Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

HABARI KWA UFUPI: Katibu Mkuu UN ahutubia BRICS. Pia kuna Myanmar vilevile UNICEF na hatima ya watoto Sudan

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres (Picha ya maktaba)
United Nations/Cyril Bailleul
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres (Picha ya maktaba)

HABARI KWA UFUPI: Katibu Mkuu UN ahutubia BRICS. Pia kuna Myanmar vilevile UNICEF na hatima ya watoto Sudan

Masuala ya UM

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres amehutubia mkutano wa viongozi kundi la Brazil, Urusi, India, China na Afrika Kusini au BRICS huko Johannesburg Afrika Kusini na kusema katika dunia ya sasa iliyogawanyika na kugubikwa na majanga hakuna mbadala mwingine wa kuwezesha kusonga mbele zaidi ya mshikamano hasa kwenye masuala lukuki ikiwemo marekebisho ya mfumo wa kimataifa wa fedha duniani.  

 

MYANMAR

Ikiwa kesho ni miaka 6 tangu serikali ya kijeshi nchini Myanmar ianze msako wa kufurusha waislamu wa kabila la Rohingya kutoka jimbo la Rakhine nchini humo, Kamishna Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusu Haki za Binadamu Volker Türk amesema jamii ya kimataifa isisahau warohingya na wale wanaowahifadhi, na zaidi ya yote juhudi za kimataifa ziongezwe maradufu ili wahusika wawajibishwe. 

UNICEF SUDAN

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF linaonya kuwa bila amani nchini Sudan, hatma ya watoto iko mashakani wakati huu ambapo zaidi ya watoto milioni 2 wamefurushwa makwao tangu mapigano yaanze kwenye mji mkuu Khartoum mwezi Aprili mwaka huu na sasa mapigano hayo yanaenea kwenye maeneo mapya.