Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Usonji: Umoja wa Mataifa waadhimisha Siku ya Kimataifa ya Uelewa kuhusu hali hii 

Siku ya Uelewa kuhusu Usonji Duniani huadhimishwa na UN kila mwaka tarehe 2 Aprili.
© Unsplash/Annie Spratt
Siku ya Uelewa kuhusu Usonji Duniani huadhimishwa na UN kila mwaka tarehe 2 Aprili.

Usonji: Umoja wa Mataifa waadhimisha Siku ya Kimataifa ya Uelewa kuhusu hali hii 

Haki za binadamu

Leo tarehe 2 Aprili ni Siku ya Uelewa wa kuhusu Usonji Duniani. Katika tarehe hii, Umoja wa Mataifa huadhimisha michango ya watu wanaoishi na usonji na ulinzi wa haki za kujumuishwa kwa kila mmoja wao. 

Katika ujumbe wake kuhusu siku hii ya kimataifa ya Uelewa Kuhusu Usonji, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres anasema kuwa Umoja wa Mataifa umedhamiria kuendeleza haki na kukuza ushirikishwaji wa wale wanaoishi na usonji. 

Uhuru binafsi na heshima 

Kwa Guterres, licha ya mafanikio muhimu, watu wanaendelea kukumbana na vikwazo vya kijamii na kimazingira katika kutumia haki zao kamili na uhuru wa kimsingi. 

Ametoa mfano wa Mkataba wa Haki za Watu wenye Ulemavu na Ajenda ya mwaka 2030 ya maendeleo endelevu. 

Kiongozi huyo wa Umoja wa Mataifa anaamini kuwa kuna mengi zaidi yanapaswa kufanywa ili kukuza elimu-jumuishi, fursa sawa za kazi na uhuru katika mazingira yenye heshima. 

António Guterres pia anaangazia umuhimu wa jukumu la familia na walezi wa watu wanaoishi na Usonji. 

Anaeleza kwamba, sio tu Aprili 2, lakini kila siku, “tunahitaji kutambua michango hai na tofauti ya watu walio na Usonji kwa jamii kote ulimwenguni. 

Mada ya mwaka huu ni “Iangaze Bluu" ambapo katika Umoja wa Mataifa, tukio la mtandaoni leo hii linaangazia michango ya watu wanaoishi na Usonji nyumbani, kazini, katika sanaa na katika uundaji wa sera za umma. 

Mojawapo ya mijadala hiyo imejikita kwenye kile kiitwacho “neurodiversity paradigm”, dhana iliyoanzishwa katika miaka ya 1990 na mwanasosholojia Judy Singer. 

Neurodiversity inaelezea wazo ambalo watu hupitia na kuingiliana na ulimwengu unaowazunguka kwa njia nyingi tofauti; hakuna njia moja "sahihi" ya kufikiri, kujifunza, na tabia, na tofauti hazionekani kama upungufu. 

Pendekezo ni kuondoka kutoka katika simulizi kuhusu uponyaji au kuwabadilisha watu wenye Usonji  na badala yake iwe kuzingatia kukubalika, kuungwa mkono na kujumuika, daima kutetea haki zao. 

Kupitishwa kwa dhana hii kunasaidia wale wanaoishi na Usonji kukuza kujiamini, utu na kuunganishwa kikamilifu katika familia na jamii. 

Siku ya Uelewa Kuhusu Usonji Duniani iliundwa na Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa ili kukabiliana na ubaguzi na changamoto zingine zinazowakabili wale wanaoishi na Usonji. Viwango vya kukubalika vinatofautiana kutoka nchi hadi nchi. 

Tukio hilo la kuiadhimisha siku hii ya kimataifa ya uelewa kuhusu Usonji unaweza kuliona hapa 

TAGS: Usonji, Autism