Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ugonjwa wa chagas wabisha hodi mijini, UNITAID yataka hatua zaidi za kinga

Mdudu anayesambaza kimelea kinachosababisha ugonjwa wa chagas.
© CDC/James Gathany
Mdudu anayesambaza kimelea kinachosababisha ugonjwa wa chagas.

Ugonjwa wa chagas wabisha hodi mijini, UNITAID yataka hatua zaidi za kinga

Afya

Hii leo ikiwa ni siku ya kimataifa ya kuelimisha umma kuhusu ugonjwa wa Chagas, Umoja wa Mataifa unaonesha wasiwasi mkubwa juu ya kusambaa kwa ugonjwa huo hivi sasa kutoka maeneo ya vijijini hadi mijini huko Amerika ya Kusini ambako ugonjwa huu umejikita zaidi.

Shirika la Umoja wa Mataifa la kufanikisha upatikanaji wa dawa na tiba kwa gharama nafuu UNITAID kupitia taarifa yake iliyotolewa mjini Geneva, Uswisi linasema ugonjwa huo unaosababishwa na vimelea viitwavyo Trypanosoma cruzi na kusambazwa na wadudu, unachukuliwa kama ugonjwa wa kimya kwa sababu inaweza kuchukua miongo kadhaa kwa dalili kuonekana, licha ya kwamba kwa sasa unaathiri hadi watu milioni 7 duniani kote.

Mkuu wa Mawasiliano UNITAID, Herve Verhoosel anasema ugonjwa wa chagas unaweza kusababisha mshtuko wa moyo, matatizo ya mishipa ya fahamu na umeng’enyaji wa chakula.

“Ugonjwa huu umejikita katika nchi 21 huko Amerika ya Kusini na unaongoza kwa kuwa chanzo cha vifo vya magonjwa yasababishwayo na vimelea baada ya Malaria,” amesema Bwana Verhoosel.

Upimaji wa chagas bado ni changamoto

Kinachowatia hofu ni kwamba ugonjwa huo awali ulikuwa vijjini lakini hivi sasa umebisha hodi mijini. Kiwango cha kubaini ugonjwa huo ni cha chini sana kwenye mataifa mengi, anasema Afisa huyo wa UNITAID akiongeza kuwa ni asilimia 10 tu ya watu wenye ugonjwa huo wa chagas ndio hufanyiwa uchunguzi na kati yao hao ni asilimia 1 pekee ndio wanapata matibabu kwa ufanisi.

Hata hivyo amesema kwa ubia na wadau wa kikanda na kimataifa, UNITAID inahaha kuzuia maambukizi ya ugonjwa huo kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto aliye tumboni, halikadhalika kuimarisha upatikanaji wa vipimo na matibabu.

Mathalani mradi wa CUIDA ambao ni mpango bunifu wa kimataifa unaomulika katika upimaji, tiba na huduma kwa watu waliokumbwa na ugonjwa wa chagas huko Brazil, Bolivia, Colombia na Paraguay.

Ugonjwa ujumuishwe kwenye huduma za msingi

“Kutatua changamoto ya ugonjwa huu, ni lazima ugonjwa huu ujumuishwe kwenye huduma ya msingi ya afya na kwamab huduma muhimu ziwafikie wale wote wanaohitaji kokote waliko,” anasema Bwana Verhoosel huku akitaja mikakati mingine ya kujumuisha kuwa ni pamoja na huduma ya afya kwa wote, udhibiti wa mazalia ya wadudu, na kila mtu apate huduma za vipimo na tiba,

“UNITAID inatoa wito kwa jamii ya afya duniani kote pamoja na serikali kupatia kipaumbele ugonjwa wa chagas na kusaidia juhudi za kuepusha maambukizi kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto,” amesisitiza afisa huyo wa UNITAID.

Kuhusu ugonjwa wa chagas

Takribani watu milioni 7 duniani kote, wengi wao wakiwa Amerika ya Kusini wanakadiriwa kuwa na kimelea aina ya Trypanosoma cruzi au T-Cruzi kinachosababisha ugonjwa wa chagas.

Kimelea hiki kinasambazwa kwa kung’atwa na mdudu, kula chakula au kupitia damu, halikadhalika kutoka kwa mama mjamzito kwenda kwa mtoto, wakati wa upandikizaji viungo vya mwili au kwenye maabara.