Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wanahabari tukikatishwa tamaa tunawaangusha wananchi – Waandishi wa habari DRC

Regine Ngamanene Okando (kushoto), mwandishi wa habari wa Radio Canal Rafiki kwenye mji wa Beni jimboni Kivu Kaskazini na Erickson Luhembwe, mwandishi wa habari wa RFI katika majimbo ya Ituri na Kivu Kaskazini nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC…
UN News/George Musubao
Regine Ngamanene Okando (kushoto), mwandishi wa habari wa Radio Canal Rafiki kwenye mji wa Beni jimboni Kivu Kaskazini na Erickson Luhembwe, mwandishi wa habari wa RFI katika majimbo ya Ituri na Kivu Kaskazini nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC wamezungumza na Idhaa ya Umoja wa Mataifa kuhusu changamoto za kuripoti kwenye maeneo hayo yenye mzozo.

Wanahabari tukikatishwa tamaa tunawaangusha wananchi – Waandishi wa habari DRC

Utamaduni na Elimu

Hii leo ikiwa ni siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari duniani maudhui yakiwa Kuumba mustakabali wa Haki: Uhuru wa kujieleza kama kichocheo cha haki zote za binadamu, huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC mapigano ya mara kwa mara yamekwamisha harakati za waandishi wa habari kupatia wananchi haki yao ya msingi ya kupata habari.

Ingawa hivyo waandishi hao, baadhi ya waliozungumza na Idhaa ya Kiswahili ya Umoja wa Mataifa kwenye mji wa Beni jimboni Kivu Kaskazini, mashariki mwa DRC wamesema kutokana na kupenda kazi hiyo na kutokatisha tamaa wananchi wanaowategemea wao kupata taarifa, wanaendelea kufanya kazi hiyo licha ya mazingira magumu.

Kazi yangu ni kipaji na wananchi wanatutegemea

Wakizungumza na George Musubao, mwandishi wa Idhaa ya Kiswahili ya Umoja wa Mataifa huko mjini Beni, jimboni Kivu Kaskaizni waandishi hao wamefunguka kuhusu kile wanachopitia na ni nini wangalipenda kuona.

Mathalani, Erickson Luhembwe, mwandishi wa habari wa Idhaa ya Kiswahili ya Radio international, (RFI) kwenye majimbo ya Kivu Kaskazini na Ituri amesema changamoto ni kwamba hawawezi kuelekea kule ambako anataka kupata habari iliyo kamili.

“Mara nyingi sana tunazungumuza kwa njia ya simu na yule ambaye unangumza naye ndiye atakueleza kile ambacho anahisi au anajitetea au anadhihaki mtu mwiengine,” anafafanua Bwana Luhembwe.

Halikadhalika amesema wanakosa pia kazi ya kufanya kwa kuwa watu wanahamahama kutokana na mapigano na hivyo kuacha vituo vya redio mbali. Na huku waendako hawaajiriwi.

Changamoto nyingine ni ukosefu wa usalama kwani “ukiandika dhidi ya serikali na viongozi wa serikali au mamlaka ya nchi inakusikia umesema kitu tofauti unakuwa matatani, halikadhalika unapozungumza kile ambacho serikali inapendekeza waasi nao wanakusikia vibaya. Hali kama hiyo inatutia katika hali ya sintofahamu hatuwezi tena kuelewa  tunaweza kufanya nini au kutumika tena namna gani ndio mazingira ya utatanishi ambamo tunafanyia kazi.”

Regine Ngamanene Okando, mwandishi wa habari wa Radio Canal Rafiki kwenye mji wa Beni jimboni Kivu Kaskazin nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC amezungumza na Idhaa ya Umoja wa Mataifa kuhusu changamoto za kuripoti kwenye maeneo hayo yenye mzozo.
UN News/George Musubao
Regine Ngamanene Okando, mwandishi wa habari wa Radio Canal Rafiki kwenye mji wa Beni jimboni Kivu Kaskazin nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC amezungumza na Idhaa ya Umoja wa Mataifa kuhusu changamoto za kuripoti kwenye maeneo hayo yenye mzozo.

Wanahabari wanawake tunakumbwa na ukatili wa kingono

Kwa Regine Ngamanene Okando, mwandishi wa habari wa redio Canal Rafiki mjini Beni anaunga mkono hoja ya ukosefu wa usalama akisema, “kuna mahali hatuwezi kufika kwa sababu ya ukosefu wa usalama hapa kwetu Beni. Polisi na jeshi wanatuzuia kwani usalama ni mdogo. Na pia sisi wanawake tunakutana na changamoto za ukatili wa kingono na wakati mwingine tunafanyiwa vitendo hivyo kazini.”

Sikati tamaa kwani naipenda kazi yangu

Bi. Okando alipoulizwa kwa nini bado anapenda kazi hiyo licha ya changamoto anazopitia amesema naipenda kazi yangu kwani ni kazi ambayo nimeichagua na nitaifanya kadri niwezavyo. Pia viongozi kazini wanatutia moyo na hivyo inafaa tubaki katika kazi hii licha ya changamoto.”

Bwana Luhembwe wa RFI anasisitiza kuwa kipaji alichonacho kwenye uandishi wa habari ndicho kinamfanya aamke kila siku kuendelea kuitekeleza jimboni Kivu Kaskazini na Ituri.

Na zaidi ya yote yeye ni raia akisema, ni kwamba  wananchi wanajua fursa ya kuelezea yanayowafika ni kupitia waandishi wa habari, halafu kila mara wananchi wanapotupigia simu na kutaka kutueleza kuna hiki na kile halafu wewe kama mwandishi wa habari haukitangazi, ina maana kwamba wananchi wanaka tamaa mara tena na tena.”

Amesema wao ndio wa kuzungumzia mazuri au mabaya kufuatana na hali halisi ilivyo hivyo “tunalazimika kufanya kazi licha ya kwamba hali si nzuri kiusalama kwetu sisi wenyewe na hata  ndani ya nchi yenyewe.”

Sasa nini kifanyike ili wanahabari DRC wafanye kazi yao kwa amani?

Bi. Okando anasema serikali ya DRC iwaletee amani kwani kwenye usalama watafanya kazi kwa uhuru. Halikadhalika “watulinde zaidi na sisi wanawake ndani ya kazi dhidi ya ukatili wa kingono. Serikali ikitulinda, tutafanya kazi kwa uhuru na watu watapata habari kamili pasipo tatizo.”

Kwa Bwana Luhembwe, suluhu anayoona yeye ni kwa mashirika ya kimataifa zisihi serikali za Afrika kuzingatia uhuru wa vyombo vya  habari. “Endapo hakutakuwepo na chombo kilicho kizito kusihi serikali kuzingatia uhuru huo na kuheshimu sheria, basi kazi yetu sisi waandishi wa habari itakuwa na matata.”