Haki Center, mdau wa UNHCR moja ya mashirika yaliyosaidia Wapemba kutambulika rasmi Kenya
Haki Center, mdau wa UNHCR moja ya mashirika yaliyosaidia Wapemba kutambulika rasmi Kenya
Mwishoni mwa mwezi uliopita Rais wa Kenya William Ruto akiwa Kilifi mashariki mwa Kenya alitangaza kutambulika rasmi kwa jamii ya Wapemba ambao kwa miaka mingi waliishi nchini humo wakikosa hadhi ya utaifa kwa kuwa vizazi vyao vya nyuma vilitoka nje ya Kenya. Nyuma ya mafanikio haya zimekuwepo harakati za muda mrefu za kuitafuta haki hiyo zikifanywa na wananchi na mashirika yasiyo ya kiserikali. Moja ya mashirika hayo ni Haki Center ambalo ni mdau wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi (UNHCR) katika eneo la pwani na kaskazinimashariki mwa Kenya.
Barke Hamisi kutoka jamii ya wapemba anatambua mchango wa shirika hili na anakumbuka hali ilivyokuwa kabla ya hatua ya juzi ya kutambulika,
“Mimi nimezaliwa hapa watamu na nikalelewa hapa watamu na pia nilisoma shule ya msingi watamu. Nilikuwa najumuika vizuri na jamii zingine lakini shida ilikuwa ni mtu anakwambia wewe ni mpemba. Sasa mtu akikuambia wewe ni mpemba, hiyo ni kama mtu amekudunga mkuki. Unakosa morali (ari).”
Na ni kwa vipi basi shirika la Haki Center lilichangia harakati hizi? Barke anaeleza, “Haki Center ilikuwa na mchango mkubwa katika utetezi wetu kwa sababu walituwezesha sana kutojificha tena kupigania haki yetu kupitia msaada wao, ndipo tuliposhirikiana na wabunge na kutoka kwenye mazungumzo na majadiliano tuliyokuwa nayo pamoja nao tuliandika ombi.”