Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Tuungane kwenye maombi ya amani wakati tukisherehekea Pasaka na Ramadhani - Guterres

Reem Abaza wa UN News akizungumza na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres kuhusu ziara zake za kila mwaka za mshikamano wa Ramadhan.
UN Video
Reem Abaza wa UN News akizungumza na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres kuhusu ziara zake za kila mwaka za mshikamano wa Ramadhan.

Tuungane kwenye maombi ya amani wakati tukisherehekea Pasaka na Ramadhani - Guterres

Amani na Usalama

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ametoa wito kwa watu wa imani zote duniani kote "kuunganisha sauti zao katika maombi ya pamoja ya amani", wakati dunia ikijiandaa kusherehekea sikukuu za Pasaka na Ramadhani.

Guterres ametoa ombi la amani akikiri kwamba "imekosekana" katika sehemu nyingi za dunia, wakati wa mahojiano na Idhaa ya Kiarabu ya Umoja wa Mataifa, wakati huu akijiandaa na ziara yake ya kila mwaka anayoifanya katika kipindi cha mwezi mtukufu wa Ramadhani kwenda kwenye nchi za Kiislamu ambazo zimekumbwa na changamoto.

"Nadhani huu ni wakati wa sisi kuwa na umoja kwa ajili ya amani. Amani ni kitu cha thamani zaidi ambacho tunaweza kuwa nacho duniani”, Guterres alisema.

Amani ya thamani

"Kwa hivyo, huu ni wakati wa kukusanyika pamoja na kwa wale wanaomwamini Mungu katika njia tofauti, kwa usemi tofauti, kujiunga na sauti zao katika maombi ya pamoja ya amani."

Mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa alianza utamaduni wake wa kufanya ziara ya mshikamano wakati wa Ramadhani, wakati akiwa Kamishna Mkuu wa Wakimbizi, katika Shirika la Umoja wa Mataifa linahusika na masuala ya wakimbizi UNHCR - kazi aliyoifanya kwa miaka kumi, kabla ya kuwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa mwaka 2017.

"Wakimbizi wengi walikuwa Waislamu, na jamii nyingi zinazowahifadhi wakimbizi kwa ukarimu mkubwa na mshikamano, walikuwa Waislamu," aliamwambia Reem Abaza wa Idhaa ya Kiarabu, akibainisha kuwa Mkataba wa Wakimbizi wa 1951 juu ya ulinzi wa wakimbizi, unaendana kikamilifu na maadili ya kiroho ya Quran Tukufu.

Tufunge kwa mshikamano

Alisema ziara yake ya kila mwaka katika kambi za wakimbizi au makazi kama mkuu wa UNHCR, ambako alikuwa nayeye anashiriki kufunga kuonesha mshikamano, pia ilitoa fursa ya kuangazia ukarimu unaoonyeshwa na jumuiya zinazowapokea.

"Nilipokuja kuwa Katibu Mkuu, nilidhani kwamba mila hii inapaswa kudumishwa na sasa, sio kulenga jamii za wakimbizi pekee, lakini inalenga jamii za Kiislamu zinazoteseka", alisema.

Sura ya kweli ya Uislamu

Alipoulizwa ni maarifa gani ameyapata tangu kuanza utamaduni wa kujumuika na Waislamu kufunga wakati wa Ramadhani, mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa alisema hali hiyo imemuonyesha, "Sura ya kweli ya Uislamu."

"Hisia ya amani, hisia ya mshikamano, hali ya ukarimu ambayo nilishuhudia katika jumuiya zinazohifadhi wakimbizi, na pia ujasiri wa wakimbizi wenyewe ulikuwa wa kutia moyo sana. Na inasalia kuwa msukumo muhimu sana wa kila kitu ninachofanya leo, kama Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa.”