Viwango vya joto duniani vitavunja rekodi katika miaka 5 ijayo: WMO
Viwango vya joto duniani vitavunja rekodi katika miaka 5 ijayo: WMO
Hali ya joto duniani huenda ikapanda na kufikia viwango vya juu zaidi katika miaka mitano ijayo, ikichochewa na gesi chafuzi za viwandani na matukio ya asili ya El Niño, kulingana na taarifa mpya iliyotolewa leo na shirika la utabiri wa hali ya hewa duniani WMO.
Taarifa hiyo imesema kuna uwezekano wa asilimia 66 kwamba wastani wa joto duniani karibu na uso wa dunia kati ya mwaka 2023 na 2027, utakuwa zaidi ya nyuzi joto 1.5 ° C juu ya viwango vya kabla ya maendeleo ya viwanda kwa angalau mwaka mmoja.
Mwaka wenye joto zaidi kuwahi kushuhudiwa
Shirika hilo la utabiri wa hali ya hewa duniani limeongeza kuwa pia kuna uwezekano wa asilimia 98 kwamba angalau moja ya miaka mitano ijayo, na kipindi cha miaka mitano, utakuwa na joto zaidi la kuvunja rekodi.
"Kuongezeka kwa joto kwa matukio ya El Niño kunatarajiwa kuendelea katika miezi ijayo na hii itachanganyika na mabadiliko ya tabianchi yanayochochewa na binadamu ili kusukuma kiwango cha joto duniani katika eneo ambalo halijulikani," imesema taarifa.
Kuhusu taarifa hisi Petteri Taalas katibu mkuu wa WMO amesema “Hii itakuwa na madhara makubwa kwa afya, uhakika wa chakula, usimamizi wa maji na mazingira. Tunahitaji kujiandaa.”
Baadhi ya mambo muhimu
• Kwa kawaida, El Niño huongeza viwango vya joto duniani mwaka baada ya kutokea, katika hali hii, hiyo inamaanisha ni mwaka 2024.
• Kuna uwezekano wa asilimia 98 wa angalau moja katika miaka mitano ijayo kushinda rekodi ya halijoto zaidi iliyowekwa mwaka wa 2016, wakati kulikuwa na El Niño yenye nguvu ya kipekee.
• Ongezeko la joto la Arctic ni la juu sana. Ikilinganishwa na wastani wa mwaka kati ya 1991-2020, hitilafu ya halijoto inatabiriwa kuwa kubwa zaidi mara tatu ya hali isiyo ya kawaida inayotarajiwa kimataifa wakati wa kuzingatia majira ya baridi kali tano zinazofuata za ulimwengu wa eneo la Kaskazini.
• Mwenendo wa mvua uliotabiriwa kwa wastani wa Mei hadi Septemba mwaka 2023-2027, ikilinganishwa na wastani wa mwaka 1991-2020, unapendekeza kuongezeka kwa mvua katika Ukanda wa Sahel, Ulaya ya Kaskazini, Alaska na kaskazini mwa Siberia, na kupunguza mvua kwa msimu huu kwenye eneo la Amazon na sehemu za Australia.
Mkataba wa Paris
Mbali na kuongezeka kwa hali ya joto duniani, gesi chafuzi zinazotokana na binadamu zinasababisha joto zaidi baharini na kuongeza tindikali, barafu ya baharini na barafu ya milimani kuyeyuka, kupanda kwa kina cha bahari na hali mbaya zaidi ya hewa.
Mkataba wa Paris umeweka malengo ya muda mrefu ya kuongoza mataifa yote kupunguza kwa kiasi kikubwa utoaji wa gesi chafuzi duniani ili kupunguza ongezeko la joto duniani katika karne hii hadi nyuzi joto 2°C huku ikifuatilia juhudi za kupunguza ongezeko hilo hata zaidi na kufikia nyuzi joto 1.5°C, ili kuepuka au kupunguza athari mbaya na hasara zinazohusiana na uharibifu.
Jopo la serikali mbalimbali kuhusu mabadiliko ya tabianchi linasema kwamba hatari zinazohusiana na hali ya hewa kwa ongezeko la joto duniani ni kubwa kuliko nyuzi joto 1.5 °C lakini chini ya nyuzi joto 2 °C.
Ripoti hiyo mpya iliyolewa kabla ya kongamano la hali ya hewa duniani liytakalofanyika kuanzia Mei 22 hadi Juni 2 ambalo litajadili jinsi ya kuimarisha huduma za hali ya hewa na hali ya hewa ili kusaidia kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.
Vipaumbele vya majadiliano katika kongamano hilo ni pamoja na mpango wa Umoja wa Mataifa wa utoaji wa tahadhari ya mapema kwa wote ili kuwalinda watu kutokana na hali mbaya ya mabadiliko ya tabianchi inayozidi kuongezeka na muundombinu mpya wa ufuatiliaji wa gesi chafuzi ili kufahamisha kuhusu kukabiliana na tabianchi.