Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Malaria na changamoto kwa wakazi wa Beni, DRC

Mtoto akipatiwa tiba dhidi ya malaria kwenye kituo cha afya cha Gracia kwenye mji wa Beni jimboni Kivu Kaskazini nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC.
UN News/George Musubao
Mtoto akipatiwa tiba dhidi ya malaria kwenye kituo cha afya cha Gracia kwenye mji wa Beni jimboni Kivu Kaskazini nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC.

Malaria na changamoto kwa wakazi wa Beni, DRC

Afya

Hii leo ikiwa ni siku ya Malaria duniani, huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC, jinamizi la Malaria bado linatikisa taifa hilo ambapo shirika la Umoja wa Mataifa la afya ulimwenguni , WHO, Kanda ya Afrika linasema, asilimia 96 ya wagonjwa wa Malaria duniani kwa mwaka 2022 walikuwa katika nchi 29 ikiwemo DRC.

Akiwa huko mjini Beni jimboni Kivu Kaskazini nchini DRC, mwandishi wa habari wa Umoja wa Mataifa George Musubao alivinjari mjini humo hadi hospitali ya Gracia ambako huko Daktari wa watoto Julien Mathe Kahehere amethibitisha kuwa malaria ni changamoto kubwa kwenye eneo hilo isikumbua sio tu watu wazima bali pia watoto.

Kwa faida ya wasiofahamu Malaria inaambukizwa vipi, Dkt. Kahehere akasema “malaria ni ugonjwa unasababishwa na vimelea aina ya Plasimodium na inaingizwa katika mwili wa binadamu na mbu aitwaye Anopheles.”

Kuhusu madhara amesema kuna madhara mbalimbali lakini la msingi ni kwamba kuna malaria aina mbili ambapo aina ya kwanza ni ile ambayo inampata mtu lakini haitamsonga sana.  “Mwili unauma , kichwa kinauma na anapata homa. Anateseka lakini akipata dawa haraka na nzuri atapona.”

Aina ya pili ni Malaria ambayo vijidudu maradhi vimeingia maeneo mbali mbali ya mwili na madhara yake inategemea vijidudu hivyo kwa wingi sehemu gani. “Mfano kama vijidudu hivyo vingi vimeingia hadi kwenye  ubongo, mtu anaweza kupata degedege au anaweza kupoteza kabisa fahamu.”

Julien Mathe Kihehere ni daktari wa watoto katika Kituo cha Afya cha Gracia kilichoko mji wa Beni, kwenye jimbo la Kivu Kaskazini nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC.
UN News/George Musubao
Julien Mathe Kihehere ni daktari wa watoto katika Kituo cha Afya cha Gracia kilichoko mji wa Beni, kwenye jimbo la Kivu Kaskazini nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC.

Malaria kwa mjamzito huharibu mimba na hudumaza ukuaji wa mtoto

Akaelezea madhara ya Malaria kwa wanawake hasa wajawazito akisema iwapo haitabainika mapema na kutibiwa vizuri, mimba inaweza kuharibika.  “Na kama malaria ikiwa kali sana na kutopata tiba mapema, mtoto anaweza kufariki tumboni. Na iwapo mtoto hatofariki tumboni, kama mama ataugua malaria mara moja, mbili, tatu au mara nne  malaria akiwa mjamzito basi mtoto aliye tumboni hakomai vizuri.”

Dkt. Kehehere akasema ili kuijkinga dhidi ya malaria ni vema mtu ajikinge mbali na mbu anayesambaza malaria kwa kutumia chandarua, “kwa sababu mbu huyu anang’ata mtu nyakati za magharibi au usiku. Kwa hiyo ukitumie chandarua inakuwa njia moja ya kuzuia ugonjwa.”

Shirika la Umoja wa Mataifa la afya ulimwenguni, WHO linasema ugonjwa Malaria unasababisha vifo kwani kila siku watoto 1320 wanakufa kutokana na Malaria.

Halikadhalika husababisha uzito wa mtoto kupungua na mtoto anaweza kudumaa.

Wagonjwa wa malaria wana matumaini na tiba

Katika kituo cha afya cha Gracia, Francoise Mulekya amefika ili kupata tiba ya mtoto wake anayeugua malaria. “Niko hapa kwa sababu mtoto alipata homa, alikuwa hapendi kula na nilipofika hapa nimempima na kuambiwa ana malaria. Hivyo Niko hapa nione anaendelea namna gani.”

Naye Moise Mupila ambaye amelazwa hospitalini kwa sababu ya malaria anasema “nilikuwa nasikia kizunguzungu, sikuwa na hamu ya kula nikaona bora nifike hapa nijue nini kinanipata. Hapa wamenifanyia uchunguzi na kugundua kuwa nina malaria.”

WHO inasema kinachotakiwa sasa ni uwekezaji wa kutosha, ubunifu mpya na utekelezaji wa mipango sahihi ili kutokomeza malaria ifikapo mwaka 2030.

Ripoti hii imeandaliwa na George Musubao, mwandishi wa habari wa UN News huko Kivu Kaskazini nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.