Skip to main content

Kuvuka eneo la msitu wa Darién ni hatari kwa wahamiaji - IOM 

Romeu Mauricio na mtoto wake wa umri wa miaka mitatu wakivuka eneo la Darien linalotenganisha Colombia na Panama
© UNICEF/William Urdaneta
Romeu Mauricio na mtoto wake wa umri wa miaka mitatu wakivuka eneo la Darien linalotenganisha Colombia na Panama

Kuvuka eneo la msitu wa Darién ni hatari kwa wahamiaji - IOM 

Wahamiaji na Wakimbizi

Shirika la Umoja wa Mataifa la Uhamiaji (IOM) linaongeza juhudi za msaada wa kibinadamu kwenye mipaka ya Colombia, Costa Rica na Panama ili kusaidia wahamiaji wanaovuka kuelekea eneo la kaskazini mwa Amerika hasa kupitia msitu hatari wa Darien unaounganisha Amerika kusini na kaskazini. 

Kwa miaka mingi, jimbo la Darien nchini Panama limekuwa kituo cha kawaida cha kupita kwa wahamiaji wanaotoka kusini mwa Amerika kuelekea kaskazini. Takwimu za hivi karibuni za mwaka huu 2023 zinazidi kwa kiasi kikubwa idadi ya juu ya mwaka 2022, wakati watu 258,000 walivuka mwaka mzima. Kwa mujibu wa Mradi wa Wahamiaji Wasiofahamika waliko, wahamiaji wengi hawana vifaa vya kutosha vinavyofaa kwa safari ya siku mbili hadi kumi na karibu wahamiaji 137 walifariki dunia au kutoweka mwaka jana 2022. Luz Santo ni Afisa Mratibu wa IOM akiwa tu punde amewapokea wahamiaji waliovuka mto Chucunaque anasema, “Katika kituo hiki, tunapokea takriban watu 700 hadi 1,000 kila siku, na tunawapa taarifa za msingi kuhusu huduma zinazopatikana kwa ajili yao katika kituo cha mapokezi cha uhamiaji cha Lajas Blancas, na pia taarifa kuhusu njia." 

Wakati wa safari ndefu msituni, watoto na familia hukabiliwa na aina nyingi za unyanyasaji, ikiwa ni pamoja na unyanyasaji wa kijinsia, unyonyaji, pamoja na ukosefu wa maji salama na chakula, mashambulizi ya wanyama mwitu, na mito inayofurika. Robo tatu ya watu wamejeruhiwa wakiwa safarini, na theluthi moja wamekumbana na aina fulani ya kutendewa vibaya au unyanyasaji, hasa wakati wa kuvuka msitu huo wa Darien, IOM inaeleza. 

Kuanzia Januari hadi Oktoba 2022, zaidi ya wahamiaji 200,000 walivuka Pengo la Darien kuendelea na safari zao.
© UNICEF/Eduard Serra

Miongoni mwa wahamiaji wapya waliowasili ni Luisa Maria Laya, mama raia wa Venezuela anayesafiri na watoto wake wawili na mumewe. Waliuza kila kitu walichokuwa nacho ili kumudu chakula na sehemu ya njia yako kutoka Venezuela walikuwa wanatumia usafiri wa kuomba msaada njiani. Matumaini yao ni kujiunga na familia ambayo tayari inaishi Marekani, “Tulipoanza safari yetu msituni, ilikuwa ngumu kwa sababu mimi, mume wangu na watoto wangu hatukuwa tumeizoea. Ilikuwa ngumu, kali, na hatari kwa maisha yetu. Namshukuru Mungu tumefika salama. Muhimu ni kwamba tulifika hai kwa sababu watu wengi huko wanadhani ni mchezo. Si mchezo, kinachoendelea si mchezo kujitosa kwenye msitu huo. Ni kitu hatari, hatari. Unahatarisha maisha ya watoto wako na yako mwenyewe.” 

Wahamiaji wa zaidi ya mataifa 40 wamevuka eneo la Darién mwaka huu. IOM inaeleza kwamba watu hao wanatoka katika mataifa ya Amerika, Asia na Afrika, kama vile Venezuela, Haiti, Ecuador, China, India, Afghanistan, Cameroon, na Somalia. Wengi wao wanatoka Venezuela lakini pia kumekuwa na ongezeko la idadi ya wahamiaji kutoka Haiti, Ecuador, na China.