Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

CSW67 imenifungua macho, sasa ni kushirikiana kusambaza teknolojia kwenye huduma- LHRC

Getrude Dyabene, Wakili kutoka Tanzania na Afisa wa Dawati la Jinsia katika Kituo cha Sheria na Haki za binadamu nchini humo akizungumza na Idhaa ya Kiswahili ya UN jijini New York, Marekani.
UN News/Selina Jerobon
Getrude Dyabene, Wakili kutoka Tanzania na Afisa wa Dawati la Jinsia katika Kituo cha Sheria na Haki za binadamu nchini humo akizungumza na Idhaa ya Kiswahili ya UN jijini New York, Marekani.

CSW67 imenifungua macho, sasa ni kushirikiana kusambaza teknolojia kwenye huduma- LHRC

Wanawake

Ushiriki wangu katika mkutano wa 67 wa kamisheni ya hali ya wanawake duniani, CSW67 umenifumbua macho ya kwamba pengo la kiteknolojia kati ya wanawake na wanaume si kwa nchi yetu ya Tanzania au bara la Afrika pekee bali pia mataifa mengine ikiwemo Marekani.

Ni kauli ya Getrude Dyabene Afisa Mwandamizi wa Dawati la Jinsia kutoka Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu nchini Tanzania, LHRC wakati akihojiwa na Idhaa ya Kiswahili ya Umoja wa Mataifa, jijini New York, Marekani ili kupata tathmini yake ya mkutano huo.

Bi. Dyabene amesema alishiriki vikao vingi ambako pengo la kidijitali limeshamiri na alitumia fursa hiyo kusaka wadau wa kuweza kushirikiana ili kuondoa pengo la teknolojia kati ya wanawake na wanaume hasa wakati huu wa zama za kidijitali.

Mifumo ya kiteknolojia katika utabibu

Maudhui ya mkutano huo yalikuwa ni vipi teknolojia na uvumbuzi vinaweza kumkwamua mwanamke na msichana katika zama za kidijitali ambapo Bi. Dyabene alitoa mfano wa jambo ambalo ameona linaweza kutumika Tanzania.

“Mfano kuna kikao niliingia kuhusu masuala ya afya. Walitoa mfano ya kwamba kuna mfumo ambapo daktari anaweza kumfikia mgonjwa bila hata mgonjwa kusafiri. Ni kwamba wanakijiji wanapewa elimu kuhusu afya ambapo iwapo wanakijiji wakiwa na mgonjwa wanaingia kwenye mfumo na kutuma taarifa na kisha daktari anakwenda kutoa huduma badala ya kusafiri,” amefafanua Afisa huyo wa LHRC.

Amesema anatambua kuwa mfumo huo si rahisi kulingana na mazingira ya Tanzania, “lakini tukiamua tunaweza kwa sababu mfumo huo hautumii mtandao bali unatumia simu ya kiswaswadu.”

Bi. Dyabene amezungumzia pia kikao alichoshiriki kuhusu mauaji ya wanawake ambako walielezea mfumo wa kutumia namba ya simu ya kuweza kufikisha elimu kuhusu masuala ya ukatili wa kijinsia na halikadhalika kufikisha taarifa haraka kwa wahusika.

Najua Tanzania nasi tuna hizo namba, lakini sasa wao wameweka kwenye mfumo.”

Getrude Dyabene (kulia) Wakili kutoka Tanzania na Afisa wa dawati la Jinsia katika kituo cha Sheria na Haki za binadamu, LHRC nchini humo akihojiwa na Assumpta Massoi wa Idhaa ya Kiswahili ya UN jijini New York, Marekani.
UN News/Selina Jerobon
Getrude Dyabene (kulia) Wakili kutoka Tanzania na Afisa wa dawati la Jinsia katika kituo cha Sheria na Haki za binadamu, LHRC nchini humo akihojiwa na Assumpta Massoi wa Idhaa ya Kiswahili ya UN jijini New York, Marekani.

Serikali pia ziko mstari wa mbele kusongesha wanawake

Mshiriki huyo pia amesema ameona kwa dhahiri jinsi serikali ikiwemo ya Tanzania imesonga mbele katika kuhakikisha inasimamia haki za wanawake ili waweze kufurahia haki zao na vile vile hawaachwi nyuma katika kunufaika na teknolojia ya kidijitali.

“Hii ni mara ya kwanza kwa LHRC kushiriki mkutano huu, hata mimi vile vile na hivyo nimeona ni kwa jinsi gani kuna fursa ya sisi kutumia kupitia watu niliokutana nao na pia niliyojifunza.”

Kuna fursa kwa Tanzania kutumia teknolojia ya kidijitali kusongesha wanawake

Bi. Dyabene amesema anaona kuna fursa kubwa zaidi kwa wanawake kunufaika na teknolojia ya kidijitali sio tu kwenye biashara bali pia kwenye huduma iwe katika afya, na hata kwa kituo chao cha kutoa msaada wa kisheria.

“Sisi kama kituo cha sheria na haki za binadamu tunatoa huduma za msaada wa sheria, kuna hospitali, kuna polisi .Tukiamua kutumia teknolojia kuweza kufikia wale wanaotegemea huduma zetu, itasaidia zaidi kwanza kupunguza gharama na pili kufikisha huduma kwa haraka zaidi.”

Amesema fursa nyingine ni kuangalia jinsi ya kusambaza mitandao ya kijamii kwenye maeneo ya ndani zaidi ili kupunguza pengo la umiliki wa simu na pia utumiaji wa intaneti ili hatimaye ifike kila mahali na watu waweze kufikiwa na huduma za kidijitali.

Pande mbili za fursa za teknolojia ya kidijitali

Bi. Dyabene amezungumzia ukatili na udhalilishaji wa mitandaoni akisema ni jambo ambalo lilijadiliwa kwenye mkutano.

“Elimu tunayotoa katika utumiaji wa mitandao au teknolojia ni kwamba wewe una haki ya kutumia mitandao lakini vile vile una wajibu.”