Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Madereva wa malori Malawi wajifunza kuhusu hatari za usafirishaji haramu wa binadamu

Maxwell Matewere (kushoto) mtaalamu wa kuzuia uhalifu UNODC Malawi, akiwa na maafisa wawili wakati wa uchunguzi wa usafirishaji haramu Malawi.
UNODC
Maxwell Matewere (kushoto) mtaalamu wa kuzuia uhalifu UNODC Malawi, akiwa na maafisa wawili wakati wa uchunguzi wa usafirishaji haramu Malawi.

Madereva wa malori Malawi wajifunza kuhusu hatari za usafirishaji haramu wa binadamu

Utamaduni na Elimu

Madereva wa malori kusini mwa Afrika ambao wamekuwa wakitumika kusafirisha kiharamu watu au kinyume cha sheria, sasa wanajifunza kuhusu hatari zinazohusiana na shughuli hiyo isiyo halali.  Shukrani kwa shirika la Umoja wa Mataifa la madawa ya kulevya na uhalifu, UNODC.

"Nilikuwa nikisafirisha sukari kutoka Malawi," aanasema dereva ambaye jina lake halikujulikana, ambaye alikamatwa kwa usafirishaji haramu wa wahamiaji. “Mwaka 2016, nililazimika kusubiri kwa siku kadhaa kwenye kivuko cha mpakani nchini Tanzania kwa ajili ya ukaguzi wa forodha. Nilifuatwa na mwanamume mmoja ambaye alinipa pesa nyingi za kusafirisha mbuzi.”

Simulizi yake sio ya kipekee

Malawi iko katika njiapanda ya misururu kadhaa ya watu wanaokimbia migogoro, ukosefu wa utulivu na umaskini katika Afrika ya Kati na Pembe ya Afrika.

Harakati kama hizo hutoa fursa nzuri kwa wasafirishaji haramu na kwa madereva 5,000 wa lori wa Malawi waliosajiliwa.

Dereva ambaye aliyesimulia hadithi yake alisema alilipwa mapema, na mtu aliyempa mpango huo alichukua picha zake na za lori lake. Dereva alianza kutumia baadhi ya pesa na kutuma zaidi kwa mkewe.

"Siku niliyotakiwa kuondoka, mtu huyo aliniambia 'mbuzi' hao walikuwa wahamiaji haramu 30 kutoka Ethiopia," alisema. “Walionekana wagonjwa sana, wamechoka, na wenye utapiamlo. Alisema ilinibidi kuwapeleka katika eneo nchini Malawi ambalo liko karibu na kambi kubwa ya wakimbizi.”

Vitisho vya wasafirishaji haramu

Lori linasafiri hadi Afrika Mashariki.
© ILO/Marcel Crozet

Dereva alipojaribu kupinga, msafirishaji huyo alidai kurejeshewa pesa zake na kutishia kuchukua lori hilo na kupeleka picha zake kwa mamlaka.

"Hivi ndivyo yote yalivyoanza, na ghafla ikawa biashara yangu kuu," alisema. "Mwanaume huyo alikuwa ananilipa pesa nyingi na kunisindikiza kwa gari dogo, ili aweze kuwahonga polisi wafisadi na maafisa wa uhamiaji njiani."

Kulingana na dereva huyo, mwanzoni hakujua kuwa alichokuwa akifanya ni kinyume cha sheria.

Kisha, mwaka wa 2019, alikamatwa nchini Msumbiji alipokuwa akisafirisha wahamiaji 72 kutoka Malawi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).

"Sasa mimi ni mgonjwa, sina kazi, na nimetalikiana," dereva huyo anasema.

Hatari za biashara haramu

Madereva wa malori wanaoishi Malawi sasa wanajifunza kuhusu hatari za kusafirisha wahamiaji na waathiriwa wa usafirishaji haramu wa binadamu, kutokana na mpango unaoungwa mkono na Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kukabiliana na Madawa na Uhalifu (UNODC). Kozi hizo zilizoanza Februari, tayari zinaonekana kuwa na mafanikio.

Feckson Chimodzi, dereva wa lori ambaye husafirisha mazao ya kilimo kutoka nchi za Kusini mwa Afrika hadi Malawi na pia ameshiriki katika mafunzo haya, anasema madereva wanaofanya kazi na maharamia na wasafirishaji haramu mara nyingi hufanya hivyo "kwa lazima" ili kuongeza mishahara yao midogo.

"Waajiri wetu wanahitaji kuboresha mazingira yetu ya kazi na kutupa mafunzo ya kina kuhusu hatari ya kujihusisha na uhalifu huu," Bwana. Chimodzi anasema.

Adhabu kali

Maxwell Matewere akizungumza na jamii nchini malawi kuhusu madhara ya usafirishaji haramu wa binadamu.
UNODC

Wahalifu wanaofanya magendo au kusafirisha binadamu kiharamu ndani ya nchi au kuvuka mipaka hutumia njia zote za usafiri kuwahamisha watu kwa faida na unyonyaji.

Iwapo watakamatwa na mamlaka, madereva wa lori kawaida hukamatwa na kufungwa, alielezea Maxwell Matewere, Afisa Mradi wa Kitaifa wa UNODC juu ya usafirishaji haramu wa watu.

"Kuna uelewa mdogo wa biashara haramu ya binadamu na ulanguzi wa wahamiaji katika kanda, na malipo ya kusafirisha watu kinyume cha sheria ni kubwa zaidi kuliko mshahara wa kawaida wa madereva wa lori," anasema Bwana Matewere, ambaye anaendesha mafunzo hayo.

"Madereva wengi wanajua wanachofanya ni kinyume cha sheria, lakini wanaambiwa kwamba wanapovuka mipaka, viongozi mafisadi watawaruhusu kupita, kwa hivyo, wanachukua pesa na hatari."

Kutaifishwa kwa gari na kukamatwa

Wahamiaji husafiri kwa miguu na kwa magari kote barani Afrika ili kufika Ulaya na maeneo mengine
IOM/Alexander Bee

Kufuatia mfululizo wa kutaifishwa na kukamatwa kwa magari katika nchi jirani, Chama cha Madereva Wataalamu cha Malawi kiliomba UNODC kutoa mafunzo kwa wanachama wake kuhusu hatari za kusafirisha wahamiaji na wahanga wa biashara haramu.

Jumla ya kozi nne kwa karibu madereva 400 zimefanyika, na vipindi vingine vimepangwa mnamo Oktoba. Washiriki wanafahamishwa kuhusu adhabu wanazokabiliana nazo iwapo watakamatwa, ikiwa ni pamoja na kupoteza lori na ajira zao, rekodi ya uhalifu, na kufungwa jela kwa hadi miaka 14 katika nchi ya kigeni.

Matokeo chanya, washirika wapya

Tangu kuanza kwa kozi za UNODC, Chama cha Madereva Wataalamu kimeripoti kupungua kwa idadi ya kukamatwa kwa madereva wa Malawi kwa tuhuma za ulanguzi wa wahamiaji na usafirishaji haramu wa binadamu.

Madereva wengi waliohudhuria mafunzo wanathibitisha kuwa "washirika muhimu sana" katika kuzuia na kugundua visa vya magendo ya wahamiaji na usafirishaji haramu wa binadamu, anasema Bwana Matewere.

"Tunaeleza kuwa magendo ya wahamiaji na usafirishaji haramu wa binadamu ni vitendo vya uhalifu vilivyopangwa ambavyo vinaadhibiwa na sheria nchini Malawi na nchi ambazo madereva wanapitia, kama vile Zimbabwe, Zambia, Tanzania na Msumbiji," anasema.

SDG 16: Amani, Haki na Taasisi Imara.
Umoja wa Mataifa

"Zaidi ya hayo, madereva wanaambiwa kwamba uhalifu huu unahusishwa na unyonyaji, unyanyasaji, na unyanyasaji na unaweza hata kusababisha kifo, na tunawaambia kuhusu uhusiano na shughuli nyingine haramu kama vile madawa ya kulevya na magendo ya silaha," Anaongeza Bwana Matewere.

Mwaka jana, Wizara ya Usalama wa Ndani ya Malawi iliteua kundi jipya la maafisa wa kutekeleza sheria kukabiliana na ongezeko la visa vya ulanguzi wa wahamiaji na biashara haramu ya binadamu.

Aidha Matewere anaeleza kwa matumaini akisema, "Tumeanzisha mawasiliano kati ya madereva wa lori tuliowafunza na kitengo hiki maalum, kwa hivyo sasa wanajua ni nani wa kumjulisha wanapofikiwa na wahalifu kubeba watu kwenye magari yao." 

Tangu Mei, majaribio saba ya biashara haramu ya binadamu na magendo ya wahamiaji yamesimamishwa na mamlaka katika vivuko vya mpaka kutokana na taarifa kutoka kwa madereva wa lori. Kesi ya hivi karibuni ilihusisha Wamalawi 40, wakiwemo watoto, waliokuwa wakichukuliwa kwa malori matatu kuelekea Afrika Kusini na kuzuiwa kwenye mpaka na Zambia.

Kozi hizo za kuongeza ufahamu zimeandaliwa kupitia kitengo cha UNODC cha biashara haramu ya binadamu na magendo ya wahamiaji, kwa ushirikiano wa Wizara ya Usalama wa Ndani ya Malawi na usaidizi wa kifedha kutoka kwa Serikali ya Sweden.

Fahamu zaidi kuhusu jinsi UNODC inavyokabiliana na biashara haramu ya binadamu na ulanguzi wa wahamiaji kwa kubofya hapa.