Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Afrika fikiria upya kupanua wigo wa bidhaa za kuuza nje- UNCTAD

Wakulima wa karanga wa Kiafrika wanapata punguzo la bei ya rejareja wakati mazao yao yanauzwa katika maeneo kama Rumania (pichani).
World Bank
Wakulima wa karanga wa Kiafrika wanapata punguzo la bei ya rejareja wakati mazao yao yanauzwa katika maeneo kama Rumania (pichani).

Afrika fikiria upya kupanua wigo wa bidhaa za kuuza nje- UNCTAD

Ukuaji wa Kiuchumi

Hii leo ikiwa ni siku ya Afrika, Kamati ya Umoja wa Mataifa ya Biashara na Maendeleo, UNCTAD imesema siri ya kujikwamua kwa bara hilo kiuchumi ni kupanua wito wa bidhaa inazouza nje. 

 

Ripoti ya UNCTAD ya Maendeleo barani Afrika mwaka 2022 inaonesha kuwa uchumi barani humo umeendelea kusuasua ukichangiwa na ongezeko la bei za vyakula na nishati hasa zinapohaha kujikwamua kutoka katika janga la coronavirus">COVID-19, madhara ya mabadiliko ya tabianchi na vita nchini Ukraine. 

“Ili kuhimili majanga ya sasa na kujikinga dhidi ya changamoto za siku za usoni, Afrika lazima ipanue wigo wa uchumi wake. Bara hili lina watu bilioni 1.4 lakini liko nyuma zaidi katika kuwa na aina mbali mbali za vyanzo vya kuinua uchumi wake,” imesema ripoti hiyo. 

Bidhaa huchangia zaidi ya asilimia 60 ya mauzo ya nje ya nchi 45 kati ya 54 za bara la Afrika, na hivyo kuliacha bara hilo kuwa hatarini zaidi pindi bei za bidhaa duniani zinapoporomoka na hivyo kukandamiza matumaini ya ujumuishi wa Afrika katika maendeleo ya kiuchumi. 

Ripoti ya UNCTAD inaonesha kuwa kupuuza nafasi kubwa inayoweza kuleta mabadiliko kwa kutumia huduma zinazohitaji ufahamu wa hali ya juu au stadi za juu, kama vile teknolojia za habari na mawasiliano, biashara ya huduma na huduma za fedha kidijitali ndio moja ya sababu kuu zinazofanya Afrika kusalia nyuma katika kupanua wigo wa vyanzo vya kukuza uchumi wake. 

Sasa ripoti inataka Afrika lazima iondoe vikwazo kwenye biashara ya huduma kupitia Eneo huru la biashara Afrika, AfCTA, ikisema huo utakuwa msingi wa kuchagiza nafasi muhimu ya huduma katika kupanua wigo wa vyanzo vya kiuchumi barani Afrika. 

“Sera lazima ziweko ili kuchagiza ufikiaji jumuishi wa teknolojia bunifu na ufadhili kwa biashara ndogo na za kati” imesema UNCTAD. 

Akizungumzia ripoti hiyo, Rebecca Grynspan ambaye ni Katibu Mkuu wa UNCTAD, amesema Ripoti ya Maendeleo ya kiuchumi Afrika mwaka 2022, inaunganisha Afrika na minyororo ya thamani ya juu. Natumai ripoti hii itakuwa mwongozo wenye thamani kwa watunga sera katika kuchochea upanuaji wigo wa bidhaa na huduma zinazouzwa nje kwa kuwezesha biashara binafsi kuingia katika masoko mapya.