Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Jiandaeni na athari za kiafya ziletwazo na El Niño:WHO

Ukame unaosababishwa na El Niño huko Ziway Dugda, eneo la Oromia nchini Ethiopia, unaathiri kila familia na hawana chakula cha kutosha nyumbani cha kujilisha.
OCHA/Charlotte Cans
Ukame unaosababishwa na El Niño huko Ziway Dugda, eneo la Oromia nchini Ethiopia, unaathiri kila familia na hawana chakula cha kutosha nyumbani cha kujilisha.

Jiandaeni na athari za kiafya ziletwazo na El Niño:WHO

Tabianchi na mazingira

Shirika la Umoja wa Mataifa la afya ulimwenguni WHO limesema linajiandaa na uwezekano mkubwa mwaka huu 2023 na 2024 itaathiriwa na El Niño. 

Akizungungumza kupitia mtandao akiwa jijini Geneva Uswisi Dkt. Maria Neira ambaye ni Mkurugenzi wa Mazingira,mabadiliko ya tabianci na afya wa WHO amesema utabiri wa hivi karibuni unaonesha kuwa hali ya El Niño sasa iko na inatarajiwa kufikia kilele chake kati ya mwezi Septemba 2023 na Februari 2024.

“El Niño inaweza kusababisha matukio mbalimbali ya  hali mbaya ya hewa, ikiwa ni pamoja na ukame, mafuriko, vimbunga, na mawimbi ya joto, ambayo yote ni hatari kwa afya ya binadamu.” Amesema Dkt Neira.

El Niño inatarajiwa kuathiri maeneo mengi ulimwenguni lakini athari kubwa zaidi zitaonekana kwenye maeneo yenye hali ya ya joto, ikiwa ni pamoja na nchi na maeneo ya Afrika, Amerika ya Kusin, pamoja na Kusini na Kusini-Mashariki mwa Asia ambako huathirika zaidi na majanga ya asili.

Athari za kiafya ziletwazo na El Niño

Kwa kubadilisha hali ya hewa, El Niño inaweza kuwa na madhara makubwa kwa viashirio muhimu vya afya kupitia, mambo mbalimbali kama vile; athari kwa usalama wa chakula, ubora wa hewa na maji, mifumo ikolojia na usalama wa miundombinu ya afya. Matukio ya magonjwa yanayoenezwa na wadudu na magonjwa yanayoenezwa na maji, kukabiliwa na moshi na moto wa nyikani, na mafuriko na athari za kiafya na lishe zinazohusiana na ukame.

Miradi ya mashirika ya Umoja wa Mataifa yakwamua jamii nchini Ethiopia.
Picha: FAO/Tamiru Legesse
Miradi ya mashirika ya Umoja wa Mataifa yakwamua jamii nchini Ethiopia.

Nchi zijiandae na athari zifuatazo za kiafya:

  1. Uhaba wa chakula na kuongezeka kwa utapiamlo wa wastani na wa hali ya juu hasa miongoni mwa walio hatarini zaidi.
  2. Kuongezeka kwa magonjwa yatokanayo na maji kama vile kipindupindu kutokana na uhaba wa maji au mafuriko na miundombinu ya vyoo.
  3. Ongezeko la milipuko ya magonjwa yanayoenezwa na mbu kama vile malaria katika maeneo ya nyanda za juu ambayo kwa kawaida ni baridi san, na ongezeko la hatari ya Homa ya Bonde la Ufa.
  4. Kuongezeka kwa idadi ya watu walioathiriwa na magonjwa ya kuambukiza kama vile surua na uti wa mgongo.
  5. Kukatizwa kwa huduma za afya kutokana na ukosefu wa maji katika hali ya ukame au uharibifu wa miundombinu ya afya kutokana na mafuriko na vimbunga.
  6. Joto kali na ongezeko la hatari ya moto wa mwituni
Familia ikipata mlo wao wa kila siku nyumbani kwao wilaya ya Balaka nchini Malawi (Juni 2016)
UNICEF/Sebastian Rich
Familia ikipata mlo wao wa kila siku nyumbani kwao wilaya ya Balaka nchini Malawi (Juni 2016)

WHO inafanya nini?

Ingawa athari halisi za matukio ya El Nino haziwezi kutabiriwa kwa usahihi, lakini WHO inatoa msaada kwa nchi ambazo athari ya El Niño zinatarajiwa kutokea. 

Wanafanya hivyo kupitia ufuatiliaji endelevu wa utabiri, tathmini za hatari, uimarishaji wa juhudi zinazowezekana za kukabiliana na kujiandaa pamoja na mipango ya dharura na uimarishaji wa magonjwa yaletwayo na El Niño

WHO ni sehemu ya mifumo ya Umoja wa Mataifa ya uratibu na ufuatiliaji wa El Niño na inafanya kazi kwa karibu na mashirika kama vile WMO linalohusika na utabiri wa hali ya hewa duniani. 

WHO inaratibu katika ngazi za kimataifa, kikanda na nchi ili kutoa taarifa na usaidizi wa kiufundi kwa Nchi Wanachama na washirika wa afya na kuimarisha utayari wa matukio ya afya yanayohusiana na El Niño.