Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNHCR imeonya dhidi ya kuongezeka kwa ukatili dhidi ya wanawake na wasicha Mashariki mwa DRC

Mtoto akibeba maji kupitia eneo la kambi ya wakimbizi wa ndani ya Kanyaruchinya mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
© UNICEF/Arlette Bashizi
Mtoto akibeba maji kupitia eneo la kambi ya wakimbizi wa ndani ya Kanyaruchinya mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

UNHCR imeonya dhidi ya kuongezeka kwa ukatili dhidi ya wanawake na wasicha Mashariki mwa DRC

Haki za binadamu

Hali ya kusikitisha inajitokeza Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC, ambapo ghasia zilizozuka upya kati ya makundi yasiyo ya kiserikali yenye silaha na vikosi vya serikali zimerejea katika majimbo ya Kivu Kaskazini, Kivu Kusini na Ituri zikiambatana na ukatili mkubwa dhidi ya wanawake na wasichana na kutawanya maelfu ya watu, limeonya leo shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR.

Katika taarifa yalke iliyotolewa leo mjini Geneva Uswis kamishina msaidizi wa masuala ya ulinzi wa UNHCR Gillian Triggs amesema kutokana na hali hiyo, watu milioni 2.8 wamekimbia makazi yao katika majimbo hayo tangu mwezi Machi 2022. 

Miongoni mwa orodha ya sheria za kibinadamu na ukiukaji wa haki za binadamu, unaoendelea ni raia kuuawa na kuteswa, huku kukamatwa kiholela, uporaji wa vituo vya afya, nyumba za raia, na uharibifu za shule pia vimeripotiwa.

Triggd ameongeza kuwa “Pia tunasikitishwa sana na kuongezeka kwa ripoti za ukatili wa kijinsia dhidi ya wanawake na wasichana waliolazimika kukimbia makwao, ikiwa ni pamoja na vitendo vya ubakaji na unyanyasaji wa kijinsia.

Cha kusikitisha, zaidi takwimu za hivi karibuni zinaonyesha kwamba kati ya zaidi ya watu 10,000 waliopata huduma za unyanyasaji wa kijinsia (GBV) huko Kivu Kaskazini katika robo ya kwanza ya mwaka, asilimia 66 ya kesi hizi zilikuwa za ubakaji.”

Ameendelea kusema kwamba visa vingi vya ukiukaji huu mbaya wa GBV vimeripotiwa kufanywa na watu wenye silaha. 

Hata hiuvyo amesema anaamini takwimu hizo ni sehemu ndogo tu ya kile kinachoendelea kwani nmanusura wengi wa GBV hawaripoti ukatili huo au kufuata msaada wa huduma kutokana na hofu ya unyanyapaa kwenye jamii lakini pia fursa ya kuwafikia waathirika bado ni finyu kutokana nna hali ya usalama na masuala ya kiufundi.

Kwa mujibu wa afisa huyo wa UNHCR hali ngumu ya maisha imewasukuma wanawake na wasichana wengi kugeukia mbinu za hatari kama biashara ya ngono hasa Goma Kivu Kaskazini ili kujikimu kimaisha na familia zao hasa wakati huu ambapo changamoto ya kutokuwa na uhakika wa chakula inaongezeka.

Lakini pia amesema wanawake na wasichana wengi wanabakwa wakati wakienda kusenya kuni na kuteka maji.

Amehitimisha taarifa yake kwa kusema “Tunatoa wito kwa serikali na mamlaka za mitaa kuchukua hatua za haraka kukabiliana na janga hili la kutisha la GBV. Wale waliohusika na ukiukaji huu mbaya wa haki za binadamu na sheria za kibinadamu lazima wawajibishwe.”