Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNICEF yawawezesha wahudumu wa afya wa vijiji Uganda kupambana na malaria

Mjumbe wa timu ya afya ya kijiji VHT, Fenehasi Bazimbana akipatia huduma za afya mtoto wilayani Ntungamo nchini Uganda.
UNICEF Video/Uganda
Mjumbe wa timu ya afya ya kijiji VHT, Fenehasi Bazimbana akipatia huduma za afya mtoto wilayani Ntungamo nchini Uganda.

UNICEF yawawezesha wahudumu wa afya wa vijiji Uganda kupambana na malaria

Afya

Malaria ni moja ya magonjwa hatari zaidi duniani ikielezwa na ripoiti ya mwaka 2022 ya shirika la afya la Umoja wa Mataifa WHO kuwa ilikatili maisha ya watu 619,000 duniani kote mwaka 2021 na waliougua ugonjwa huo kufikia milioni 247. Shirika hilo linasema asilimia kubwa ya vifo na wagonjwa wako barani Afrika hasa Kusini mwa Jangwa la Sahara.

Uganda ni moja ya mataifa yaliyoathirika na ugonjwa huo na wahanga wakubwa ni watoto walio na umri wa chini ya miaka mitano. Kwa kulitambua hilo shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF kwa kushirikiana na wadau limeanzisha program ya kuziwezesha timu za wahudumu wa afya wa vijijini VHT kushiriki katika vita dhidi ya malaria ikiwemo kwenye wilaya ya Ntungamo.

Katika kijiji cha Kabingo kwenye wilaya ya Tungamo nchini Uganda, Mjumbe wa timu ya afya ya kijiji VHT, Fenehasi Bazimbana amepata ujumbe kupitia simu yake ya rununu kwamba katika jamii yake kuna mtoto mgonjwa.

Amekusanya vifaa kwake na haraka anaelekea kwenye nyumba ya Ester Nakachwa aliko mtoto huyo. Nakachwa ni mama wa watoto wanne na watatu kati yao wana umri wa chini ya miaka 5 ambao wako katika hatari kubwa ya kupata magonjwa ikiwemo malaria. Bazimbana anasema, “Tunashughulika na watoto wenye homa, watoto wenye vichomi, Watoto wanaohara na Watoto hao lazima wawe na umri wa chini ya miaka mitano.”

Mjumbe wa timu ya afya ya kijiji VHT, Fenehasi Bazimbana akipatia huduma za afya mtoto wilayani Ntungamo nchini Uganda.
UNICEF Video/Uganda
Mjumbe wa timu ya afya ya kijiji VHT, Fenehasi Bazimbana akipatia huduma za afya mtoto wilayani Ntungamo nchini Uganda.

Fenehasi anampima malaria mtoto anayeumwa kwa kutumia kipimo kinachotoa majibu ya haraka kichulikanacho kama RTD.

Safari hii Nakachwa ana bahati kwani mwanaye hana malaria na Fenehasi anamshauri kumpeleka mtoto kwenye kituo cha afya kwa ajili ya uchunguzi zaidi

Fenehasi ameweza kufika haraka kwa Nakachwa kwa sababu ya msaada wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF ambalo limeziwezesha timu za wahudumu wa afya za kijiji VHT kwa simu za rununu zenye App maalum inayoitwa ‘VHT APP’. App hiyo Inawawezesha wanakijiji kutoa tarifa wanapouguliwa na watoto ili muhudumu afike haraka kuwapima endapo wana malalia na kuchukua hatua zinazopaswa. Fenehasi anasema hali hiyo imesaidia sana kwani, “Mwenendo wa malaria umepungua, kwa sababu unapowapima watoto 10 unawakuta wawili hadi watatu wanayo. Na hii inachangiwa na ushauri tunaowapa walezi wao.”

Na anasisitiza kuwa ushauri huo ni muhimu mfano, “Kuhakikisha unafunga madirisha na milango ifikapo saa kumi na mbili jioni, kulalia vyandarua vya mbu, kukata majani yanayozunguka nyumba na hata kuondoa maji yaliyotuama. Hizo ni sababu kubwa zilizochangia kupungua kusambaa kwa malaria majumbani.”

Mjumbe wa timu ya afya ya kijiji VHT, Fenehasi Bazimbana akipatia huduma za afya mtoto wilayani Ntungamo nchini Uganda.
UNICEF Video/Uganda
Mjumbe wa timu ya afya ya kijiji VHT, Fenehasi Bazimbana akipatia huduma za afya mtoto wilayani Ntungamo nchini Uganda.

Fenehasi ambaye ni babu wa wajukuu saba anafanyakazi kutwa nzima hadi saa 11 jioni baada ya kuwapima watoto kadhaa basi anarejea nyumbani akiwa ameridhika na mchango anaoutoa kwa jamii yake wa kuboresha afya.

Yeye ni miongoni mwa zaidi ya timu ya watu 1000 katika wilaya ya Ntungamo waliopatiwa mafunzo na wizara ya afya kwa msaada kutoka UNICEF na washirika wengine ikiwemo Jumuiya ya Madola ambayo yamewapa ujuzi wa kusaidia jamii katika kudhibiti magonjwa mbalimbali yanayozuilika na kutibika ikiwemo malaria.