Tabianchi inaendelea kubadilika: Ripoti ya WMO
Tabianchi inaendelea kubadilika: Ripoti ya WMO
Mnamo mwaka 2022, mchakato wa mabadiliko ya tabianchi duniani uliendelea kushika kasi. Haya ni miongoni mwa yaliyobainishwa katika ripoti ya kila mwaka ya Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO), iliyochapishwa hii leo Ijumaa mjini Geneva, Uswisi.
Ripoti ya WMO ya Tabianchi mwaka 2022 inachunguza viashiria muhimu vya tabianchi: kiwango cha gesi chafuzi katika angahewa, mabadiliko ya hali ya joto, kupanda kwa kina cha bahari, joto la bahari na kuongeza tindikali, hali ya barafu ya bahari na barafu. Utafiti huo pia unafuatilia athari za mabadiliko ya tabianchi na kuchambua sababu za matukio ya hali mbaya ya hali ya hewa.
Mwaka 2022, ukame, mafuriko na mawimbi ya joto yameathiri kila bara na kugharimu hasara ya mabilioni ya dola. Barafu ya bahari ya Antarctic imepungua hadi kiwango cha chini kabisa, na kiwango cha kuyeyuka kwa barafu kiasi fulani cha barafu ya Ulaya kimeweka rekodi mpya.
Miaka nane iliyovunja rekodi
WMO inasema kipindi cha kuanzia mwaka 2015 hadi 2022 kilikuwa kipindi cha joto zaidi cha miaka minane kwenye rekodi, licha ya athari ya baridi ya tukio la La Niña katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita. Kiwango cha barafu kinachoyeyuka na kupanda kwa viwango vya bahari, ambavyo vilipiga rekodi ya juu tena mnamo 2022, vinatarajiwa kuendelea kwa maelfu ya miaka.
"Wakati uzalishaji wa hewa chafuzi unaongezeka na tabianchi inapitia mabadiliko makubwa, idadi ya watu duniani inaendelea kuathiriwa sana na hali mbaya ya hewa na hali ya hewa," Katibu Mkuu wa WMO Profesa Petteri Taalas amesema na kuongeza "Kwa hiyo, mwaka wa 2022, ukame wa muda mrefu katika Afrika Mashariki, mvua iliyorekodiwa nchini Pakistani, na mawimbi makubwa ya joto nchini China na Ulaya yaliathiri makumi ya mamilioni ya watu, kusababisha upungufu wa chakula, kuongezeka kwa uhamaji wa watu wengi, na kugharimu mabilioni ya dola."
Wakati huo huo, Profesa Taalas anaamini kuwa ushirikiano kati ya mashirika ya Umoja wa Mataifa umethibitisha ufanisi katika kupambana na athari za kibinadamu zinazosababishwa na hali mbaya ya hali ya hewa na tabianchi, hasa katika kupunguza vifo vinavyohusishwa na hasara za kiuchumi.
Viashiria vikuu vya tabianchi
Wastani wa joto duniani mwaka 2022 ulikuwa 1.15°C juu ya wastani wa mwaka 1850 hadi mwaka 1900. Mwaka 2022 ulikuwa mwaka wa 5 au pengine wa 6 kwa joto zaidi katika rekodi.
Viwango vya angahewa vya hwa kuu tatu za chafuzi - carbon dioxide, methane na nitrous oxide vilifikia rekodi ya juu katika mwaka 2021. Ongezeko la kila mwaka la mkusanyiko wa methane kutoka 2020 hadi 2021 lilikuwa la juu zaidi katika rekodi. Data ya wakati halisi kutoka maeneo mahususi inaonesha kuwa viwango vya angahewa vya hewa hizi tatu chafuzi viliendelea kuongezeka mnamo maka 2022.
Barafu, hali ambayo wataalamu wa WMO hufanya ufuatiliaji wa muda mrefu, imepoteza zaidi ya mita 1.3 ya unene wake katika kipindi cha Oktoba 2021 hadi Oktoba 2022. Upotevu wa wastani wa unene wake tangu 1970 ni karibu mita 30.
Ulimwenguni kote kwa kipindi cha mwaka 1993-2019 barafu imepoteza maji sawa na kama maziwa 75 ya ukubwa wa Ziwa Geneva, kubwa zaidi katika Ulaya Magharibi.
Joto la baharini lilifikia kiwango kipya cha rekodi mnamo mwaka 2022. Takriban asilimia 90 ya nishati iliyonaswa katika mfumo wa tabianchi na hewa chafuzi huishia baharini, kwa kiasi fulani kupunguza viwango vya juu vya kupanda kwa joto lakini kuhatarisha mazingira ya baharini. Kiwango cha ongezeko la joto baharini kimekuwa cha juu sana katika miongo miwili iliyopita.
Kiwango cha wastani cha bahari duniani kiliendelea kupanda mwaka wa 2022, na kufikia kiwango cha juu zaidi cha rekodi. Katika muongo wa kwanza wa kurekodi kwa njia ya satelaiti, kiwango cha ongezeko la kiashiria hiki kiliongezeka mara mbili.
Siku ya Kimataifa ya Mama Dunia
Ripoti hii ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Hali ya Hewa Duniani imetolewa siku moja kabla ya Siku ya Kimataifa ya Mama Dunia 2023. Hitimisho lake kuu linalingana na ujumbe wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres, kwa ajili ya siku hii anaposema, "Tuna zana zote muhimu, maarifa na suluhisho, lakini lazima tuongeze kasi," Guterres anasema akiongeza kuwa "Tunahitaji kuharakisha mwitikio wetu dhidi ya mabadiliko ya tabianchi na kufikia upunguzaji wa ndani na wa haraka wa uzalishaji ili kupunguza ongezeko la joto duniani hadi nyuzi 1.5 za Selsiasi. Pia tunahitaji uwekezaji mkubwa katika kukabiliana na hali hiyo na ustahimilivu, hasa kwa nchi zilizo hatarini zaidi na jamii ambazo zilifanya kidogo zaidi kusababisha shida.”