Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Watu 460,000 waathirika na mafuriko Somalia UN imeanza kuwasaidia

Mafuriko mapya Somalia yasababisha maelfu kutawanywa (Kutoka Maktaba)
United Nations
Mafuriko mapya Somalia yasababisha maelfu kutawanywa (Kutoka Maktaba)

Watu 460,000 waathirika na mafuriko Somalia UN imeanza kuwasaidia

Tabianchi na mazingira

Mvua kubwa za msimu wa masika zinazonyesha Somalia zimesabisha mafuriko makubwa yaliyoleta uharibifu wa hali ya juu ikiwemo kubomoa nyumba, mashamba kusambaratishwa, mifugo kusombwa na maji huku shule na vituo vya afya vikufungwa kwa muda kwa mujibu wa mashirika ya Umoja wa Mataifa ambayo hivi sasa yanahaha kutoa msaada kwa maelfu ya waathirika wa mafuriko hayo.

Umoja wa Mataifa umesema kwa kushirikiana na serikali uatafanya tathimini ya haraka ya mahitaji kesho Jumanne, kwani makadirio ya awali ya mashirika ya Umoja wa Mataifa na washirika wake yanaonyesha kwamba hadi kufikia sasa “Zaidi ya watu 460,000 wameathirika wakiwemo wanaume, wanawake na watoto 219,000 ambao wametawanywa kutokana na mafuriko hayo.”

Akizungumzia mafuriko hayo mjini New York Marekani wakati wa mkutano na waandishi wa habari hii leo msemaji wa Umoja wa Mataifa Stephane Dujarric amesema “Wenzetu walioko Somalia wamejuza kwamba jimbo la Hirshabelle ni moja ya maeneo yaliyoathirika zaidi kwani matawi ya mto Shebelle yalifurika na kulazimisha maelfu ya watu kukimbilia katika maeneo yenye mwinuko.”

Msaada kwa waathirika

Ameongeza kuwa Umoja wa Mataifa na washirika wake hivi sasa wanatekeleza mpango wa usaidizi wa maandalizi ya kitaifa ya mafuriko, “Lakini tutahitaji fedha ili kukidhi mahitaji yanayoongezeka, kwani mpango wa usaidizi wa kibinadamu Somalia unaohitaji dola bilioni 2.6 hadi sasa umefadhiliwa kwa asilimia 25 pekee.”

Mafuriko mapya yafurusha watu Somalia (Kutoka Maktaba)
United Nations

Shirika la chakula na kilimo la Umoja wa Mataifa FAO wametuma ujumbe mfupi wa maandishi wa tahadhari ya mapema kwa wakulima 5,000 katika jimbo hilo. FAO na washirika wake pia wametoa mifuko ya mchanga, makoleo na vifaa vingine kusaidia kusafisha mifereji ya maji na kupunguza maji ya mafuriko.

Nalo shirika la Umoja wa Mataifa la mpango wa cha duniani WFP pia linatuma tani 17 za biskutiza kutia nguvu na limetoa boti ili kuwafikia watu waliokwama katika maeneo yaliyofurika.

Dujarric amesema “Iwapo mvua zitaendelea kunyesha nchini Somalia na katika nyanda za juu za Ethiopia, tunakadiria kuwa hadi watu milioni 1.6 wanaweza kuathiriwa, huku zaidi ya watu 600,000 wakihama makazi yao. Mvua hizo pia zinaongeza hatari ya milipuko ya magonjwa yatokanayo na maji.”