Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ndoa za utotoni zimepungua duniani lakini kasi ni ndogo mno – Ripoti UNICEF

Msichana huyu mwenye umri wa miaka 14 wa Uganda alilazimishwa kuolewa na wazazi wake akiwa na umri wa miaka 8.
© UNICEF/Stuart Tibaweswa Msichana huyu mwenye umri wa miaka 14 wa Uganda alilazimishwa kuolewa na wazazi wake akiwa na umri wa miaka 8.

Ndoa za utotoni zimepungua duniani lakini kasi ni ndogo mno – Ripoti UNICEF

Malengo ya Maendeleo Endelevu

Ripoti ya shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF) imeeleza kwamba vitendo vya ndoa za utotoni vimeendelea kupungua duniani ingawa upunguzaji huo hauna kasi ya kutosha kufikia lengo la kutokomeza ndoa za utotoni ifikapo mwaka 2030 kama yalivyo Malengo ya Umoja wa Mataifa ya Maendeleo Endelevu, SDGs.

Kupitia ripoti hiyo ya UNICEF iliyotolewa usiku wa kuamkia leo Jumatano kwa saa za New York, Marekani, takwimu zinazoonesha kupungua kwa ndoa za utotoni duniani zimechangiwa zaidi na kupungua kwa vitendo hivyo nchini India nchi yenye watu wengi zaidi na ambayo imekuwa ikiukumbatia utamaduni huu.  

Pamoja na kupungua huko kwa vitendo vya kuozesha watoto, UNICEF inasema India inasalia kuwa na idadi kubwa zaidi duniani ya watoto wanaoolewa.  

Tweet URL

Hata hivyo ripoti hiyo inaeleza kuwa ingawa baadhi ya maeneo ya dunia yameshudia kupungua kwa vitendo vya ndoa katika umri mdogo, mataifa mengine yamekwama hasa zaidi katika eneo la Afŕika Maghaŕibi na Kati, kanda inayotajwa kuwa yenye matukio mengi zaidi ya ndoa za utotoni. 

Nchi nyingi katika kanda hii, hasa zile za Sahel, zimekumbwa na migogoro inayoendelea ambayo inazidisha mazingira magumu kwa wasichana. Kanda nyingine yenye maendeleo madogo katika ndoa za watoto ni Amerika Kusini na Karibea. Katika eneo hili, mapungufu makubwa katika makundi ya kijamii na kiuchumi yanaonesha kuwa ndoa za utotoni ni suala lililokita mizizi miongoni mwa jamii maskini. 

Aidha ripoti hii imeeleza kwamba nchi nyingine zaidi ya India ambazo zimeonesha kupunguza ndoa za utotoni ingawa kwa miaka mingi zilishamiri kwa matukio haya ni Bangladesh na Ethiopia huku Rwanda na Maldives zikitajwa kuwa nchi ambazo tangu awali zimekuwa na matukio machache ya ndoa za utotoni na wanakaribia kuvitokomeza kabisa vitendo hivyo. 

Ingawa ripoti inasema kuwa licha ya maendeleo haya kiasi yaliyopatikana kimataifa kasi bado ni ndogo mno na ikiendelea hivi inaweza kuchukua miaka 300 hadi kutokomeza kabisa ndoa za utotoni, Mkurugenzi Mtendaji wa UNICEF, Catherine Russell ana matumaini akisema, "Tumethibitisha kwamba maendeleo ya kukomesha ndoa za utotoni yanawezekana. Inahitaji msaada usioyumba kwa wasichana na familia zilizo katika mazingira hatarishi. Ni lazima kuzingatia kuwaweka wasichana shuleni na kuhakikisha wanapata fursa za kiuchumi."