Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mfuko wa Elimu haiwezi kusubiri kupanua uwekezaji nchini Colombia

Watoto wakichora darasani katika idara ya Arauca, Colombia.
© UNMVC/ Diego Morales
Watoto wakichora darasani katika idara ya Arauca, Colombia.

Mfuko wa Elimu haiwezi kusubiri kupanua uwekezaji nchini Colombia

Msaada wa Kibinadamu

Mfuko wa Umoja wa Mataifa wa kuchagiza elimu kwenye maeneo ya mizozo, Education Cannot Wait, ECW, au Elimu Haiwezi Kusubiri umetangaza nia yake ya kupanua uwekezaji nchini Colombia kwa kuwekeza dola milioni 12 ili uweze kuwafikia watoto wengi zaidi raia wa Colombia na wakimbizi kutoka nchini Venezuela.

Nia hiyo imetangazwa na Mkurugenzi mtendaji wa Mfuko wa Elimu haiwezi kusubiri Yasmine Sherif akiwa ziarani nchini Colombia wiki iliyopita ambako alijionea utekelezaji wa miradi mbalimbali ambayo shirika hilo limetekeleza kwa miaka mitatu.

ECW wametangaza kutenga dola million 12, wakati tayari walishawekeza miradi mbalimbali ambayo inafanya jumla ya uwekezaji nchini humo kufikia zaidi ya dola milioni 28 na kuweza kuwafikia zaidi ya watu 107,000 kwa takwimu zilizoishia mwezi Novemba 2022.

Miradi inayotelezwa wamekuwa wakishirikiana na mashirika ya Umoja wa Mataifa pamoja na wadau wengine na Bi Sherif anasema

“Inafurahisha sana kurejea hapa na kujionea matokeo yaliyofikiwa, kuona jinsi UNICEF, Save the Children, World Vision, Shirika la kimataifa la Plan, na Shirika la kuwasaidia wakimbizi la Norway wnavyofanya kazi bega kwa bega katika kusaidia, maendeleo ya kibinadamu wakishirikiana na serikali ya Colombia.”

Mbali na nchi ya Colombia kuwa na wakimbizi wa ndani milioni 5.6, lakini nchi hiyo pia imewapatia makazi zaidi ya wakimbizi milioni 2.5 kutoka nchi jirani ya Venezuela hali inayoongeza mzigo kwa serikali kwenye kutekeleza haki ya kupata elimu hususan kwa watoto.

Mkurugenzi huyo wa ECW anasema wanatambua jukumu zito lililobebwa na serikali. “Tunajua kuwa serikali ya Colombia kwa ukarimu wake wame wajumuisha Wavenezuela 500,000 katika mfumo wa kitaifa wa umma. Washirika wetu nao wameweza kuwafikia zaidi ya watu 110,000, na sasa sisi Elimu Haiwezi kusubiri tunafuata na mpango wetu ulioboreshwa na wakuweza kusonga mbele zaid maendeleoi.”

Msaada wa haraka wa dola milioni 46.4 zinahitajika nchini Colombia ili kuweza kuziba pengo la ustahimilivu la miaka mingi nchini humo.

Programu zilizotekelezwa nchini Colombia ni pamoja na kuhakikishwa watoto wanafikiwa na elimu rasmi na isiyo rasmi katika mazingira salama, huduma za afya ya akili na usaidizi wa kisaikolojia, huduma maalum za kusaidia mabadiliko ya mfumo wa kitaifa wa elimu kwa watoto walio katika hatari ya kuachwa nyuma wakati wengine wakisonga mbele kielimu, pamoja na hatua mbalimbali za kuimarisha uwezo wa mamlaka za elimu za mitaa na kitaifa ili kusaidia elimu kuanzia ngazi ya elimu ya awali hadi shule za sekondari.