Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Leo ni siku ya kimataifa ya tabaka la Ozoni

Mtazamo kutoka juu wa safu nene ya mawingu ya cumulus, ukiangalia juu angani ya bluu huku miale ya jua ikipita kwenye mawingu upande wa kulia.
Unsplash/Gordon Lau Tabaka la ozoni linalopatikana juu katika anga, linaikinga dunia dhidi ya mionzi mikali yenye jua yenye madhara.

Leo ni siku ya kimataifa ya tabaka la Ozoni

Masuala ya UM

Mwaka1994, Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa lilitangaza Septemba 16 kama Siku ya kimataifa ya uhifadhi wa Tabaka la Ozoni, katika kuadhimisha kutiwa saini kwa Itifaki ya Montreal juu ya vitu Vinavyopunguza na kuathiri tabaka la Ozoni iliyopitishwa mwaka 1987.

Ozoni ni aina maalum ya oksijeni yenye fomula ya kemikali O3. Ozoni ni sehemu ndogo sana ya anga ya juu, lakini uwepo wake ni muhimu kwa afya na ustawi wa binadamu.

Tabaka la Ozoni hupatikana kati ya kilomita 10 na 40 juu ya uso wa Dunia. Eneo hili linaitwa stratosphere, na lina karibu asilimia 90 ya ozoni yote ya angani.

Umuhimu wa itifaki ya Montreal

Kaulimbiu ya siku ya kimataifa ya Ozoni mwaka huu inalenga kuangazia nafasi ya Itifaki ya Montreal katika kulinda tabaka la ozoni na kupambana na mabadiliko ya tabianchi.

Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa utafiti wa kisayansi umegundua kuwa kemikali kadhaa zinazotumiwa sana ni hatari sana kwa tabaka la ozoni. 

Uthibitisho wa kisayansi wa kuharibika kwa tabaka la ozoni umeifanya jumuiya ya kimataifa kuunda utaratibu wa ushirikiano wa kuchukua hatua za kulilinda tabaka hilo. 

Mwezi Machi tarehe 22, mwaka 1985, nchi 28 zilipitisha na kutia saini Mkataba wa Vienna wa Ulinzi wa Tabaka la Ozoni

Na mwezi Septemba 1987, rasimu ya itifaki ya Montreal kuhusu vitu vinavyopunguza Tabaka la Ozoni ilitengenezwa.

Umuhimu wa mikataba ya kulinda Ozoni

Mikataba ya kimataifa ya kulinda tabaka la ozoni imesaidia kuleta mabadiliko makubwa na yanayoonekana katika kulinda watu na sayari.

Lengo kuu la itifaki ya Montreal ni kulinda tabaka la ozoni kwa kuchukua hatua za kupunguza uzalishaji na matumizi ya kimataifa ya vitu vinavyoiharibu tabaka hilo. 

Itifaki inadhibiti karibu kemikali 100 katika makundi kadhaa. Kwa kila kundi, mkataba unaweka ratiba ya kukomesha uzalishaji na matumizi, kwa lengo la hatimaye kuviondoa kabisa vitu hivyo.

Kwa kuzingatia maendeleo thabiti yaliyopatikana chini ya Itifaki hiyo mapema tangu mwaka 2003, Katibu Mkuu wa sita wa Umoja wa Mataifa, Kofi Annan, aliita Itifaki ya Montreal kuwa pengine ni " makubaliano ya kimataifa yenye mafanikio makubwa zaidi katika historia ya binadamu." Maoni yake yanashirikiwa na wanasayansi na jumuiya pana ya kimataifa.

"Mikataba ya kimataifa ya kulinda tabaka la ozoni imesaidia kufikia mabadiliko makubwa na yanayoonekana katika kulinda watu na sayari," anasema Katibu Mkuu wa sasa wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres katika ujumbe wake kuadhimisha siku ya kimataifa ya Ozoni.

Ameongeza kuwa "Inathibitisha ufanisi wa mbinu ya kimataifa." Watu wote wanapaswa kuhamasisha matumaini kwamba kwa pamoja tunaweza kuepuka athari mbaya zaidi za mabadiliko ya tabianchi na kuhakikisha uendelevu wa mazingira na mnepo kwenye sayari.

Tarehe 16 Septemba 2009 mkataba wa Vienna na itifaki ya Montreal ilikuwa mikataba ya kwanza katika historia ya Umoja wa Mataifa kuidhinishwa duniani kote.