Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mtoro kinara katika mauaji ya kimbari Rwanda akamatwa Afrika Kusini

Kijana mwenye umri wa miaka 14 wa Kinyarwanda kutoka mji wa Nyamata,. Alipigwa picha mwaka 1994. Aliponea chupuchupu kuuawa  katika mauaji ya kimbari kwa kujificha katikati  ya maiti kwa siku mbili
UNICEF/UNI55086/Press
Kijana mwenye umri wa miaka 14 wa Kinyarwanda kutoka mji wa Nyamata,. Alipigwa picha mwaka 1994. Aliponea chupuchupu kuuawa katika mauaji ya kimbari kwa kujificha katikati ya maiti kwa siku mbili

Mtoro kinara katika mauaji ya kimbari Rwanda akamatwa Afrika Kusini

Sheria na Kuzuia Uhalifu

Baada ya kuwa mtoro kwa zaidi ya miaka 20, hatimaye Fulgence Kayishema, mmoja wa watuhumiwa vinara waliokuwa wanasakwa zaidi kwa kuhusika na mauaji ya kimbari nchini Rwanda, amekamatwa jana huko Paarl nchini Afrika Kusini kufuatia ushirikiano baina ya ofisi ya mwendesha mashtaka ya mfumo wa kimataifa wa kushughulikia mabaki ya kesi za mauaji ya kimbari, IRMCT na serikali ya Afrika Kusini.

Taarifa iliyotolewa na IRMCT inasema Kayishema anadaiwa kuongoza mauaji ya takribani wakimbizi 2000 wa kitutsi, wanawake, wanaume, watoto na wazee kwenye kanisa katoliki la Nyange wakati wa mauaji ya kimbari ya Watutsi nchini Rwanda mwaka 1994. 

Tuhuma dhidi ya Kayishema 

Akizungumzia kukamatwa kwa Kayishema, Mwendesha Mashtaka Mkuu wa IRMCT Serge Brammertz amesema “Fulgence Kayishema amekuwa mtoro kwa zaidi ya miaka 20. Kukamatwa kwake hatimaye kutamwezesha afikishwe mbele ya sheria kwa tuhuma za uhalifu zinazomkabili.” 

 Kayishema alishtakiwa na Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu nchini Rwanda (ICTR) mwaka 2001 kwa makosa ya mauaji ya kimbari, kufanikisha mauaji ya kimbari, kuchochea mauaji ya kimbari na uhalifu dhidi ya binadamu kwa mauaji na makosa mengine yaliyofanyika kwneye kitongoji cha Kivumu jimbo la Kibuye. 

Inadaiwa kuwa tarehe 15 mwezi Aprili mwaka 1994, Kayishema pamoja na watuhumiwa wengine waliua zaidi ya watu 2,000 kwenye kanisa hilo huko Nyange na inadaiwa kuwa alishiirki moja kwa moja katika kupanga na utekelezaji wa mauaji hayo ikiwemo kununua na kusambaza petroli na kuchoma moto kanisa ilhali wakimbizi hao walikuwemo ndani yake. 

Halikadhalika Kayishema na watuhumiwa hao wengine kwa siku mbili zilizofuatia walisimamia usafirishaji wa maiti kutoka kanisani hadi kwenye makaburi ya halaiki. 

Hatulali hadi watoro wote wakamatwe na haki itendeke 

Bwana Brammertz amesema leo ni siku ya kukumbuka waliouawa pamoja na manusura wa mauaji ya kimbari nchini Rwanda mwaka 1994. “Ingawa miaka 29 imepita, bado wanaendelea kubeba makovu ya kimwili na kifikra kutokana na machungu waliyopitia. Ofisi  yangu inasisitiza kwamba tutaendelea na juhudi zetu za kusaka haki kwa niaba yao, na kuendeleza jukumu letu la kuchangia katika mustakabali wenye haki na amani kwa wananchi wa Rwanda.” 

 Kukamatwa kwa Kayishema, ni hatua muhimu kufanikisha mkakati wa Ofisi ya Mwendesha Mashtaka ya IRMCT ya kuhakikisha watoro wote waliosalia wanakamatwa. 

Tangu mwaka 2020 ofisi ya ufuatiliaji wa watoro wa mauaji ya kimbari Rwanda ilibaini maeneo ya watoro watano wakiwemo Félicien Kabuga, Augustin Bizimana, Protais Mpiranya, na Phéneas Munyarugarama. Kwa sasa ambao bado watoro watatu.

UN yakaribisha kukamatwa kwa Kayishema 

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres amekaribisha kitendo cha kukamatwa kwa kinara mtoro wa mauaji ya kimbari nchini Rwanda Fulgence Kayishema huko Afrika Kusini akisema kukamatwa kwake kunatuma ujumbe mzito ya kwamba wote wanaotuhumiwa kutekeleza makosa kama hayo hawawezi kukwepa sheria kwani hatimaye watakamatwa hata baada yar obo karne baadaye. 

Kupitia taarifa iliyotolewa leo jijini New York, Marekani na msemaji wa Umoja wa Mataifa Stéphane Dujarric, Katibu Mkuu amepongeza ushirikiano kati ya mfumo wa kimataifa wa kushughulikia mabaki ya kesi za mauaji ya kimbari, IRMCT na mamlaka za Afrika Kusini uliowezesha kukamatwa kwa Kayishema. 

Amerejelea kuwa nchi zote zina wajibu wa kushirikiana na Mfumo huo katika kubaini watoro waliosalia waliko, kuwakamata, kuwasalimisha na kuwahamishia kule wanakotakiwa kwenda. 

Katibu Mkuu amesema fikra zake leo hii kwanza kabisa ni kwa waliouawa kutokana na tuhuma hizo zinazomkabili Kayishema, halikadhalika waliouawa na manusura wa uhalifu mwingine mkubwa wa kimataifa duniani kote na familia zao. 

“Kuondokana na ukwepaji sheria ni muhimu kwa ajili ya amani, usalama na haki,” ametamatisha Katibu Mkuu.