Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

TANBAT6 watoa msaada wa matibabu na dawa nchini CAR

Mwananchi akipatiwa huduma za matibabu na walinda amani wa Tanzania Kikosi cha TANZBATT6 katika zahanati ya WAPO nchini CAR.
TANZBATT 6/ Capt. Mwijage Iyoma
Mwananchi akipatiwa huduma za matibabu na walinda amani wa Tanzania Kikosi cha TANZBATT6 katika zahanati ya WAPO nchini CAR.

TANBAT6 watoa msaada wa matibabu na dawa nchini CAR

Afya

Mbali na shughuli za ulinzi wa amani chini ya ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kulinda amani nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati MINUSCA, walinda amani wa kikosi cha 6 kutoka Tanzania TANBAT6 wameshiriki huduma ya kutoa matibabu na kukabidhi msaada wa dawa katika zahanati ya WAPO iliyoko mkoa wa mjini Berberati mkoa wa Mambéré-Kadéï.

Kwa kutambua ulinzi wa amani unahusika pia na kusaidia jamii kuwa bora, Mkuu wa kikosi cha TANBAT6, Luteni kanali Amini Setephen Mshana anaendesha kampeni ya afya kwa kuruhusu watabibu wa kikosi hicho kutoa za matibabu katika vijiji vya mkoa wa Mambéré-Kadéï.

Katika Zahanati ya WAPO mjini Berberati, Mganga mkuu wa kikundi cha TANBAT6 kapten Nashiru Bakari Mzego kwa niaba ya Mkuu wa TANBAT6 luteni kanali Amin Stephen Mshana anakabidhi msaada wa dawa za matibabu huku akiwa ameambatana na timu ya matabibu wa kikosi hicho wakiwa tayari kutoa huduma kwa wagonjwa wa kituoni hapo.

“Tupo katika muendelezo wa kampeni ya utoaji wa huduma za afya, awali tulitoa katika zahanati ya POTOPOTO sasa tupo WAPO. Hii ni muendelezo wa utoaji huduma katika maeneo yetu ya uwajibikaji.” Amesema Kapten Nashiru Bakari Mzego ambaye ni Mganga Mkuu wa TANZBAT6.

Kikosi cha TANZBATT6 kikitoa msaada katika zahanati ya WAPO nchini CAR
TANZABATT 6/ Capt. Mwijage
Kikosi cha TANZBATT6 kikitoa msaada katika zahanati ya WAPO nchini CAR

Msaada huo umepokelewa na Mganga mkuu wa zahanati ya WAPO Bi Serastini Masungu ambaye amekishukuru kikosi hicho.

Tunashukuru kwa kutoa matibabu kwa wagojwa kadhaa katika zahanati hii ya WAPO lakini pia tunaomba mumfikishie shukrani za dhati mkuu wa kikosi cha sita toka Tanzania Luteni kanali Amini Stephen Mshana, kazi nyingi tunaziona wanavyosaidia wananchi wa Mambere hasa hii ya kampeni ya Afya kwa wananchi. Kampeni hii tuliona ilianzia Zahanati ya POTOPOTO sasa ni hapa kwetu zahanati ya WAPO asanteni sana walinda amani kutoka Tanzania kwa upendo mnaotuonesha hapa kwetu.”

Taarifa hii imeandikwa na Kapten Mwijage Inyoma wa TANBAT6.