Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNESCO: Nchi zidhibiti matumizi ya AI mashuleni

Shule kote ulimwenguni zinahimizwa kubuni sera kuhusu matumizi ya programu za AI au akili bandia katika elimu.
© Unsplash/Hitesh Choudhary
Shule kote ulimwenguni zinahimizwa kubuni sera kuhusu matumizi ya programu za AI au akili bandia katika elimu.

UNESCO: Nchi zidhibiti matumizi ya AI mashuleni

Utamaduni na Elimu

Wakati muhula mpya wa masomo ukianza maeneo mengi duniani, Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu Sayansi na Utamaduni UNESCO limetoa muongozo wenye vipengele saba unaotaka nchi kudhibiti matumizi ya akili mnemba au -AI mashuleni.

Katika taarifa yake aliyoitoa hii leo mjini Paris Ufaransa Mkurugenzi Mkuu wa UNESCO Audrey Azoulay amesema matumizi ya AI yanaweza kuwa na fursa kubwa kwa maendeleo ya binadamu, lakini pia inaweza kusababisha madhara na chuki. 

“AI haiwezi kuunganishwa katika elimu bila ushirikiano wa umma, na ulinzi na kanuni muhimu kutoka kwa serikali.”

Mwongozo huo utazinduliwa rasmi Makao Makuu ya UNESCO wakati wa Wiki ya Mafunzo ya Dijitali ya UNESCO ambayo inakutanisha washiriki zaidi ya 1000 ili kujadili mada kuhusu majukwaa ya umma ya kujifunza kidijitali na matumizi yaAI katika elimu, pamoja na mada nyingine nyingi.

Yapi yaliyomo katika muongozo 

Miongoni mwa mambo yanayopaswa na kushughulikiwa haraka na nchi ni pamoja na kuwa na sera ya matumizi AI kimaadili katika elimu na utafiti, kuwe na faragha, umri uanzie miaka 13, pamoja na walimu wapatiwe mafunzo kuhusu AI.

Mwongozo huu pia unajibu hoja zilizoonyeshwa kwenye jedwali la kwanza la mawaziri la kimataifa kuhusu AI lililopitishwa na UNESCO mwezi Mei 2023.

Bi.Azoulay amesema mongozo huo wa UNESCO utasaidia watunga sera na walimu kutumia vyema uwezo wa AI kwa maslahi ya kimsingi ya wanafunzi. 

Kusoma muongozo wote wa UNESCO kuhusu elimu na utafiti bofya hapa.