Maisha ya kila siku nchini Sudan ni jinamizi - OCHA
Maisha ya kila siku nchini Sudan ni jinamizi - OCHA
Mkuu wa kitengo cha Operesheni na Uchechemuzi kwenye Ofisi ya Umoja wa Mataifa inayohusika na masuala ya kibinadamu na kuratibu masuala ya dharura OCHA Edem Wosornu amesema maisha ya kila siku ya wananchi nchini Sudan yamegubikwa na sintofahamu kutokana na vita inayoendelea hivyo amesihi pande husika kukomesha mapigano na wakati huo huo wahisani waongeze ufadhili wa kibinadamu.
Akihojiwa na Idhaa ya kiarabu ya Umoja wa Mataifa Bi. Wosornu ambaye alikuwa ziarani nchini humo hivi karibuni, amesema hali ya sintofahamu imekumba wananchi akitolea mfano Hawaa, mama, bibi na mfanyabiashara ambaye alikuwa mchuuzi nje kidogo ya mji mkuu wa Sudan Khartoum ambaye sasa tangu vita ianze hawezi kujikimu bali anategemea malipo kidogo ya fedha kila mwezi ili anunue dawa za kujitibu kisukari.
Na kwa watoa misaada ya dharura nao hali ni mbayá,
“Na niliwauliza maisha yako vipi kwa mtu wa kawaida mjini Khartoum? Na wakasema ni kama jinamizi kwa sababu hufahamu kama upande wowote ule utakukamata na kukuweka ndani. Hufahamu iwapo utatoweshwa. Lakini wanaendelea na maisha kwa sababu wameazimia kuliko wakati wowote ule kusambaza misaada ya kiutu.”
Afisa huyo wa OCHA ametoa wito kwa wahisani wengine zaidi wajitokeza kuchangia ili kufanikisha mahitaji ya wananchi wa Sudan huku akipeleka ujumbe kwa pande kinzani ambazo ni jeshi la serikali, (SAF) na wanamgambo waasi wa kikundi cha Rapid Support Forces (RSF),
“Ujumbe wangu kwa pande kinzani ni ujumbe ambao wasudan wamenieleza nilipotembelea Sudan. Acheni vita. Acheni mapigano ma tuacheni turejee majumbani mwetu na tuishi maisha yetu.”