Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UN yaadhimisha siku ya usalama wa chakula duniani ikihimiza viwango bora huokoa maisha

Mwanamke na mtoto mdogo wako katika kambi ya misaada nchini Msumbiji baada ya vimbunga. Mwanamke anaandaa chakula kwenye kikapu huku mtoto akiwa amesimama karibu.
UN Photo/Eskinder Debebe Usalama wa chakula una jukumu muhimu la kuhakikisha chakula kinakuwa salama katika kila hatua ya mnyororo wa chakula

UN yaadhimisha siku ya usalama wa chakula duniani ikihimiza viwango bora huokoa maisha

Afya

Leo ni siku ya usalama wa chakula duniani mwaka huu ikibeba kaulimbiu “Viwango vya chakula huokoa Maisha” ikilenga kuchagiza mwenendo na viwango vya usalama ambavyo hupunguza hatari ya uchafuzi wa chakula.

Kwa mujibu wa shirika la Umoja wa Mataifa la afya duniani WHO na lile la chakula na kilimo FAO ambao huibeba siku hii lengo kubwa ni kuongeza habari na taarifa kuhusu hatari ya sumu ya chakula na uchafuzi, ambayo inaua watu 420,000 kila mwaka huku vifo 125,000 miongoni mwao vikiwa ni vya Watoto wa umri wa chini ya miaka mitano.

Na takwimu za mashirika hayo zinaonyesha kuwa kila mwaka kuna angalau kesi 600,000 za magonjwa unaosababishwa na chakula ambacho huandaliwa bila hata usalama mdogo.

Pia mashirika hayo yamesema watu mafukara na walio hatarini zaidi mara nyingi ndio wanaoathirika zaidi wakiwemo wanawake na watoto.

FAO imetoa wito wa “kuitumia siku hii muhimu kutanabaisha kuhusu umakini na kuhamasisha hatua za kusaidia kuzuia, kugundua na kudhibiti hatari zinazotokana na chakula, kuchangia uhakika wa chakula, afya ya binadamu, ustawi wa kiuchumi, kilimo, upatikanaji wa soko, utalii na maendeleo endelevu.”

Nalo shirika la WHO limesisitiza kuwa “Siku hii ya kimataifa ni fursa ya kuimarisha juhudi za kuhakikisha kuwa chakula tunachokula ni salama, usalama wa chakula katika mfumo wa umma wa chakula na kupunguza mzigo wa magonjwa yanayotokana na chakula duniani.”

Kwa kutambua umuhimu wa kuhakikisha usalama kwa chakula duniani kote FAO pia imezindua imezindua nyenzo za kina, za vitendo na zinachoweza kufikiwa zilizoundwa ili kuwasaidia wale wote wanaofanya kazi katika sekta ya chakula kuzingatia viwango vya kimataifa vya usafi wa chakula.

Siku ya usalama wa chakula duniani huazimishwa kila mwaka Juni 7 tangu ilipopitishwa rasmi mwaka 2018.