Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Vifo vya wahamiaji Mexico; UN yatuma salamu za rambirambi

Alama kwenye ukuta wa mpaka upande wa Marekani huko Ciudad Juárez, Chihuahua nchini Mexico.
© Unsplash/Alejandro Cartagena
Alama kwenye ukuta wa mpaka upande wa Marekani huko Ciudad Juárez, Chihuahua nchini Mexico.

Vifo vya wahamiaji Mexico; UN yatuma salamu za rambirambi

Wahamiaji na Wakimbizi

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ameeleza masikitiko yake kufuatia vifo vya takribani watu 39 katika kituo cha kushikilia wahamiaji nchini Mexico.

Watu wao wameteketea kwa moto jumatatu usiku kwenye kituo hicho cha uhamiaji kilichoko mjini Ciudad Juarez mpakani na Marekani.

Msemaji wa Umoja wa Mataifa Stéphane Dujarric amesema kupitia taarifa aliyoitoa Jumanne jijini New York, Marekani ya kwamba Katibu Mkuu anatuma salamu za rambirambi kwa familia za wafiwa na wapendwa wao na huku akiwatakia ahueni ya haraka majeruhi.

“Katibu Mkuu anatoa wito wa kufanyika kwa uchunguzi wa kina wa kisa hicho cha kutisha na anasisitiza azma yake ya kuendelea kushirikiana na mamlaka za nchi ambako mienendo mbali mbali ya watu inatokea ili kuhakikisha harakati zao hizo zinakuwa salama, zinasimamiwa kwa kanuni nan jia za uhamiaji zinakuwa zimepangwa,” amesema Katibu Mkuu.

Wakati huu ambapo uchunguzi wa chanzo cha moto huo unaendelea, vyombo vya habari vinadai kuwa moto ulianza baada ya wahamiaji waliokuwa wanahofiwa kurejeshwa makwao kutia moto magodoro yao.