Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

WFP kupunguza kwa nusu mgao wa chakula kwa wakimbizi Burundi sababu ya ukata

Julienne Irankunda, mkimbizi wa ndani katika kambi ya Gitaza nchini Burundi.
Photo: IOM Burundi / Gustave Munezero
Julienne Irankunda, mkimbizi wa ndani katika kambi ya Gitaza nchini Burundi.

WFP kupunguza kwa nusu mgao wa chakula kwa wakimbizi Burundi sababu ya ukata

Msaada wa Kibinadamu

Shirika la Umoja wa Mataifa la mpango wa chakula duniani WFP limesema halina budi bali kupunguza mgao wa chakula linachotoa kwa wakimbizi nchini Burundi kwa sababu ya ukata unaolikabili shirika hilo.

Katika taarifa yake iliyotolewa leo mjini Bujumbura WFP inasema “Karibu wakimbizi 56,000 kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC, hivi karibuni wataanza kupukea nusu mgao wa chakula wanachikihitaji kutokana na upungufu mkubwa wa fedha za ufadhili kwa ajili ya kukidhi mahitaji ya chakula katika kambi tano nchini Burundi.”

Wengi wa wakimbizi hao wanaotokea Mashariki mwa DRC wanahitaji msaada wa chakula ili kikidhi lishe ya familia zao.

Bila fedha mgao hauepukiki

WFP inasema inahitaji haraka dola milioni 7.1 ili kurejea kutoa mgao wa chakula unaohitajika kwa wakimbizi hao 56,000 kwa kipindi cha miezi sita ijayo.

“Bila fedha hizo kuanzia Aprili Mosi 2023 WFP italazimika kupunguza mgao wa chakula nchini Burundi taifa ambalo linashuhudia mahitaji makubwa ya kibinadamu yanayotokana na kiwango kikubwa cha kutokuwa na uhakika wa chakula, umasikini na kuendelea kumiminika kwa wimbi la wakimbizi kutoka maeneo yenye mizozo.”

Kwa mujibu wa shirika hilo kukatwa kwa mgao wa chakula kutazidisha uhaba wa chakula na hali ya lishe ya wakimbizi na kunaweza kuzidisha mvutano kati ya jamii zinazowahifadhi na wakimbizi karibu na kambi na vituo vya mpito vya wakimbizi hao.

WFP inatoa msaada wa chakula na pia pesa taslimu za kununua chakula katika masoko ya ndani.

Hadi sasa, kila mtu amekuwa akipokea pesa taslimu na au chakula sawa chenye gharama ya dola 0.55 kwa siku, ambazo zimetengwa ili kugharamia mgao kamili wa chakula, ambayo ni kilocalories 2,100 zinazohitajika ili kukidhi mahitaji ya msingi ya chakula na lishe. Sasa Jumla hii itakuwa nusu.

Tunahitaji haraka ufadhili

Akizungumzia uhitaji wa haraka wa fedha za ufadhili katika shirika hilo Housainou Taal, mwakilishi na mkurugenzi wa WFP nchini Burundi amesema "Ingawa tunashukuru kwa msaada uliopokelewa hadi sasa, tunahitaji kwa haraka dola milioni 7.1 kulisha wakimbizi 56,000 kwa mgao kamili unaohitajika kwa muda wa miezi 6 ijayo. Hii ni muhimu ili kukidhi mahitaji ya lishe ya kaya katika kambi na vituo vya mpito vya usafiri nchini Burundi. Wakimbizi wako katika hatari kubwa ya kutopata fursa ya ardhi au kufanya kazi nje ya kambi na wanategemea tu msaada wa kibinadamu kwa ajili ya maisha yao.”

Mwaka jana 2022, kwa msaada mkubwa wa wafadhili na kwa ushirikiano na wahisani na washirika wa maendeleo, WFP ilifikia karibu watu milioni 1 wasio na chakula kote nchini Burundi.

Kati ya hao, asilimia 52 walikuwa wanawake na asilimia 12 walikuwa watu wenye ulemavu.

WFP pia ilitoa tani 11,202 za chakula na zaidi ya dola milioni 6 katika msaada wa fedha taslimu.

Walionufaika ni pamoja na wakimbizi 55,577 wanaohifadhiwa katika kambi tano, Warundi waliorejea kutoka nchi jirani, watu walioathiriwa na athari za kijamii na kiuchumi za coronavirus">COVID-19,  wale walioathiriwa na majanga ya mabadiliko ya tabianchi na waliokimbia makazi yao kutokana na kuongezeka kwa kina cha maji ya Ziwa Tanganyika. Walengwa wengine ni pamoja na watoto wa shule katika maeneo yenye uhaba wa chakula pamoja na wanawake wajawazito na wanaonyonyesha wenye utapiamlo na wasichana na watoto wenye umri wa miezi 6 hadi 59.