Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Sheria ya LGBQI+ Uganda itarejesha nyuma harakati za kupambana na UKIMWI

Kampala, mji kuu wa  nchi ya Uganda
IMF/Esther Ruth Mbabazi
Kampala, mji kuu wa nchi ya Uganda

Sheria ya LGBQI+ Uganda itarejesha nyuma harakati za kupambana na UKIMWI

Afya

Serikali ya Uganda chini ya Rais wake Yoweri Museveni imepongezwa kwa juhudi za kuhakikisha wananchi wake wenye Virusi vya UKIMWI wanagundulika na kupatiwa huduma na katika kuendeleza hali hiyo imeombwa kujitafakari na kuhakikisha wananchi wanaoshiriki mapenzi ya jinsia moja hawaathiriki wala kunyanyapaliwa baada ya sheria mpya dhidi ya ushoga kutiwa saini na Rais kuwa sheria.

Wito huo wa pamoja umetolewa leo na mashirika matatu ya kimataifa kutoka jijini Geneva Uswisi na Washington DC Marekani ambapo yameeleza wasiwasi wao kuwa sheria mpya ya wapenzi wa jinsia moja italeta unyanyapaa na kusababisha wale wenye UKIMWI kushindwa kusaka huduma za matibabu na kupatiwa elimu ya kujikinga wao na wenza wao.

Mashirika hayo ni lile la Umoja wa Mataifa linalohusika na vita dhidi ya UKIMWI UNAIDS, Mfuko la kimataifa la ufadhili Global Fund na Mfuko wa Kimataifa wa UKIMWI, Kifua Kikuu na Malaria, PEPFAR.

Taarifa hiyo ya pamoja imesema “maendeleo ya Uganda katika mwitikio wake wa VVU sasa yako katika hatari kubwa kwani sheria ya Kupinga ushoga ya mwaka 2023 itazuia elimu ya afya na uchechemuzi ambao unaweza kusaidia kukomesha UKIMWI kama tishio kwa afya ya umma.”

Watu wameanza kuogopa kusaka huduma

Pamoja na kuwa Uganda imedhihirisha mara kwa mara uongozi na kujitolea kwake kukomesha UKIMWI pamoja na kujipatia mafanikio makubwa katika kampeni yake ya kutomuacha mtu yeyote nyuma unyanyapaa na ubaguzi unaohusishwa na kupitishwa kwa sheria hiyo tayari umesababisha kupunguza upatikanaji wa huduma za kinga na matibabu.

“Imani, usiri, na ushiriki usio na unyanyapaa ni muhimu kwa mtu yeyote anayetafuta huduma ya afya na watu LGBTQI+ nchini Uganda wanazidi kuhofia usalama wao, na idadi inayoongezeka ya watu wanakatishwa tamaa kutafuta huduma muhimu za afya kwa kuhofia kushambuliwa, kuadhibiwa na kutengwa zaidi.”

Maendeleo yanawezekana

Mashirika hayo kwa pamoja yametoa wito kwa sheria hiyo kuangaliwa upya ili Uganda iendelee na njia yake ya kuhakikisha upatikanaji wa huduma za afya kwa usawa na kukomesha UKIMWI kama tishio la afya ya umma ifikapo 2030.

“Tunajua kwamba tutaweza kuondokana na tishio hili la afya ya umma tunapohakikisha kwamba 95% ya watu wanaoishi na VVU wanajua hali yao, 95% yao wanatumia matibabu, na 95% ya wale wanaopata matibabu wamefanikiwa kukandamiza virusi Uganda wanaweza kufikia hilo.”

Hadi kufikia mwaka wa 2021, 89% ya watu wanaoishi na VVU nchini Uganda walikuwa wanajua hali yao, zaidi ya 92% ya watu ambao walijua hali yao ya VVU walikuwa wakipokea tiba ya kurefusha maisha, na 95% ya wale waliokuwa kwenye matibabu walikuwa wamekandamizwa na virusi. Uganda iko katika njia nzuri ya kufikia malengo ya UNAIDS ya matibabu ya VVU ikiwa maendeleo yanaweza kudumishwa.