Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UN yalaani mashambulizi dhidi ya maeneo ya kihistoria Odesa, Ukraine

Mitaa ya mji wa Odesa wakati huu wa uvamizi wa Urusi
Ofisi ya Meya wa Odesa
Mitaa ya mji wa Odesa wakati huu wa uvamizi wa Urusi

UN yalaani mashambulizi dhidi ya maeneo ya kihistoria Odesa, Ukraine

Utamaduni na Elimu

Maafisa waandamizi wa Umoja wa Mataifa wamelaani vkali mashambulio makubwa yaliyofanywa na makombora ya Urusi dhidi ya mji wa Odesa nchini Ukraine, mashambulio ambayo yameharibu majengo kadhaa ya kihistoria.

Kwa wiki nzima iliyopita, Urusi tangu ijitoe kwenye makubaliano ya kihistoria ya kusafirisha mbolea na nafaka kupitia Bahari Nyeusi, imekuwa ikifanya mashambulio ya kutoka angani dhidi ya mji wa Odesa na miji mingine miwili ya bandari nchini Ukraine ambayo ni Chornomorsk na Mykolaiv.

Vyombo vya habari vya kimataifa vimeripoti kwamba mtu mmoja  ameuawa na watu wengine zaidi ya 20 wamejeruhiwa katika shambulio la Jumapili ambalo limeharibu majengo ya kihistoria mjini Odesa likiwemo kanisa kuu katika ene eneo ambako Yesu alibadilika sura mbele ya mitume wake, (Transfiguration Church).

Kanisa hilo kuu liliasisiwa mwaka 1794 na liko kwenye kituo cha historia cha Odesa, na ni kanisa ambalo mwei Januari mwaka huu wa 2023 liliingizwa kwene orodha ya Maeneo ya urithi wa dunia na hivyo linatunzwa na shirika la Umoja wa MAtaifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni, UNESCO.

Utamaduni sasa umelengwa

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa  António Guterres amelaani vikali shambulio hilo ambapo pamoja na kuchukizwa na kitendo cha vita kusababisha vifo, amesema “hili ni shambulio linguine kwenye eneo ambalo liko chini ya Mkataba wa Kimataifa wa urithi wa dunia na linakiuka mkataba wa kimataifa wa The Hague wa ulinzi wa mali za kitamaduni kwenye maeneo ya kivita, mkataba wa mwaka 1954.”

Halikadhalika, Bwana Guterres alielezea wasiwasi wake kuhusu vita hivyo vinavyoendelea kutishia utamaduni na urithi nchini Ukraine.

UNESCO imethibitisha uharibifu wa maeneo 270 ya kitamaduni, yakiwemo maeneo 116 ya kidini tangu kuanza kwa uvamizi wa Urusi nchini Ukraine tarehe 24 mwezi Februari mwaka 2022.

“Katibu Mkuu amesihi Urusi kusitisha mara moja mashabulizi dhidi ya mali za kitamaduni zinazolindwa na mikataba ya kimataifa. Katibu Mkuu pia ameendelea kusihi sitisho la mapigano dhidi ya miundombinu yoyote ya kiraia,” imesema taarifa iliyotolewa na msemaji wa UN jijini New York, Marekani.

'Uharibifu mkubwa'

UNESCO imesikitishwa sana na shambulio hilo huku ikisema ujumbe maalum utapelekwa siku chache zijazo kutathmini uharibifu.

Shirika hilo limesema kitendo hicho cha chuki, kinafuatia shambulio linguine kwenye maeneo ya urithi yaliyook Lviv na Odesa, maeneo ambayo nayo yako chini ya mkataba wa kimataifa wa urithi wa dunia.

Mkurugenzi Mkuu wa UNESCO, Audrey Azoulay amesema uharibifu huo mkubwa unaonesha tena ghasia dhidi ya urithi wa kitamaduni nchini Ukraine.

Amesihi Urusi ichukue hatua bora kuzingatia wajibu wake chini ya sheria ya kimataifa ikiwemo zile za ulinzi wa mali za kitamaduni kwenye mazingira ya vita.

UNESCO inasema itahitajika dola bilioni 7 katika muongo ujao ili kujenga upya sekta ya utamaduni Ukraine.