Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UN yatoa wito kwa Taliban kukomesha adhabu kali za kuumiza mwili nchini Afghanistan

Mitaa ya Jalalabad Afghanistan. (Maktaba)
UN Photo/Fardin Waezi
Mitaa ya Jalalabad Afghanistan. (Maktaba)

UN yatoa wito kwa Taliban kukomesha adhabu kali za kuumiza mwili nchini Afghanistan

Haki za binadamu

Utumiaji wa adhabu kali kama ya viboko unaofanywa na mamlaka ya isiyo halali ya nchini Afghanistan unakwenda kinyume na sheria za kimataifa na lazima ukomeshwe, Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini humo (UNAMA), umesema leo Jumatatu. 

"Adhabu kali za kuumiza mwili ni ukiukaji wa Mkataba dhidi ya Mateso na lazima ikome," mkuu wa haki za binadamu wa UNAMA, Fiona Frazer, akisisitiza kwamba Umoja wa Mataifa "unapinga vikali" hukumu ya kifo. 

Ametoa wito kwa mamlaka hiyo isiyotambulika kuanzisha "kusitishwa mara moja" kwa mauaji. 

Kuchapwa na kupigwa mawe 

Katika ripoti mpya, UNAMA ilisema kuwa imeandika "aina mbalimbali za adhabu ya mateso" ziliyotekelezwa na Taliban tangu warudi madarakani tarehe 15 Agosti 2021 baada ya kuiondoa serikali iliyochaguliwa kidemokrasia, "ikiwa ni pamoja na kuchapwa viboko, kupigwa mawe, kulazimishwa." watu kusimama kwenye maji baridi, na kulazimisha kunyoa nywele”. Katika kipindi cha miezi sita pekee, wanaume 274, wanawake 58 na wavulana wawili wamechapwa viboko hadharani. 

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, mfumo wa sheria nchini Afghanistan kwa sasa "unashindwa kusimamia kesi chini ya haki na dhamana ya mchakato unaotazamiwa". 

UNAMA imeonya kuwa kukataa kwa Taliban kutoa leseni kwa mawakili wa utetezi wanawake na kuwatenga majaji wanawake katika mfumo wa mahakama kunaathiri upatikanaji wa haki kwa wanawake na wasichana. 

Kukiuka sheria za kimataifa 

Adhabu kali ya mateso (Corporal punishment) imefafanuliwa kuwa "adhabu yoyote ambayo nguvu ya kimwili inatumiwa na inalenga kusababisha kiwango fulani cha maumivu au usumbufu, hata kama ni nyepesi". 

Marufuku ya utesaji na ukatili, unyama au adhabu ya kudhalilisha inachukuliwa kuwa kanuni ya kimsingi ya sheria za kimataifa, ripoti hiyo imesistiza. 

Ahukumiwa kwa ‘mijeledi 100’ 

Kati ya tarehe 15 Agosti 2021 na 12 Novemba 2022 pekee, UNAMA iliandika angalau matukio 18 ya adhabu ya viboko vilivyotekelezwa na mahakama za mkoa, wilaya na mahakama za rufaa. 

“Katika matukio 18 yaliyoandikwa, wanaume 33 na wanawake 22 waliadhibiwa, wakiwemo wasichana wawili; idadi kubwa ya adhabu, kwa wanaume na wanawake, kuhusiana na uzinzi au ‘kukimbia nyumbani’ na wanawake na wasichana wote walioadhibiwa waliripotiwa kutiwa hatiani kwa makosa hayo,” ripoti hiyo ilionesha. 

Kwa ujumla, adhabu ilikuwa ni viboko 30 hadi 39 kwa kila aliyepatikana na hatia. Hata hivyo, "katika visa vingine, watu waliadhibiwa hadi viboko 80 hadi 100", kwa mujibu wa ripoti hiyo.