Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

HABARI KWA UFUPI: Sudan na Mediteranea

Mhamiaji mvulana akitazama rasi upande wa Italia
© UNICEF/Ashley Gilbertson VII
Mhamiaji mvulana akitazama rasi upande wa Italia

HABARI KWA UFUPI: Sudan na Mediteranea

Afya

Hii leo katika Habari Kwa Ufupi tunamulika athari za vita nchini Sudan kwa wakimbizi, halikadhalika kwenye utoaji huduma za afya na kisha tunakwenda bahari  ya Mediteranea ambako huko kuna ajali nyingine ya meli.

 

SUDAN - UNHCR

Wakati idadi ya watu wanaokimbia machafuko nchini Sudan ikifikia milioni 4, Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR limesema lina wasiwasi mkubwa kuhusu kuzorota kwa afya za wakimbizi hao ikiwa ni pamoja na wale wanaoishi katika kambi za wakimbizi.

UNHCR inatolea mfano jimbo la White Nile, ambako ukosefu wa dawa muhimu, watumishi na vifaa vya matibabu unakwamisha kwa kiasi kikubwa huduma za afya na lishe katika kambi zote 10 za wakimbizi, ambako wakimbizi wapya 144,000 kutoka mji mkuu wa Sudan, Khartoum wamewasili tangu kuanza kwa vita.

SUDAN - WHO

Tukisalia na vita nchini Sudan, nalo shirika la Afya la Umoja wa Mataifa WHO limeeleza kukabiliwa na uhaba wa vifaa vya matibabu pamoja na huduma za maji na umeme katika maeneo yaliyoathirika na vita.

WHO pia imelaani vikali mashambulizi yanayolenga watoa huduma za afya na vituo vya afya ambapo hadi  mwishoni mwa mwezi Julai mwaka huu,  jumla ya vituo 53 vilikuwa vimeshambuliwa na kusababisha vifo vya watu 11 na majeruhi 38.

MEDITERANEA - UNICEF

Na tuhitimishie pwani ya Lampedusa, nchini Italia ambapo Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF limesikitishwa na ajali nyingine ya meli katika bahari hiyo ya Mediterania.

Miongoni mwa waliopoteza maisha ni pamoja na mjamzito pamoja na mtoto mwenye umri wa miezi 18. 

Unicef inasema hadi sasa watu wengine 30 hawajulikani waliko.

Katika nusu ya kwanza ya mwaka huu takribani watoto 289 wamekufa au hawajulikani waliko wakijaribu kuvuka mediteranea ya kati kuelekea Ulaya.

MWISHO WA HABARI KWA UFUPI