Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wakati ni sasa kuhakikisha fistula inakuwa historia ifikapo 2030: UNFPA

Daktari akimfanyia uchunguzi wa kawaida mama mjamzito katika Hospitali Kuu ya Mocuba, jimbo la Zambezia, Msumbiji.
UNFPA / Alfredo Zuniga
Daktari akimfanyia uchunguzi wa kawaida mama mjamzito katika Hospitali Kuu ya Mocuba, jimbo la Zambezia, Msumbiji.

Wakati ni sasa kuhakikisha fistula inakuwa historia ifikapo 2030: UNFPA

Afya

Leo ni siku ya kimataifa ya kutokomeza Fistula moja ya majeraha makubwa na ya kutisha ya wakati wa kujifungua kwa mujibu wa shirika la Umoja wa Mataifa la idadi ya watu na afya ya uzazi UNFPA.

Fistula ya uzazi ni shimo kati ya njia ya uzazi na kibofu cha mkojo au rektamu, inayosababishwa na uchungu wa kujifungua wa muda mrefu, bila kupata matibabu ya wakati, na ya hali ya juu.

Ugonjwa huu huwaacha wanawake na wasichana kwakivujwa na mkojo , kinyesi au vyote na mara nyingi husababisha matatizo ya kiafya ya muda mrefu , msongo wa mawazo, kujitenga na kutumbukia kwenye umasikini.

Takwimu za UNFPA zinaonyesha kuwa asilimia 90 ya mimba zinazohusiana na ugonjwa wa Fistula huishia kuzaa watoto wafu.

Vita dhidi ya Fistula

Maudhui ya mwaka huu ni “Miaka 20 ya vita dhidi ya ugonjwa huu kuna maendeleo lakini hayatoshi, hivyo hatua zinahitajika sasa kutokomeza Fistula ifikapo 2030”

UNFPA inasema kwa bahati mbaya wanawake na wasichana  nusu milioni Afrika Kusini mwa jangwa la Sahara, Asia, Mataifa ya Kiarabu na Ukanda wa Amerika Kusini na Caribbea wanaendelea kuathirika na jinamizi hili licha ya usemi wa Afrika kwa “Jua ahiliwezi kuchomoza na kuzama mara mbili kwa mama mwenye uchungu”

Kwa mujibu wa UNFPA mifumo ya afya na jamii zinapungukiwa katika jitihada za kukomesha fistula ya uzazi.

Ubaguzi wa kijinsia na utengano wa kijamii huleta hatari zaidi, na kusababisha fistula kutokea kwa wingi miongoni mwa wanawake na wasichana maskini, wasio na uwezo na makundi ya waliotengwa.

Nini kifanyike kutokomeza Fistula

UNFPA imesisitiza kuwa wakati huu siku ya kimataifa ya kutokomeza Fistula  ikiadhimishwa juhudi kubwa za kupunguza majeraha na ulemavu wakati wa kujifungua ni muhimu sana kuliko wakati mwingine wowote.

Kwa matiki hiyo shirika hilo limependekeza suluhu tatu na za gharama nafuu za kuzuia Fistula ambazo ni   mosi “Matibabu ya dharura ya wakati na ya kiwango kinachofaa na pia huduma kwa watoto wachanga.”

Pili ,” Mafunzo kwa wataalam wa afya hasa ya ukungwa wakati wa kujifungua”

Na tatu “ Fursa kwa wote ya kupata huduma za kisasa za uzazi wa mpango.”

UNFPA inasema kuwa mifumo ya afya inaweza kupunguza fistula kwa kufuatilia maambukizi, kurekebisha mapengo katika huduma na kuhakikisha upatikanaji wa wafanyakazi wa afya wenye uwezo.

Pia imehimiza kuwa mipango ya kitaifa ya afya lazima kushughulikia ubaguzi wa kijinsia na mambo mengine yanayowafanya wanawake na wasichana kuwa katika hatari zaidi ya vifo vya uzazi na magonjwa.