Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Heko Vatican kwa kutupilia mbali nyaraka iliyohalalisha utwaaji wa ardhi ya watu wa jamii ya asili

Mtazamo wa mji wa Vatikani.
UN News/Li Zhang
Mtazamo wa mji wa Vatikani.

Heko Vatican kwa kutupilia mbali nyaraka iliyohalalisha utwaaji wa ardhi ya watu wa jamii ya asili

Haki za binadamu

Mtaalamu huru wa Umoja wa Mataifa kuhusu haki za watu wa jamii ya asili hii leo amekaribisha hatua ya Vatican kutupilia mbali Nyaraka ya Ugunduzi, ambayo ni amri iliyotolewa na kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani zaidi ya miaka 500 ikitumika kuhalalisha wakoloni kutwaa ardhi ya watu wa jamii ya asili.

Mtaalamu huyo José Francisco Calí Tzay amesema nyaraka hiyo inasalia kuwa kidonda kibichi kwa watu wa jamii ya asili na amekaribisha wito wa kiongozi wa kanisa katoliki duniani Papa Francis wa kuachana na fikra za ukoloni na kusongesha kuheshimiana na mazungumzo. 

Kupitia taarifa iliyotolewa leo Geneva, Uswisi na ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Haki za Binadamu, OHCHR, Bwana Calí Tzay ametaka na mataifa mengine yafuate mfano huo wa Vatican na kwamba hoja hii itumike kama njia ya kusaka maridhiano kati ya jamii za asili na nchi zilizotekeleza ukoloni. 

Jamii ya asili ilionekana haina haki ya umiliki kwa madai ya kukosa dini  

“Holy See imechukua hatua muhimu kuelekea maridhiano na kuponya vidonda kwa kukataa fikra zote ambazo zilishindwa kutambua haki zao za urithi za kibinadamu. Nyaraka hiyo ilitambua haki ya msingi kwa wakoloni wazungu kudai umiliki na mamlaka juu ya watu wa jamii ya asili kwenye ardhi na rasilimali zao kwa msingi ya kwamba walikuwa si wastaarabu na hawakuwa na dini,” amesema Calí Tzay. 

Nyaraka hiyo ya kiongozi huyo wa kanisa katoliki duniani ilitumika kudai na kumiliki maeneo ya ardhi ya jamii ya watu wa asili huko Amerika, Afrika na maeneo mengine duniani. 

Hadi sasa nyaraka hiyo inaendela kuwa na madhara ya kuwezesha watu wa jamii ya asili kufurahi haki zao katika baadhi yan chi. 

Kuhusu Nyaraka ya Ugunduzi 

Nyaraka hiyo inapatia msingi wa kisheria wa kuwanyima watu wa jamii ya asili haki ya kumiliki ardhi zao za asili na serikali zinaendelea kutumia nadharia hii ya kisheria kama sheria za kitaifa na kanuni hasa pale linapoibuka suala la migogoro ya ardhi. 

Mtaalamu huyo wa Umoja wa Mataifa amesema nyaraka hiyo ilikuwa ni chanzo kikuu cha kiwewe kinachokumba watu wa jamii ya asili kizazi na kizazi na sasa inajitokeza katika kiwango cha juu cha kujiua miongoni mwa vijana wa jamii ya asili, watu wengi wa jamii ya asili kukumbwa na matukio mengi ya uhalifu,ubaguzi wa rangi na ukatili dhidi ya wanawake na wasichana wa jamii ya asili. 

Mtaalamu huyo huru amesihi nchi ambazo bado zinakumbatia na kutukia nyaraka hiyo zifuate mfano wa Vatican kwa kuifuta na kupitia upya kanuni za kisheria zilizokuwa zinaitegemea.