Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Takriban watu milioni 1 wamefurushwa makwao DRC nusu ya kwanza ya 2023: IOM

Familia iliyofukuzwa kazi kutoka DRC imeketi nje ya makazi ya muda katika kambi ya wakimbizi.
© UNHCR/Hélène Caux Familia moja iliyokimbia makazi yao sasa inaishi katika kambi ya muda huko Plain Savo, nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Takriban watu milioni 1 wamefurushwa makwao DRC nusu ya kwanza ya 2023: IOM

Wahamiaji na Wakimbizi

Ongezeko la mashambulizi dhidi ya raia yanayofanywa na makundi yenye silaha yasiyo ya kiserikali yamesababisha takriban watu milioni 1 kuyahama makazi yao nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC, tangu Januari mwaka huu kulingana na kitengo cha DTM cha ufuatiliaji wa takwimu za watu waliotawanywa  cha shirika la Umoja wa Mataifa la uahamiaji IOM.

Watu wapatao milioni 6.1 kwa sasa ni wakimbizi wa ndani nchini DRC, ikiwa ni ongezeko la asilimia 17 tangu Oktoba 2022.

IOM inasema tangu mwanzoni mwa mwaka huu, raia wameathiriwa kwa kiasi kikubwa na ghasia na mashambulizi ya kikatili yanayofanywa na makundi yasiyo ya kiserikali yenye silaha mashariki mwa DRC, na kusababisha hasara ya kwatu kupoteza maisha, kulazimika kufungasha virako Kwenda kusaka usalama, na kuongezeka kwa hali ya kutokuwa na utulivu. 

Wakati mzozo unavyozidi kuongezeka nchini humo nayo hali ya kibinadamu inaendelea kuzorota, na mamilioni wanakabiliwa na uhaba mkubwa wa chakula pamoja na mahitaji mengine muhimu.

Watoto wanne wadogo wa Kiafrika wamesimama kwa safu mbele ya nyumba rahisi yenye paa la nyasi na kuta za matope katika mazingira ya vijijini.
UNHCR Video Solange, (kushoto) akiwa na ndugu zake. Mama yao aliuawa kwenye nyumba jirani na makazi yao na sasa kwa hofu iliyowakumba wanaamua kulala mjini Bule na mchana wanakuwa kambini Plain Savo.

Watu wanaendelea kuuawa

Kwa mujibu wa IOM tarehe 11 Juni, takriban watu 46 waliuawa, wakiwemo watoto, na wengine kujeruhiwa kufuatia shambulio la kundi lenye silaha kwenye kambi ya wakimbizi wa ndani ya Lala iliyoko Mashariki mwa jimbo la Ituri. Shambulio hilo, lililoripotiwa kutekelezwa na kundi lisilo la serikali la CODECO (Coopérative pour le développement du Congo), pia limesababisha wakimbizi wa zaidi ya 7,800 kuhama tena kutoka eneo hilo, uharibifu wa makazi na mali za watu binafsi. 

IOM inalaani vikali ukiukaji huu mkubwa wa sheria za kimataifa za binadamu na inakumbusha kwamba mashambulizi dhidi ya raia yanaweza kuwa uhalifu wa kivita.Mkurugenzi wa idara ya dharura wa IOM Federico Sida amesema "Shambulio hili baya la hivi karibuni ni uthibitisho wa hatari zisizovumilika ambazo watu waliokimbia makazi yao nchini DRC wanakabiliana nazo kila siku. IOM inalaani vikali ukiukaji huu mbaya wa sheria za kimataifa za kibinadamu na inakumbusha kwamba mashambulizi dhidi ya raia yanaweza kuwa uhalifu wa kivita. Juhudi za pamoja zinahitajika sana kukomesha ghasia na kusaidia watu wa Congo kupata amani."

Msichana mdogo ameketi nje ya hema jeupe katika kambi ya watu waliokimbia makazi yao, akila kutoka kwenye bakuli la bluu.
© UNICEF/Jospin Benekire Mtoto akila chakula katika kambi ya wakimbizi wa ndani Kivu Kaskazini nchini DRC

Watu zaidi ya milioni 26 wanahitaji msaada

Kote nchini, DRC shirika hilo la uhamiaji linasema zaidi ya watu milioni 26 wanahitaji misaada ya kibinadamu. 

Licha ya ukosefu wa usalama, na ufikiaji mdogo wa misaada ya kibinadamu katika baadhi ya maeneo ya nchi hiyo, IOM na washirika wake wamekuwa wakijitahidi kutoa misaada ya dharura kwa wale waliokimbia makazi yao na wale walioathiriwa na ghasia na kuendelea kujitolea kukaa na kutoa msaada kwa watu wa Congo kulingana na mpango wake. 

Mpango ambao ni wa Kukabiliana na migogoro.

Kutokana na mwingiliano wa changamoto za kisiasa, kibinadamu, na kiuchumi katika maeneo mbalimbali ya DRC, IOM imetangaza kuongezeka kwa operesheni zake nchini humo. 

Hii itawezesha kuchukuliwa hatua nzuri zaidi za kukabiliana na dharura ya kibinadamu inayosababishwa na kuongezeka kwa ghasia.