Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ongezeko kubwa la uhalifu wa kimataifa na dawa bandia Asia linahitaji ushirikiano wa kimataifa

Kikosi cha wanamaji wa Thailand cha Mekong Riverine kikiwa katika doria  kwenye mpaka kati ya  Thailand na Myanmar na Laos.
UN News/Daniel Dickinson
Kikosi cha wanamaji wa Thailand cha Mekong Riverine kikiwa katika doria kwenye mpaka kati ya Thailand na Myanmar na Laos.

Ongezeko kubwa la uhalifu wa kimataifa na dawa bandia Asia linahitaji ushirikiano wa kimataifa

Sheria na Kuzuia Uhalifu

Usafirishaji haramu wa dawa za kulevya, kemikali, mbao na wanyamapori, watu na bidhaa haramu kote Kusini-mashariki mwa Asia unashughulikiwa kutokana na uungwaji mkono wa ofisi maalum ya Umoja wa Mataifa inayohusika na dawa za kulevya na uhalifu UNODC.

Jeshi la wanamaji la Thailand  limezindua usafiri kwa mwendo wa kasi chini ya maji yenye matope ya kahawia ya Mto Mekong karibu na mji wa mpakani wa Chiang Saen kaskazini mwa Thailand.

Kulia ni Laos, ambako miradi mikubwa ya ujenzi inayofadhiliwa na uwekezaji wa kigeni inachipuka kutoka kwenye vichaka vilivyoko kando ya mto na mbele upande wa kushoto ni misitu minene ya Myanmar.

Huu ni ufalme wa Pembetatu ya dhahabu ambapo kihistoria kasumba ililimwa ili kuzalisha mihadarati aina ya heroini kwa ajili ya kuuza nje ya nchi lakini katika miaka ya hivi karibuni, biashara ya dawa bandia hatari zaidi na zenye faida zaidi imechukua nafasi.

Thailand, Laos na Myanmar ziko mstari wa mbele katika biashara haramu barani Asia inayotawaliwa na magenge au vikundi vya uhalifu wa kimataifa.

Kuzinmgirwa kwa mto

Wafanyakazi kwenye boti ya Thai wanachangamka kufuatia kunaswa kwa hivi karibuni tembe milioni 6.4 za dawa iliyopigwa marufuku na inayolevya sana ya methamphetamine, inayojulikana nchini humo kama yaba.

"Nilishangaa lakini pia nilifurahishwa sana kwamba tulikamata kiasi hiki cha yaba," Kapteni Phakorn Maniam mkuu wa operesheni na idara ya ujasusi wa kitengo cha Mekong Riverine, Royal Thai Navy ameiambia UN News.

“Kwa kawaida kiasi hiki cha dawa za kulevya hukamatwa nchi kavu ni operesheni ngumu ya kuwakamata wahalifu katikati ya mto," amesema, "na kwa hivyo ninajivunia wafanyikazi wetu, ambao wamejitolea sana kulinda nchi yetu na watu wetu."

Kapteni Phakorn Maniam amepelekwa kwenye kikosi cha wanamaji cha Thailand cha Mekong Riverine
UN News/Daniel Dickinson
Kapteni Phakorn Maniam amepelekwa kwenye kikosi cha wanamaji cha Thailand cha Mekong Riverine

Maili chache chini ya mto katika mji mdogo wa Houay Xai upande wa Laos wa Mekong, mamlaka za mpakani zinasherehekea ukamataji wao wenyewe ambao ni muhimu wa dawa za kulevya, usiku uliopita kufuatia kutonywa, doria ya kijeshi ya nchi kavu ilikamata walanguzi wa dawa za kulevya wakiwa wamebeba kilo 500 za methi ya fuwele. Mwezi uliopita tembe milioni 7.1 za methamphetamine pia zilikuwa zimenaswa katika eneo hilohilo.

Dawa hizo zilizofuatiliwa nchini Laos na Thailand zilitoka katika maabara za viwanda haramu zinazoendeshwa na wanamgambo na magenge ya wahalifu katika misitu ya mbali ya milima ya kaskazini mwa jimbo la Shan nchini Myanmar na zilikuwa zikipitishwa kupitia nchi zote mbili hadi mji mkuu wa Thailand, Bangkok, lakini pia kuvuka.

Asia ya Kusini-Mashariki na masoko ya mbali yenye faida kubwa ikiwa ni pamoja na Japan, Korea Kusini, New Zealand na Australia.

Ni vigumu kuhesabu kwa uhakika ni kiasi gani cha madawa ya kulevya yanatengenezwa nchini Myanmar, lakini baadhi ya makadirio yanaonyesha kuwa mamia ya tani zinasafirishwa nje ya nchi.

Licha ya utiririshaji wa dawa za kulevya unaoonekana kutokomea, mamlaka za Thailand na Lao zinapata baadhi ya mafanikio kutokana na msaada wa ofisi ya Umoja wa Mataifa ya (UNODC) ambayo inakuza mtandao wa kukusanya taarifa za kijasusi za kikanda.

Afisa uhusiano wa masuala ya mpakani Laos
UN News/Daniel Dickinson
Afisa uhusiano wa masuala ya mpakani Laos

Afisa C, ambaye yuko Houay Xai na mamlaka ya Lao na ambaye hakutaka jina lake litajwe kwa sababu za kiusalama, aamesema kuwa kushirikiana na vyombo vya kutekeleza sheria katika mpaka wa Thailand kupitia simu za kawaida, mikutano ya ana kwa ana na mawasiliano mengine huboresha hatua za biashara haramu.

"Kwa ushirikiano huu wa kuvuka mpaka na upashanaji habari, tumeweza kukabiliana na ulanguzi wa mihadarati na pia aina nyingine za uhalifu uliopangwa wa kimataifa."

Mamlaka zinazopambana na uhalifu nchini Thailand na Laos zinashirikiana kwa karibu zaidi kutokana na Mpango wa UNODC wa Kusimamia Mipaka wa Kikanda ambapo mtandao wa ofisi za uhusiano wa mpakani au BLOs ulianzishwa ili kuimarisha ushirikiano wa kuvuka mpaka na upashanaji habari.

Mtandao wa zaidi ya BLOs 120 unaenea kote Asia ya Kusini-Mashariki kutoka Myanmar upande wa magharibi hadi Uchina upande wa mashariki na Indonesia upande wa kusini na pia inajumuisha Thailand, Cambodia na Viet Nam.

BLOs zinaimarishwa kwa msaada wa UNODC ili kukabiliana na kile ambacho Mwakilishi wa Wakala wa Kanda ya Kusini-Mashariki mwa Asia na Pasifiki, Jeremy Douglas, anaiita "moja ya njia kubwa zaidi za biashara ya dawa za kulevya duniani."

Nchi tatu Thailand, Myanmar na Laos zinashirikiana katika pembe tatu ya dhahabu
UN News/Daniel Dickinson
Nchi tatu Thailand, Myanmar na Laos zinashirikiana katika pembe tatu ya dhahabu

Changamoto za kuvuruga biashara hii ya kimataifa ni kubwa kulingana na Bwana Douglas: “Kuna masuala tata ya utawala yanayoshughulikiwa katika eneo la Pembetatu ya dhahabu na ndani ya Myanmar, kukiwa na makundi yaliyogawanyika yenye silaha na wanamgambo wanaojihusisha na biashara ya dawa za kulevya na biashara nyingine haramu zinazodhibiti eneo hilo, " amesema.

Na kuongeza kuwa "Wakati huo huo, vikundi hivi vinafanya kazi katika maeneo ya mbali sana, na katika hali zingine kando ya mipaka iliyo wazi sana. Ni rahisi kusafirisha dawa za kulevya na bidhaa haramu ndani na nje ya Myanmar, na hali ni ngumu sana kwa majirani zake kushughulikia.”

Ongezeko la uzalishaji wa dawa bandia hivi karibuni limekuwa halina kifani kulingana na mwakilishi wa Kanda wa UNODC ambaye anaamini kuwa ushirikiano kati ya nchi ni "msingi" katika kuzuia usafirishaji: "Hili ni jukumu la pamoja; kushughulikia uhalifu wa kimataifa kunahitaji mataifa kushirikiana ili kukabiliana haraka na kile kinachotokea, hasa katika maeneo ya mpakani.”

Sio tu madawa ya kulevya ambayo yanasafirishwa kote katika kanda lakini pia viambatanisho vya kemikali vya kutengeneza dawa za sanisi vinasafirishwa kwenda Myanmar kinyume cha sheria kwa idadi kubwa zaidi kuliko dawa zinazouzwa nje pia usafirishaji haramu wa watu, wanyamapori, mbao na silaha unafanyika.

Katika mazingira magumu na yenye matatizo kama haya, ujuzi mpya unahitajika ili kukabiliana na changamoto mpya imesema ofisi ya UNODC Kama sehemu ya usaidizi wake wa BLO,.

UNODC pia imeanzisha ushirikiano wa mafunzo na mashirika kote Kusini-mashariki mwa Asia.

Katika Barabara kuu ya 1, takriban kilomita 40 kusini mwa mpaka wa Thailand na Myanmar Luteni kanali wa Polisi Amonrat Wathanakhosit anawapeleka wanafunzi wake katika mazoezi ya vitendo yanayolenga kupekua magari kwa ajili ya kubaini magendo.

"Wanafunzi wetu wanatumia bidhaa za maarifa za UNODC na mafunzo na kujifunza jinsi ya kuhoji madereva, na wanazoea jinsi wanavyoendesha. Wanafunzi wetu wanakuwa na ujasiri zaidi juu ya kutambua madereva gani wanaweza kuwa wanaficha dawa bandia.”

Afisa wa polisi wa Thailand anasimamisha gari katika kituo cha ukaguzi kilometa 40 kusini mwa mpaka wa Thailand na Myanmar
UN News/Daniel Dickinson
Afisa wa polisi wa Thailand anasimamisha gari katika kituo cha ukaguzi kilometa 40 kusini mwa mpaka wa Thailand na Myanmar

Tofauti na heroini, utengenezaji wake ambao unazuiliwa na mzunguko wa asili wa ongezeko la afyuni poppy, methamphetamine inaweza kutengenezwa kwa hiari yake mradi tu kitangulizi na kemikali nyingine zipatikane.

Ushirikiano wa serikali kwa msaada wa UNODC unasaidia kuzuia utiririshaji wa dawa za kulevya, hata kama inakubalika na wengi kuwa kunasa kunawakilisha asilimia ndogo tu ya dawa zinazouzwa kote katika kanda hiyo.

Maafisa kama Luteni Kanali Amonrat Wathanakhosit wanatambua changamoto hizo lakini bila shaka anawazungumzia wengi katika eneo hilo akisema "kazi yangu ya kujaribu kukomesha dawa za kulevya ni muhimu kwa usalama wa nchi yangu."

Hatua zilizochukuliwa

• Baadhi ya BLOs 120 zimeanzishwa kote Asia ya Kusini-Mashariki.

• BLOs zimeundwa kwa jozi, katika upande wowote wa mpaka wa kimataifa.

• BLOs hushughulikia masuala mengi tofauti ya mipakani ikiwa ni pamoja na: biashara ya dawa za kulevya na kemikali, ulanguzi wa wahamiaji na usafirishaji haramu wa watu, uhalifu wa wanyamapori na misitu, na katika baadhi ya maeneo harakati za wapiganaji wa kigaidi, pamoja na afya ya umma na magonjwa yanayohusiana na janga la coronavirus">COVID-19.

• Mtandao wa BLO pia unafanya kazi ili kuimarisha uhusiano kati ya watekelezaji sheria na jumuiya za mpakani, juhudi za polisi jamii na kuunga mkono jukumu na uongozi wa wanawake katika mashirika ya kutekeleza sheria.