwenye umri wa miaka 19 nchini Tanzania ambaye akiwa kwa bibi au nyanya yake jijini Dar es salaam nchini humo aliwaza na kuwazua kuona ni kwa vipi anaweza kutumia samadi ya ng’ombe kuwa bidhaa ya kusaidia kukabili mabadiliko ya tabianchi.

Tweet URL

Utajiuliza ni kwa vipi? Ni kwamba Madina aliwaza “je haiwezekani samadi hii ikawa ‘lulu’” hasa kugeuka kuwa nishati ya kupikia badala ya kutumia mkaa ambao sio tu una madhara ya afya kwa binadamu bali pia afya ya sayari dunia. 

Binti huyu ambaye ni Balozi wa Mazingira wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF nchini Tanzania alizungumza na Flora Nducha wa Idhaa ya Kiswahili ya Umoja wa Mataifa na kumweleza kuwa wazo lake hilo liligeuka kuwa vitendo na tayari wanatumia mkaa huo kupikia nyumbani kwao.

Tayari mkaa huu tunatumia nyumbani kwetu

“Huu mradi bado ni mdogo, unahitaji ushirikiano mkubwa. Mradi nimeanza kuufanyia nyumbani. Nyumbani kwetu tunatumia huu mkaa mbadala na unafanya kazi,” amesema Madina.

Zaidi ya yote awaeleze jinsi ya kuutumia na “tukatengeneza pamoja. Licha ya kuwa ni mradi wangu mimi, lakini watu wengine wanaweza kutengeneza na kupata fedha kutokana na mkaa huo mbadala kwani watauza, na watatumia na hivyo watakuwa wanahakikisha mazingira ni salama kwani wataacha kutumia mkaa wa miti.”

Nitachanganya samadi na maganda ya miwa

Madina Jubilate Kimaro, Balozi wa Mazingira wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto duniani, UNICEF nchini Tanzania.
UN/Assumpta Massoi
Madina Jubilate Kimaro, Balozi wa Mazingira wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto duniani, UNICEF nchini Tanzania.

Madina akifafanua kuwa ninatumia mikono kiviringa samadi kupata umbo la mduara, kisha vinakauka na vinakuwa mkaa. Lakini Madina anasema akirejea nyumbani ana mpango wa kuchanga samadi hiyo na maganda ya miwa, kwani yakikauka yanawaka vizuri.

Ndoto yake sasa ni kupata nafasi ya kuhakikisha anaweza kuuzalisha kwa wingi ili utumiwe na jamii.

Nahitaji vifaa ili kuongeza ubora

“Hapo ndio ninahitaji vifaa kwa sababu kutengeneza umbo la mkaa, na pia kuvikausha kwani wakati mwingine kuna mvua au jua au kuna wakati hufahamu iwapo umekauka vizuri, inabidi upasue uangalie ndani.”

Alipoulizwa kuhusu hewa ya Methane inayotoka kwenye samadi ya ng’ombe pengine inaweza kuwa na madhara kwa binadamu na mazingira, Balozi mwema huyo wa UNICEF amesema amefanya tafiti mitandaoni kuhusu hilo na ndio maana anasaka uwezeshaji ili apate vifaa vya kufanya mkaa huo wa samadi ya ng’ombe kuwa na ubora sio tu kwa afya ya binadamu bali pia sayari ya dunia.

Pamoja na kuhusika na mradi huu, Madina pia anapita shuleni na kuelimisha wanafunzi masuala ya mazingira kwa kupanda miti.