Nilinusurika unyanyasaji ili niwasaidie watoto waliotelekezwa wa Eswatini:Siphiwe
Siphiwe Nxumalo, mfanyakazi wa kujitolea wa shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula Duniani WFP huko Eswatini, alirejea nchini mwake baada ya kumaliza masomo yake katika nchi jirani ya Afrika Kusini ili kusaidia yatima na watoto wanaoishi katika mazingira magumu, wanaokabiliwa na umaskini na kutelekezwa.
"Katika jamii hii, watoto wengi hawaendi shule au shule ya awali, kwa sababu hawana chakula. Wengine wengi hawawezi kumudu karo za shule. Siwezi kumudu kuwapeleka watoto wangu shule ya awali kwa sababu mume wangu alipoteza kazi.”
Watoto wengine wanakabiliwa na ukosefu wa upendo wa wazazi. Tumeona watoto waliotelekezwa wakiachwa kutafuta chakula chao wenyewe, na wakiwa katika hatari ya kunyanyaswa kijinsia na watu wazima, ambao wanaweza kuwaambukiza VVU.
Siphiwe anasema hili pia lilinitokea ingawa wazazi wangu hawakunitelekeza nilipokuwa mtoto, nilikabiliwa na dhuluma kutoka kwa watu wazima, wakiwemo majirani, walimu wangu, na mchungaji katika kanisa langu.

Mahala salama kwa watoto
Kabla hatujaunda kituo hiki cha Neighbourhood Care Point jengo hili lilikuwa limejaa wahalifu.
Ilitumika kwa kuhifadhi bidhaa zilizoibiwa, na kuta zilifunikwa na picha zenye jeuri za graffiti.
Tumeunda makazi salama kwa watoto. Baada ya kukarabati muundo na kufungua kituo cha huduma, uhalifu katika eneo hilo ulipungua.
Sisi si walimu wa kitaaluma, lakini tunatumia nyenzo za mtandaoni, kama vile madarasa kwenye YouTube na programu za elimu. Tunataka watoto wakuze mawazo ya ujasiriamali tangu wakiwa wadogo sana, tukiwaonyesha jinsi ya kuepuka uhalifu ulioenea na kujitengenezea fursa.
Milo ya moto, siku tano kwa wiki
Takriban watoto 75 wanakuja kwenye kituo hiki cha matunzo. Hapo awali vituo hivi vililenga watoto chini ya umri wa miaka minane, lakini tunakaribisha watoto wa rika zote, wakiwemo wale ambao wazazi wao hawana uwezo wa kuwapeleka shule, watoto wenye ulemavu, watoto wanaohitaji chakula cha haraka.
Kwa msaada kutoka WFP, tunaweza kutoa milo ya moto, siku tano kwa wiki. Kila mwezi tunaletewa mahindi, maharage, mchele na mafuta. WFP pia ilitupa zana za kilimo, na tumetengeneza bustani ya mboga, ambapo tunalima maharagwe, mchicha, lettuce na mboga nyingine.
“Sikujua, hadi pale marafiki zangu walipobainisha, kwamba mimi huzungumza kila mara kuhusu watoto, na jinsi ya kuwasaidia. Kwa hivyo, niko mahali pazuri. Nimepata wito wangu.”

Eswatini nchi yenye asilimia kubwa ya VVU
Eswatini ina kiwango kikubwa cha maambukizi ya VVU duniani kwani asilimia 27.9 ya watu wazima wanaishi na virusi hivyo, huku asilimia 71 ya watoto ni yatima au walio katika mazingira magumu na mtoto mmoja kati ya wanne amepoteza mzazi mmoja au wote wawili kutokana na VVU/UKIMWI.
• Mayatima na watoto walio katika mazingira magumu wako katika hatari kubwa ya kukabiliwa na ukatili na unyanyasaji, maambukizi ya VVU, utapiamlo, na kupunguzwa kwa upatikanaji wa elimu.
• Vituo vya Matunzo vya ujirani kama hiki cha Siphiwe vinaweza kupatikana kote nchini. Mwaka huu wa 2023, WFP inasaidia vituo 800 vya matunzo haya kwa kupeleka chakula mara kwa mara na pembejeo za kilimo.
• Wafanyakazi wa kujitolea wa ndani huhakikisha kwamba watoto wanapata elimu na huduma za afya zinazohitajika sana, shughuli za burudani na milo yenye lishe.