Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Sasa siendi tena benki bali napokea malipo ya masurufu kupitia simu ya kiganjani - Gehad 

Kuanzishwa kwa mfumo wa malipo ya fedha mtandaoni, sasa Gehad haendi tena benki kila mwezi kupokea malipo ya masurufu ya familia kutoka kwa baba yao. Hii ina maana sasa atakuwa hakosi tena vipindi vya shule asubuhi.
ITU
Kuanzishwa kwa mfumo wa malipo ya fedha mtandaoni, sasa Gehad haendi tena benki kila mwezi kupokea malipo ya masurufu ya familia kutoka kwa baba yao. Hii ina maana sasa atakuwa hakosi tena vipindi vya shule asubuhi.

Sasa siendi tena benki bali napokea malipo ya masurufu kupitia simu ya kiganjani - Gehad 

Ukuaji wa Kiuchumi

Misri, taifa lenye watu milioni 100 hivi sasa, lakini ni asilimia 30 tu ya watu hao yani watu milioni 36.8 ndio wenye akaunti za benki. 

Katika zama hizo za huduma za fedha kimtandao, mashirika ya mawasiliano ya simu yanaingia ubia na benki ili kupanua wigo wa huduma hizo. Ukosefu wa huduma za fedha kimtandao zinakuwa kikwazo kwani wananchi hupoteza muda mwingi benki kusubiria malipo ambayo wangaliweza kuyapokea kupitia simu za kiganjani au rununu.  

Wazazi kupeana talaka na msongamano benki vilikuwa shubiri 

Miongoni mwa waliokuwa wanapata machungu kwa kwenda benki kufuata malipo ni Gehad, mwanafunzi huyu wa Chuo kwenye mji mkuu wa Misri, Cairo. 

Gehad anasema “wazazi wangu walipeana talaka miaka 15 iliyopita. Malipo ya masurufu kutoka kwa baba kwenda kwa mama tulianza kupokea miaka mitano iliyopita kupitia Benki ya Nasser.” 

Waliweza kupokea fedha hizo baada ya usaidizi kutoka Wizara ya Mshikamano wa Kijamii. Hata hivyo kulikuwa na changamoto kwa sababu, “nilidamka kuwahi benki. Na nilisimama kwenye mstari mrefu sana. Kwa hiyo siku ya kwenda benki ilikuwa ni siku ngumu sana kwangu.” 

Video ya shirika la Umoja wa Mataifa la mawasiliano, ITU, inaonesha msururu ni mrefu katika Benki ya Nasser; wake kwa waume, halikadhalika vijana wa kiume na wa kike akiwemo Gehad, na pahala pa kuketi, viti ni vichache. Kwa ufupi msongamano ni mkubwa. 

Serikali ya Misri na wadau waondoa changamoto kwa wananchi 

Serikali ya Misri kwa ushirikiano na Benki ya Nasser wakabaini tatizo na hivyo wakaibuka na jawabu. 

Ahmed Khedr, Afisa Mwandamizi kutoka kampuni ya mawasiliano ya simu, Orange anasema, Wizara ya Mshikamano wa Kijamii na Benki ya Nasser waliingia ubia na kampuni ya Orange. Ubia huu umeundwa kuwezesha wateja wa Benki ya Nasser kupokea malipo yao ya masurufu kila mwezi wakiwa nyumbani. Na watapokea ujumbe mfupi kupitia simu yao kwamba umepokea malipo yako na hivyo anaweza kumtumia mtu yeyote fedha, au kulipa malipo yoyote au kutoa fedha kupitia matawi ya Orange, mawakala  au kwenye mashine za kutolea fedha.”  

Ama  hakika ikawa ni nafuu kwa Gehad kwani baada ya kupokea fedha kupitia simu yake anakumbuka hali ilivyokuwa “zamani nililazimika kukosa madarasa ya asubuhi shuleni kwa sababu nililazimika kwenda benki kuchukua fedha. Lakini sasa naweza kupata wakati wowote.” 

Harish Natarajan kutoka Benki ya Dunia anaona haya ni mafanikio makubwa kwa wateja na watoa huduma akisema, “huduma za fedha kimtandao zimeondoa kwa kiasi fulani huduma ya malipo kwa benki kama huduma inayojitegemea. Ila sasa ni hatua moja mbele. Iwapo akaunti yako iko benki, bado unaweza kufanya miamala na akaunti yako kupitia huduma zinazotolewa na mtoa huduma wa tatu.”