Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

FAO Tanzania na wadau waja na mradi kuboresha zao la parachichi

Parachichi kadhaa za kijani za HASS huonyeshwa kwenye kitambaa chenye rangi ya miraba.
UN News FAO nchini Tanzania kwa ushirikiano na wadau wamekuja na mfumo wa kutumia vinasaba au DNA kusaidia kuhakikisha ubora wa miche na mbegu ya parachichi na hivyo wakulima kutambua kupitia alama ya utambulisho wa bidhaa au BARCODE.

FAO Tanzania na wadau waja na mradi kuboresha zao la parachichi

Ukuaji wa Kiuchumi

Nchini Tanzania, shirika la Umoja wa Mataifa la chakula na kilimo, FAO kwa kushirikiana na Taasisi ya udhibiti wa ubora wa mbegu TOSCI na Kamisheni ya Sayansi na Teknolojia Tanzania, COSTEC wameandaa mpango kabambe kupitia mfuko wa mradi wa ubunifu (Innovation Fund) kuhakikisha kuwa inaunda na kuanzisha maktaba yenye aina za parachichi kwa mfumo wa vinasaba yaani DNA ambazo mkulima anaweza kuziainisha katika kitalu kwa kupitia alama ya utambulisho wa bidhaa au BARCODE. 

 

Soundcloud

FAO inasema wameamua kuchukua hatua hii baada ya kubainika kuwa ongezeko la umaarufu wa kilimo cha parachichi umetumbukiza wakulima mikononi mwa wafanyabishara walaghai wa miche ya zao hilo.

Mathalani FAO inasema baada ya miaka minne ya kulea miche shambani, mkulima anavuna matunda ya parachichi na kugundua kuwa sio aina ile inayofaa kwa soko la nje ambayo ni HASS.

Parachichi limemsomesha mwanangu kilimo

Mradi huo utanufaisha wakulima kama vile Raphael Mnohno ambaye amekuwa akilima zao la parachichi kwa miaka 15 sasa ambapo katika ekari 30 za shamba la parachichi, zenye miti ya mavuno ni ekari 15 zikimpatia mifuko 500 ya matunda.

“Wanakijiji wenzangu hapa Ibuga wananufaika na uwepo wangu kwani nimewahamasisha wamenunua miche kutoka kwangu na sasa wanakijiji kama 200 wanalima parachichi,”  anasema Bwana Mnohno.

Manufaa pia ni kwa familia yake kwani kupitia kilimo hiki ameweza kumsomesha mtoto wake wa kiume aitwae James Raphael Diploma ya kilimo.

Baba kanisomesha sasa nasimamia kitalu cha miche ya parachichi

James anasema “nilipomaliza elimu ya sekondari, baba alinishauri nisomee kilimo, nimehitimu na sasa mimi ninasimamia kitalu cha miche ya parachichi. Nashauri vijana waingie kwenye kilimo hiki kwani kina faida. Kutoka kwenye kitalu tunauzia watu miche na tunapata fecha za kujikimu.”

Kwa mujibu wa mkulima Bwana Mnohno, mkewe anasimamia wafanyakazi wanaohusika na palizi kwenye shamba.

Vikonyo vya mti ulioboreshwa vyapandikizwa kwenye miti ya kienyeji

Remijius Kawishe, ni Afisa Kilimo, halmashauri ya wilaya ya Ngara ambapo amezungumzia ni kwa vipi wanahakikisha wakulima wanapata miche yenye ubora.

“Tunatumia vikonyo kutoka kwenye miti ya mikubwa ya parachichi inapandikizwa kwenye mche uliooteshwa wa kienyeji. Chini kuna mzizi wa mbegu ya kienyeji na hiki kikonyo ni cha mbegu iliyoboreshwa. Inafungwa kwa kamba maalum kwa mwezi mmoja kisha inafunuliwa tayari kupandwa,” amesema Bwana Kawishe.

Afisa huyu wa kilimo anasema faida ya mbinu hii inamaana inapunguza maambukizi ya magonjwa lakini zaidi inachukua miaka miwili kwa mkulima kuvuna kwa kuwa kikonyo kinakuwa kimetolewa kwenye mti mkubwa wa parachichi.

Wastaafu hiki ndio kilimo chetu- Mkulima Balyendeza

Andrea Balyendeza, mwalimu mstaafu wa lugha ya kifaransa, ni miongoni mwa walioingia katika kilimo cha parachichi mkoani Kagera.

“Hiki ni kilimo chenye faida sana, kwani hakichoshi mkulima kuanika na kuanua. Zao hili mnunuzi anakufuata na ndiye anahusika na kuchuma hayo matunda,” anasema Bwana Balyendeza akiwa ameshikilia parachichi alizovuna.