Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Jawabu la changamoto za dunia hivi sasa ni mshikamano - Guterres

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres (kushoto) akizungumza kwenye mkutano wa 15 wa wakuu wa nchi za BRICS mjini Johannesburg, Afrika Kusini. Open in Google Translate •
© DIRCO
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres (kushoto) akizungumza kwenye mkutano wa 15 wa wakuu wa nchi za BRICS mjini Johannesburg, Afrika Kusini. Open in Google Translate •

Jawabu la changamoto za dunia hivi sasa ni mshikamano - Guterres

Tabianchi na mazingira

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres siku ya Alhamisi amehutubia mkutano wa viongozi wa kundi la BRICS na kusisitiza umuhimu wa Umoja na Haki katika kutatua changamoto kubwa zinazokumba binadamu hivi sasa kuanzia janga la tabianchi na ukosefu wa usawa kiuchumi hadi mizozo inayotikisa dunia. 

Tweet URL

Katika hotuba yake hiyo kwenye mji mkuu Johannesburg, Afrika Kusini, Katibu Mkuu ametumia fursa hiyo kupongeza taifa hilo linalotambulika kama taifa la upinde wa mvua kutokana na utofauti wa makabila na watu rangi mbalimbali lakini limeweza kusonga kwenye njia ya umoja kupitia hatua mbalimbali na haki. 

“Hicho ndio dunia inahitaji: Umoja kwa hatua na haki; tunakabiliwa na changamoto zinazotishia uwepo wetu,” amesema Katibu Mkuu, akimulika madhara ya kila uchao yatokanayo na mabadiliko ya tabianchi, ongezeko la umaskini,  njaa na ukosefu usawa. 

Kundi la kiuchumi la BRICS linaundwa na Brazil, Urusi, India, China na Afrika Kusini  iliyojiunga mwaka 2010, na linawasilisha asilimia 40 ya idadi ya watu wote duniani, na nchi hizo tano zote ni wanachama wa kundi pana la mataifa 20, au G20. 

Bwana Guterres ameangazia madhara yatokanayo na teknolojia zinazoibuka bila uwepo wa  mfumo wa kimataifa wa usimamizi, huku akitaja pia migawanyiko ya kijiografia na kisiasa hasa athari zitokanazo na uvamizi wa Urusi nchini Ukraine. 

‘Dunia yenye makundi mgawanyiko’ 

Katika hotuba yake, Bwana Guterres ametaja mwenendo wa sasa wa kuibuka kwa makundi yanayojigawa, akisema dunia yenye makundi kama hayo haitakuwa  hakikisho la amani na hali yenye haki. Ametoa wito wa kuweko kwa taasisi za kimataifa zenye haki na zinazoweza kuunga mkono mwenendo huo wa makundi. 

Akilinganisha na karne ya 20, Katibu Mkuu amesema somo wakati ambapo Ulaya iliyokuwa na makundi tofauti bila mfumo thabiti wa kusaidia makundi hayo ndio ulichochea kuanza kwa Vita ya Kuu ya Kwanza ya dunia. 

“Kadri jamii ya kimataifa inapoelekea kwenye mgawanyiko wa kimakundi, tunahitaji zaidi uchechemuzi wa muundo wa kimataifa ulioimarishwa kwa misingi ya Chata ya UN na Sherika za kimataifa,” amesema Katibu Mkuu. 

Akitaja miundo ya sasa ya usimamizi duniani iliyoanzishwa baada ya Vita Kuu ya Pili ya dunia, ikiengua nchi za Afrika ambazo bado zilikuwa zinatawaliwa, amesisitiza umuhimu wa taasisi hizo kuakisi mienendo ya sasa ya utawala na kiuchumi. 

Bila marekebisho, kusambaratika hakuepukiki 

Katibu Mkuu ameonya kuwa bila marekebisho ya aina hiyo, pasi shaka kusambaratika hakuepukiki. 

“Hatuwezi kuwa na dunia yenye iliyogawanyika kiuchumi na kifedha; dunia yenye mikakati tofauti dhidi ya teknolojia na akili mnemba; dunia yenye mifumo kinzani ya usalama,” amesema Bwana Guterres. 

Katibu Mkuu amesema nchi za kipato cha chini, hasa za bara la Afrika zitabeba mzizgo wa athari za mgawanyiko huo. 

“Nimekuja Johannesburg na ujumbe mwepesi: katika dunia iliyogubikwa na majanga, hakuna jawabu mbadala zaidi ya ushirikiano,” amesema Katibu Mkuu. 

Marekebisho ya mfumo wa fedha duniani

Akizungumzia changamoto za kipekee za bara la Afrika, Katibu Mkuu ameesma bara hilo ni manusura wa kihistoria wa utumwa na ukoloni, na linaendelea kukabiliwa na ukosefu mkubwa wa haki, ikiwemo tofauti za kiuchumi na mabadiliko ya tabianchi.

Ametoa wito kwa marekebisho ya muudno wa ushirikiano wa kifedha duniani na kuimarisha hatua kwa tabianchi, akitaja Makubaliano ya Mshikamano kwa Tabianchi na Ajenda ya kuongeza kasi.

“Nchi zilizoendelea lazima hatimaye zitekeleze ahadi zao kwa nchi zinazoendelea; kwa kutimiza lengo la dola bilioni 100, kuongeza maradufu ufadhili kwa miradi ya kuhimili mabadiliko ya tabianchi, kujazia Fuko la Tabianchi, na kuanza kutekeleza mwaka huu fedha za fidia kutokana na uharibifu uletwa na mabadiliko ya tabianchi.

Wito wa hatua za pamoja

Bwana Guterres ametamatisha hotuba yake kwa kutoa wito wa hatua za pamoja akisisitiza kuwa binadamu hatoweza kutatua changamoto za sasa katika mazingira ya mgawanyiko.

“Kwa pamoja, hebu na tufanye kazi kusongesha uthabiti wa hatua za pamoja, haki na ahadi ya mustakabali bora.”