Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Tunatumia lugha za asili barani Afrika kufundisha Kiswahili - Prof. Mutembei

Mfuko huu mahsusi umeandaliwa kutangaza jinsi tasnia ya habari inavyochangia katika kueneza na kukuza lugha ya Kiswahili duniani.
UN/ Stella Vuzo
Mfuko huu mahsusi umeandaliwa kutangaza jinsi tasnia ya habari inavyochangia katika kueneza na kukuza lugha ya Kiswahili duniani.

Tunatumia lugha za asili barani Afrika kufundisha Kiswahili - Prof. Mutembei

Utamaduni na Elimu

Moja ya vyuo vikuu vya kihistoria barani Afrika, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam – Tanzania, ni moja ya taasisi muhimu zilizochangia kupitia wataalamu wake kufanikisha lugha ya Kiswahili kufikia kutangazwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu Sayansi na Utamaduni (UNESCO) kuwa moja ya lugha za kitamataifa.

Lakini je baada ya hatua hiyo kubwa, taasisi hiyo inafanya nini kuikuza zaidi lugha ya Kiswahili ulimwenguni kote? Profesa Aldin Mutembei Mhadhiri mbobevu wa lugha ya Kiswahili katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ambaye ni mmoja wa walioshiriki katika mchakato wa awali wa kuifanya lugha hii itambuliwe kimataifa anaeleza hatua wanazozichukua. 

Jukumu kubwa tulilonalo sasa hivi ni kukisambaza Kiswahili mahali pengi Afrika. Tunashirikiana na Chuo Kikuu cha KwaZulu Natal ambacho kule kuna Kurugenzi ya Mifumo ya Maarifa Asilia ambayo inaongozwa na Profesa Hassan Kaya. Na yeye pamoja na sisi tumeanzisha mradi mkubwa wa Afrika nzima ambao unafundisha Kiswahili kwa kutumia lugha za asili za Afrika. 

Sasa tunafanya nini? 

Katika nchi mbalimbali tumeanza ufundishaji wa lugha ya Kiswahili kwa kutumia lugha za asili. Kwa mfano Afrika Kusini pale Kwazulu penyewe ufundishaji wa Kiswahili kwa kutumia isiZulu, kule Zimbabwe ufundishaji wa Kiswahili kwa kutumia Kishona. Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo, DRC tunafundisha Kiswahili kwa kutumia ama Lingala au KiCongo au Chiloba. Kwa hiyo tunaendeleza lugha za kiafrika lakini wakati huo huo tunataka lugha hizo zichangie katika kundelea kwa lugha ya Kiswahili. Na kwa kufanya hivyo maana yake tunaondoa ule ugomvi ambao ungweza kutokea (japo si lazima) kati ya wenyeji wenye lugha zao mbalimbali na hawa wanaopelekwa kule kama walimu. Kwasababu walimu wakiwa wanafundisha kwa kutumia lugha za wenyeji maana yake wanaziinua na kuzikuza pia lugha za wenyeji. Hili ni jambo ambalo limekubaliwa mahali pengi kwakweli.  

Walimu wa Kiswahili 

Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kimeshapeleka mwalimu kule Chuo Kikuu cha Cape Town (UCT), amenaza kazi ya kunoa walimu wenzake na pia kufundisha lugha ya Kiswahili. Kwa hiyo mahali kwingi ambako tunakwenda kupitia huo mradi mkubwa ni kufundishakugha ya Kiswahili lakini pia kuwafundisha walimu watakaoendeleza ufundishaji wa wanafunzi lugha ya Kiswahili. Ni kama mpira unaozunguka.  

Kiswahili hata Uarabuni 

Sio tu katika nchi za Afrika ya kusini mwa Jangwa la Sahara bali pia Falme za kiarabu. Kwa mfano wakati fulani nilikuwa katika Chuo Kikuu cha Sharjah na tulianza mpango wa kufindisha lugha ya Kiswahili kwa kutumia lugha ya kiarabu. Mpango huo sasa bado uko kwenye majaribio lakini unaendelea kufanikiwa.