Viwavi jeshi vimerejea Afrika Mashariki, FAO kusaidia kuvikabili
Viwavi jeshi vimerejea Afrika Mashariki, FAO kusaidia kuvikabili
Shirika la Umoja wa Mataifa la Chakula na Kilimo FAO,limetahadharisha kuwa viwavijeshi ambavyo vimeripotiwa kuonekana kwenye mbuga na hifadhi za wanyama nchini Kenya vimerejea. Wadudu hao pia wameonekana kwenye mataifa jirani ya Eritrea, Sudan Kusini, Ethiopia, Somalia na Uganda. Ifahamike kuwa mwaka 2016 viwavijeshi vilionekana kwenye mataifa 6 pekee barani Afrika. Viwavijeshi vina uwezo wa kuvamia na kukomba mazao ya mahindi, ngano, mtama, shayiri na nyasi.
Kulingana na taarifa za shirika la Umoja wa Mataifa la Kilimo na Chakula, FAO, viwavi jeshi vimeonekana katika kaunti 23 nchini Kenya.
Haya yanajiri wakati ambapo taifa na eneo zima la pembe ya Afrika linashusha pumzi kufuatia kipindi kirefu cha kiangazi na ukame.
Viwavijeshi ni tishio kubwa
Kwa mujibu wa mwakilishi wa FAO nchini Kenya, Carla Mucavi, wadudu wanaoathiri mimea na mifugo wanaoibuka tena ni tishio kubwa kwa upatikanaji wa uhakika wa chakula na lishe na, “Madhumuni ya mafunzo haya ni kuwapa ujuzi wakufunzi ili waweze kusambaza maelezo ….mbinu za uangalizi na udhibiti wa viwavijeshi ili kuhakikisha kuwa tuko na nyenzo za kupambana na wadudu hao na kuondoa kitisho.”
FAO imekuwa ikiwapa maafisa wa serikali ujuzi wa kutambua, kufuatilia na kufanya uangalizi ili kuwadhibiti viwavijeshi ardhini na angani.
Ili kulipa nguvu suala hilo, wiki hii FAO imehitimisha mjini Naivasha kongamano la siku nne la mafunzo kwa maafisa wa kilimo kutokea Ethiopia,Kenya,Somalia, Sudan Kusini na Uganda.
Kadhalika FAO iko kwenye harakati za kununua vifaa vya teknolojia itakavyowakabidhi wadau wa kilimo. Ifahamike kuwa wadudu wengi aghalabu huvuka mipaka na kusababisha madhara makubwa mashambani na kuvamia mimea kama mahindi, mtama, mawele,mchele, ngano, tefi na shayiri.
Ukame, Kiangazi na mvua haba
Itakumbukwa kuwa eneo la pembe ya Afrika limepitia misimu mitano mfululizo ya ukame na mvua haba hali inayosababisha mazingira ya hatari.
Kwenye uzinduzi wa mradi huo wa kupambana na viwavijeshi mwezi wa Machi mwaka huu, mwanzoni mwa msimu wa kupanda, kaunti ya Bungoma iliingia ubia na shirika la FAO, ili kuwaandaa wakulima.
Mwaka uliopita, mashamba mengi ya mahindi katika maeneo ya Bumala, Sirisia, Kanduyi na Mlima Elgon yalivamiwa na viwavijeshi ambavyo viliathiri mazao.
Afisa mkuu wa kilimo katika kaunti ya Bungoma Monica Fedha aliipongeza FAO kwa kuiteua Kenya kuwa muongozo wa mapambano dhidi ya viwavijeshi kwani,”Hawa viwavijeshi huathiri mahindi na wakati mwengine hata roho ya mahindi pia inaoza...hata nafaka za mahindi zinapovunwa huwa zinaonekana zimeoza kwasababu ya viwavijeshi.Huyu mdudu aitwaye kiwavijeshi ana uwezo wa kukomba mazao ya mahindi kwa asilimia 10 hadi 50.” anasimulia.
App ya FAMEWS.
Kwa upande wake, shirika la FAO, limeunda App maalum ya uangalizi na ufuatiliaji wa viwavijeshi. App hiyo ina uwezo wa kukusanya takwimu kuhusu viwavijeshi na wadudu wengine kadri wanavyoonekana jambo linaloifanyia wepesi shughuli ya kuwatambua, kuwafuatilia na kusambaza tahadhari ya mapema ili wahusika wajiandae.
Wakati huohuo, idara ya ulinzi wa mimea na usalama wa chakula nchini Kenya, KEPHIS, inashirikiana na idara ya wanyamapori, KWS, kuwaangamiza wadudu hao ambao wanatumia maeneo ya mbugani kuzaliana.
FAO inashirikiana na idara husika kupambana na viwavijeshi hivyo. Kwenye kongamano la mafunzo kwa maafisa wa kilimo lililofanyika mjini Naivasha wiki hii, mkurugenzi katika idara ya ulinzi wa mimea na usalama wa chakula nchini Kenya, KEPHIS, Collins Marangu, aliweka bayana kuwa mbinu za tahadhari za mapema zina mchango mkubwa katika kuzuwia wadudu hao kusambaa.
Kauli hizo zinaungwa mkono na Mkurugenzi wa idara ya uzalishaji wa chakula na mimea katika shirika la FAO, Dkt. Jingyuan Xia ambaye amebainisha kuwa FAO imeteua mataifa 8 kuwa kielelezo cha miradi ya kupambana na viwavijeshi.
Kwa mtazamo wake, Xia aliusisitizia umuhimu wa kubadilishana taarifa mapema miongoni mwa wakulima ili wajiandae chini ya uongozi wa wizara na idara za kilimo za kaunti ambako kwa sasa,”Tumeteua mataifa 8 kuwa sehemu ambazo mradi wa kupambana na viwavijeshi utaanzishwa kama kielelezo. Kenya ni moja ya mataifa hayo yatakayokuwa mstari wa mbele,” anafafanua.
Takwimu zinaashiria kuwa juhudi za uangalizi zimewawezesha kuyafuatilia maeneo ya ukubwa wa ekari 296,679 ambayo hayajavamiwa na viwavijeshi.
Mbinu inayofanya kazi ni unyunyizaji wa dawa kwenye mchanga.Wimbi la kwanza la uvamizi wa viwavijeshi liliripotiwa Novemba mwaka 2022.
Imeandaliwa na Thelma Mwadzaya-Nairobi Kenya