Mifumo ya Akili Bandia, (AI) yagongesha vichwa mawaziri wa elimu

Mifumo ya Akili Bandia, (AI) yagongesha vichwa mawaziri wa elimu
Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni, UNESCO limeanzisha mchakato wa kujadili fursa, changamoto na hatari za mifumo zalishi ya akili bandia katika mifumo ya elimu duniani.
UNESCO imefanya hivyo wakati wa mkutano kwa njia ya mtandao na mawaziri wa elimu kutoka nchi wanachama wa shirika hilo, mkutano uliofanyika mwishoni mwa mwezi Mei mwaka huu.
Mbinu zalishi za akili bandia, AI zinatoa fursa mpya kwenye elimu, sambamba na changamoto, imesema UNESCO kupitia taarifa yake iliyotolewa leo huko Paris, Ufaransa.
“Hata hivyo tunahitaji kuchukua hatua za dharura kuhakikisha mbinu mpya zalishi za akili bandia zinajumuishwa kwenye elimu kupitia vigezo vyetu. Ni wajibu wetu kupatia kipaumbele usalama, ujumuishi, utofauti, uwazi na ubora kama ilivyoelezwa kwenye mapendekezo ya UNESCO kuhusu Maadili ya Akili Bandia yaliyopitishwa kwa kauli moja na nchi wanachama,” amesema Stefania Giannini, Mkurugenzi Msaidizi wa Elimu ndani ya UNESCO.

Mawaziri wamulika changamoto kubwa na kushirikishana sera
Wakati wa mjadala, ilibainika kuweko kwa shaka na shuku za pamoja kutoka kwa mawaziri hao kuhusu jinsi ya kuhakikisha mifumo ya elimu inahimili vurugu itokanayo na akili bandia, AI kwenye mitaala ya elimu, mbinu za kufundishia, mitihani na jinsi ya kupunguza matatizo yaletwayo na teknolojia kama vile kuepusha kusambazwa kwa taarifa zinazoegemea upande mmoja.
Mjadala huo wa mawaziri ulibaini kuwa serikali duniani kote ziko kwenye mchakato wa kutunga sera sahihi za kukabiliana na kuibuka kwa mazingira ya akili bandia kwenye mifumo ya elimu.
Hivyo zinataka kutunga mikakati ya kitaifa kuhusu Akili Bandia, AI, ulinzi wa data na mifumo mingine ya usimamizi.
Asilimia 10 ya shule na Vyuo Vikuu vina mwongozo rasmi kuhusu AI
Utafifi mpya uliofanywa na UNESCO katika zaidi ya shule na Vyuo Vikuu 450 duniani umebaini kuwa chini ya asilimia 10 ya shule na vyuo hivyo vimetunga sera za kitaasisi au mwongozo rasmi wa jinsi ya kutumia mifumo ya akili bandia au AI.
Matokeo haya yanaonesha kuwa hatua za haraka zinahitajika kushughulikia kuibuka kwa mbinu hizi zenye nguvu za akili bandia ambazo zinaweza kuzalisha maandishi na picha bunifu ni changamoto kubwa kwa taasisi hizo.
Jukumu muhimu la walimu katika zama hizi mpya za ufundishaji lilimulikwa lakini walimu wanahitaji mwongozo na mafunzo ili kubaliana na changamoto mpya.

Mwongozo wa kisera wa UNESCO na mifumo ya ueledi
UNESCO inasema itaendelea kuchagiza mazungumzo ya kimataifa na watunga sera, wadau wa teknolojia ya elimu, wanazuoni na mashirika ya kiraia.
Kwa sasa UNESCO inaandaa miongozo ya kisera juu ya matumizi ya AI kwenye elimu na utafiti, sambamba na mifumo ya AI kwa walimu na wanafunzi kwa ajili ya kuelimisha.
Miongozo hiyo itazinduliwa wakati wa Wiki ya Kujifunza Kidijitali itakayofanyika kwenye makao makuu ya UNESCO huko Paris, Ufaransa kuanzia tarehe 4 hadi 7 mwezi Septemba mwaka 2023.