Zaidi ya matukio 300,000 ya ukatili dhidi ya watoto walio katika migogoro yathibitishwa duniani kote
Zaidi ya matukio 300,000 ya ukatili dhidi ya watoto walio katika migogoro yathibitishwa duniani kote
Matukio 315,000 ya ukiukwaji haki dhidi ya watoto walio katika migogoro yamethibitishwa na Umoja wa Mataifa kati ya mwaka 2005 na mwaka 2022, hicho kikiwa ni kielelezo tosha cha athari mbaya za vita na migogoro kwa Watoto, imeeleza taarifa ya shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto, UNICEF iliyotolewa leo jijini New York, Marekani na katika mji mkuu wa Norway, Oslo ambako leo na kesho unafanyika mkutano kuhusu Kulinda Watoto katika Migogoro yenye kutumia Silaha.
Wakati mataifa, wafadhili na jumuiya ya misaada ya kibinadamu wakikutana nchini Norway kwa ajili ya Mkutano huo wa Oslo wa Kulinda Watoto katika Migogoro yenye kutumia Silaha, UNICEF imeripoti kwamba, tangu ufuatiliaji wa matukio ya ukikukwaji wa haki za Watoto katika maeneo yenye mizozo uanze mwaka 2005, Umoja wa Mataifa umethibitisha ukiukwaji mkubwa 315,000 uliofanywa na pande zinazozozana katika zaidi ya maeneo 30 ya migogoro barani Afrika, Asia, Mashariki ya Kati na Amerika Kusini.
Matukio haya ya ukatili dhidi ya watoto ni pamoja na, zaidi ya watoto 120,000 kuuawa au kulemazwa, takribani watoto 105,000 waliandikishwa au kutumiwa na vikosi vya kijeshi au vikundi vyenye silaha, zaidi ya watoto 32,500 walitekwa nyara, na zaidi ya watoto 16,000 walifanyiwa ukatili wa kijinsia.
Umoja wa Mataifa pia umethibitisha zaidi ya mashambulizi 16,000 dhidi ya shule na hospitali, na zaidi ya matukio 22,000 ya kunyimwa haki za kibinadamu kwa watoto.
Idadi hii ni visa vile tu ambavyo vimethibitishwa, vinginevyo UNICEF inadhani kwamba idadi inaweza kuwa ni ya juu zaidi.
Zaidi ya hayo, UNICEF inaeleza kuwa mamilioni ya watoto zaidi wamefurushwa kutoka katika nyumba na jumii zao, wamepoteza marafiki au familia au wametenganishwa na wazazi au walezi.
"Vita yoyote ile hatimaye ni vita dhidi ya watoto," anasema Mkurugenzi Mtendaji wa UNICEF Catherine Russell akiongeza kwamba "Kukabiliwa na migogoro kuna athari mbaya na kunabadilisha maisha kwa watoto.”
Anasema, “Ingawa tunajua nini kifanyike ili kuwalinda watoto dhidi ya vita, ulimwengu haufanyi vya kutosha. Mwaka baada ya mwaka, Umoja wa Mataifa unaandika njia zinazoonekana, za kutisha na zinazoweza kutabirika ambazo maisha ya watoto yanasambaratika. Ni wajibu wetu sote kuhakikisha kwamba watoto hawalipi gharama ya vita ya watu wazima, na kuchukua hatua madhubuti zinazohitajika ili kuboresha ulinzi wa baadhi ya watoto walio hatarini zaidi duniani.”
Urekebishaji tabia askari watoto
Katika muktadha huu, UNICEF imeunga mkono utunzaji na ulinzi wa mamilioni ya watoto walioathiriwa katika hali ya migogoro ili kuimarisha ustawi wao, ikiwa ni pamoja na kupitia utoaji wa huduma ya afya ya akili na usaidizi wa kisaikolojia, ufuatiliaji na kuunganishwa kwa familia, na huduma kwa watoto walionusurika katika ukatili wa kijinsia. Mnamo mwaka wa 2022, UNICEF ilifikia karibu watoto 12,500 ambao waliondoka kwenye vikosi vya jeshi au vikundi vyenye silaha kwa kuwaunganishwa ten ana jamii zao au msaada mwingine wa ulinzi, na zaidi ya watoto milioni 9 wakapewa taarifa ambazo wanaweza kutumia kujilinda dhidi ya mabaki ya vilipuzi vya vita.
Kwa bahati mbaya, ukubwa wa hatari za ulinzi wa mtoto kwa watoto walioathiriwa na migogoro haulingani na kiwango cha fedha kinachopatikana kushughulikia masuala haya. Uchambuzi mpya wa Utabiri wa Ufadhili wa Kibinadamu, ulioidhinishwa na UNICEF, Save the Children, Alliance for Child Protection in Humanitarian Action na Global Child Protection Area of Responsibility, unaonesha kuwa kufikia mwaka 2024, sekta ya ulinzi wa mtoto itahitaji dola za Marekani bilioni 1.05, ikiongezeka hadi Dola bilioni 1.37 ifikapo mwaka 2026, kushughulikia mahitaji ya ulinzi wa watoto katika vita yenye matumizi ya silaha. Hii ni pamoja na huduma muhimu kama vile kuunganisha familia, usaidizi wa afya ya akili na kuzuia kuajiriwa katika vikundi vilivyo na silaha.
Ufadhili mdogo
Hata hivyo, utafiti pia unaonesha upungufu wa fedha unaokuja. Iwapo kasi ya sasa ya ufadhili wa kibinadamu itaendelea, upungufu unaotarajiwa utafikia kuwa dola za Marekani milioni 835 mwaka 2024, na kuongezeka hadi dola za Marekani milioni 941 ifikapo 2026. Pengo hili linaweza kuwaacha watoto walioathiriwa na migogoro katika mazingira ya athari za haraka na za kudumu za vita, ajira ya watoto, biashara, na vurugu.
Wakati viongozi wanakutana Oslo, UNICEF inatoa wito kwa serikali kufanya ahadi mpya kwa:
Kudumisha na kutekeleza sheria na kanuni za kimataifa ambazo tayari zimetumika kulinda watoto katika vita, ikiwa ni pamoja na kulinda shule, hospitali na vitu vingine vinavyolindwa kama vile miundombinu ya maji na usafi wa mazingira dhidi ya mashambulizi, kukomesha uandikishaji na utumiaji wa watoto na vikundi na vikosi vyenye silaha kukomesha matumizi ya silaha za milipuko katika maeneo yenye watu wengi.
Kuwawajibisha wahalifu haki za watoto zinapokiukwa.
Kuongeza rasilimali muhimu ili kufadhili ulinzi wa watoto walio kwenye migogoro kwa kiwango na kasi inayohitajika, kulingana na hitaji linalokua. Hii lazima ijumuishe uwekezaji katika mwitikio wa kibinadamu na katika nguvu kazi ya kitaifa ya ulinzi wa watoto.
UNICEF pia inatoa wito kwa wahusika wa kibinadamu kuwekeza katika sera zinazoweka watoto na ulinzi wao katikati ya hatua za kibinadamu katika hali ya migogoro ya silaha.
"Lazima tutoe jibu la ulinzi wa mtoto ambalo ni sawa na changamoto tunazokabiliana nazo," Russell aamesema akiongeza kwamba "Tunahitaji kufanya kila tuwezalo kufikia watoto wote wenye uhitaji, hasa walio hatarini zaidi. Huduma za ulinzi kwa watoto lazima zijenge juu ya mifumo iliyopo na miundo ya jumuiya, na zisaidie haki za watoto, ushiriki na maslahi yao bora. Mipango na utetezi katika miktadha hii lazima iweke watoto na ulinzi wao katikati ya hatua za kibinadamu."